Mwanasheria Mkuu aonya uendeshaji kesi za madawa ya kulevya na uhujumu uchumi

Jaji Werema
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema amewataka Mawakili wa Serikali Wafawidhi wa mikoa na Wilaya kufuata kanuni na taratibu ili kuhakikisha kesi  za Madawa ya Kulevya na Uhujumu Uchumi zinakamilishwa haraka na haki inatendeka.
“Kuna mambo mengi yanaharibu taswira ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuna malalamiko kwamba hatufanyi vizuri katika uendeshaji wa kesi za Madawa ya Kulevya na  Kesi za Uhujumu Uchumi.  Hatuna sababu za kujitetea.  Tunachopaswa kufanya ni kujisahihisha na kuwa makini wakati tunaposoma majalada ya upelelezi na kuamua kufungua mashtaka.” alisema
Aliwataka kuhakikisha wanatumia weledi wa uwakili katika kuwashauri wapelelezi ili kuwaongoza katika kupata ushahidi utakaowezesha makosa ya jinai kuthibitika Mahakamani
Jaji Werema alitoa kauli hizo jana wakati akifungua mkutano wa mawakili wa serikali wafawidhi wa  mikoa na wilaya.
Alisema wakiwa kama viongozi wana wajibu wa kuwaelekeza na kuwasimamia watumishi walio chini yao na kila mtumishi anapaswa kuzingatia nidhamu mahali pa kazi kwa kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia utumishi wa umma.
“Kuna malalamiko kuwa baadhi mnajihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kuchelewa kazini, ulevi, kuvaa mavazi yasiofaa, kufuta kesi bila kufuata utaratibu, kutojiandaa vyema kabla ya kuendesha mashauri mahakamani, kutoishauri ipasavyo mahakama katika misingi ya haki; na kujihusisha na vitendo vya rushwa” alisema
Alisema kuna taarifa baadhi yao  hawatumii nafasi ya kusoma maoni ya Mawakili vizuri na sehemu nyingine hakuna maoni ya awali ya kushtaki au kutoendelea na mashtaka na hiyo ni kasoro kubwa na ukiukwaji wa maadili ya kazi ya Uwakili wa Serikali.
Jaji Werema alisema kuna umuhimu wa kuweka na kutunza kumbukumbu, taarifa na takwimu sahihi kuhusu utendaji kazi kwani maoni ya awali ni moja ya kumbukumbu muhimu za kutambua weledi wa Mawakili; kujua sababu za kufungua mashtaka au kutoendelea na mashtaka; maoni haya yanarahisisha uendeshaji wa mashtaka kwa yeyote atakayepewa kazi ya kuendesha mashtaka hayo. .
Aliwaonya kuacha kutoa siri za serikali kwani mara nyingi wamejikuta wakishiriki kwenye mitandao ya kijamii bila kujua wanatoa siri za serikali.
“Baadhi yenu mmekuwa mkichangia kwenye mitandao ya kijamii bila kujua mnatoa siri za serikali. Nyie si wasemaji wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali” alisema.
Pia aliwataka Mawakili wa Serikali Wafawidhi, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kumpa ushirikiano Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni ili aweze kutekeleza majukumu yake vyema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka, Biswalo Mganga alisema dhumuni la mkutano huo ni kujadili kwa pamoja na kufanya tathimini ya mafanikio na changamoto wanazopata katika utekelezaji wa majukumu ya divisheni ya mashtaka na mawakili wa Serikali na ofisi zote za  Mikoa na Wilaya.
Alisema uvujaji wa siri za serikali umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwa sababu hiyo na kuangalia asili ya kazi wanazofanya wanapaswa kuwa waangalifu zaisi ili kutojiingiza katika mazingira yoyote yatakayohatarisha usalama wa ofisi zao.
Alisema kutokana na hayo utunzaji wa majalada uteketezwaji wa nyaraka zisizohitajika, mawasiliano na habari za ofisi na mamno mengine yote yanatakiwa yafanyike kwa kuzingatia sheria, utaratibu na kanuni zinazowaongoza.
 Aliwataka kujikumbusha sheria ya usalama wan chi namba 3/1970 kuhusiana na masuala ya utunzaji siri za ofisi.
Source: Sifa Lubasi, HabarileoDodoma

Post a Comment

أحدث أقدم