Escrow Njiapanda, wabunge wagawanyika

Dodoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jana alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuacha wananchi njia panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli kati yake na kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti yake kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo amekuwa mara kwa mara akilipotosha Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo hakukuwa na fedha za umma.
Kamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Singh Sethi na James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine hilo ndilo lilikuwa sababu ya upotoshaji.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo, Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine ingawa katika mjadala wa baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine waliohoji uhalali wa vielelezo alivyotoa.
Kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa kuwa kulingana na mkataba wa PPA kati ya Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa Mei 26, 1995.
“Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji.”
Gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema suala hilo si kweli.
Alifafanua kuwa Tanesco haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yoyote dhidi ya Benki ya Standard Charterd kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa na PAC.
“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na Tanesco na wala siyo Tanesco na IPTL.”
Alisema Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na mkataba wa kibiashara baina yao.
- Soma Zaidi Hapa(Mwananchi)

Post a Comment

Previous Post Next Post