Sh. bilioni 3.1 zatolewa mishahara hewa kwa walimu

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (Utumishi),Celina Kombani.
Serikali imebaini kiasi cha Sh. bilioni 3.1 zimekuwa zikitolewa kama mishahara hewa kwa walimu wa halmashauri mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi),  Celina Kombani, alipokuwa akijibu swali la nyongeza na Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR-Mageuzi), ambaye alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho kimebainika kuwa mishahara hewa kwa walimu.

Aidha, alitaka kujua ni hatua gani ambazo zimechukuliwa na serikali dhidi ya watumishi ambao hawakutenda haki na kulisababishia taifa hasara.

Awali, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho kimelipwa na kiasi gani hakijalipwa kwenye madai ya walimu.Akijibu, Kombani alisema serikali ilibaini kuwapo kwa mishahara hewa ya walimu yenye thamani ya Sh. bilioni 3.1.

Alisema fedha hizo zimerudishwa katika halmashauri husika na tayari halmashauri saba zinahojiwa ili kujua ni kwa namna  gani mishahara hiyo ililipwa kinyume na taratibu.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Selikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri,  alisema madeni ya walimu wote nchini yaliyosilishwa yanayofikia Sh. bilioni 61.7 yakiwamo malimbikizo ya mishahara ya Sh. bilioni 44.17 na yasiyo mishahara Sh. bilioni 17.5.

Mwanri alisema baada ya uhakiki madeni yasiyo mishahara yalikubaliwa na kulipwa kwa walimu walio katika halmashauri Sh. bilioni 5.38.

Alisema Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu, serikali imelipa malimbikizo ya mishahara kwa walimu Sh. bilioni 10.9 kwa walimu 10,974 na kwamba Sh. bilioni 3.4 za walimu 3,504 zimeishahakikiwa na zinasubiriwa kulipwa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم