Benki ya Exim yafungua tawi jipya Lumumba, Dar es Salaam

 
Mmoja kati ya wateja wa Benki ya Exim Tanzania akitoa fedha kutoka katika akaunti yake kupitia mashine ya ATM iliyopo katika tawi jipya la Benki hiyo la Ushirika lililopo katika Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam jana
========  ========  =========
BENKI ya Exim Tanzania imeendelea kutanua wigo kwa wateja wake nchini kwa kufungua tawi jipya lililopo katika mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za Benki hiyo kutoa huduma bora za kibenki kwa kuwafikia wateja wake wote kiurahisi. Tawi hilo la Ushirika linaongeza idadi ya mtandao wa matawi ya Benki ya Exim ambayo yameendelea kusambaa nchi nzima.  

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Operesheni wa Benki ya Exim, Bw. Eugen Masawe alisema kuwa tawi hilo jipya linaipa fursa nyingine benki ya Exim kutoa huduma zake za kipekee za kibenki kwa idadi inayozidi kuendelea kuongezeka ya wateja wake. 

“Tunayofuraha kutangaza kuwa Tawi la Ushirika sasa limefunguliwa rasmi. Hili ni eneo muhimu kwa wateja wetu, kutokana na urahisi wa upatikanaji wa huduma,” alisema Bw. Masawe. 

Alisema kuwa tawi hilo jipya ni uthibitisho pekee wa ukuaji thabiti wa biashara ya benki yake, ongezeko la idadi ya wateja na jitihada zake za kutoa huduma za kipekee kwa wateja wake na jamii yote ya biashara nchi nzima kwa ujumla. 

“Tumekuwa na mkakati wa kumuweka mbele mteja, ambayo umetuwezesha kupeleka huduma zetu pale ambapo pana wingi wa wateja wetu.  “Dar es Salaam kwa kuwa kitovu cha biashara Tanzania, tumeshuhudia ongezeko la wateja wengi ambao uhitaji huduma zetu katika mkoa huu. Tukiwa na matawi zaidi ya kumi jijini, pamoja na huduma mbali mbali za kibunifu, benki ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wateja wake wanakabiliana na ubize wa ratiba zao kwa kupata huduma za haraka na bora za kibenki kutoka Benki ya Exim,” alisema Bw. Masawe. 

Alibainisha kuwa jitihada hiyo ya benki kutanua wigo wake haitoongeza tu mizania ya benki yake kwa kiasi kikubwa na kuongeza idadi ya wateja wake, lakini pia kuhakikisha kuwa benki inayafikia masoko mengine ambayo bado hayajafikiwa nchini.  “Tunampango wa kuendelea kufungua matawi mengine nchi nzima katika siku za usoni. Utekelezwaji wa mkakati huo utaiwezesha benki ya Exim kupeleka huduma zake karibu zaidi na  wateja wake,” aliongeza.

Post a Comment

أحدث أقدم