ETI ‘SIWEZI KUISHI BILA YEYE’ KWANI YEYE NANI?

Hakuna shaka tulio wengi tupo katika uhusiano wa kimapenzi wa mashaka. Hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kujiaminisha kwa asilimia mia moja kwamba mpenzi wake aliye naye anampenda kwa dhati kabisa au anazuga. Hii inabaki kuwa siri ya anayependa!
Lakini sasa, kuna kitu nilichogundua miongoni mwetu, kitu ambacho tusipokuwa makini nacho tunaweza kujikuta tunajilazimisha kuishi maisha ya huzuni wakati tunayo haki ya kuishi maisha yenye  furaha.
Ukweli ni kwamba, kila mtu anao uhuru wa kupenda kwani maisha bila mapenzi lazima yatakuwa na kasoro.

Lakini sasa, uhuru huo usikufanye ukalazimika kumpenda mtu ambaye anaonesha wazi kutokuwa na mapenzi kwako. Hivi utampendaje mtu ambaye hakupendi? Sawa, huwezi kujua kwamba hakupendi kwani huwezi kuufungua moyo wake lakini, kuna dalili za wazi zinazoweza kukudhihirishia kuwa, mtu huyo anakuzingua tu na kutaka kukupotezea muda wako.
Kitu kinachoniuma na ambacho ndicho kimenisukuma kuandika makala haya ni tabia ya baadhi ya watu kung’ang’ania wanaume ambao wanaonesha kabisa kutowapenda, ukimuuliza kwa nini anamng’ang’ania wakati hapati anachokitaka, anakuambia eti anampenda sana.
Jamani ifike wakati tutambue kuwa, kutokea kumpenda mtu na yeye akakupenda kwa dhati ni bahati sana. Wengi wetu tunatokea kuwapenda watu wasiotupenda, matokeo yake ni kuumizwa kila wakati.
Wewe jaribu kuchunguza utabaini walio wengi hawapati mapenzi wanayoyatarajia kutoka kwa wapenzi wao badala yake huishia kulizwa kila mara.

Niseme tu kwamba, kanuni ya mapenzi inasema, nipe nikupe, nipende nikupende, niheshimu nikuheshimu. Kama unabaini dalili f’lani f’lani za wazi kwamba mpenzi wako hakupendi, usijilazimishe kuendelea kumpenda. Ukifanya hivyo utamfanya aendelee kukunyanyasa kwa kuwa anajua umeoza kwake na huwezi kumuacha.
Yapi ya kuzingatia?
Huenda wewe unayesoma makala haya sasa hivi unajiamini sana kwamba mpenzi wako anakupenda, hiyo ni nzuri na ndivyo ambavyo kila mtu anatakiwa kuishi.
Tambua kuwa na imani kwamba mpenzi wako anakupenda ndiko kutakufanya uishi maisha ya furaha na amani huku na wewe ukijitahidi kuonesha kumpenda kwa dhati, hapo mtaishi.
Lakini kama unaona penzi la mpenzi wako ni la mashaka ni wakati wako sasa wa kufanya maamuzi sahihi huku ukiamini;

Bila yeye unaweza kuishi
Kumbuka kauli ya ‘siwezi kuishi bila yeye’ ni ulimbukeni kabisa tena watu wakikusikia unasema hivyo watakuona ni mshamba wa mapenzi. Mambo hayo yamepitwa na wakati
Kimsingi unatakiwa kuwa na moyo wa ujasiri kwamba, kama yeye analipiga teke penzi lako wapo wanaolitafuta kwa udi na uvumba na huenda huyo uliyenaye anakuwekea kauzibe tu. Hebu jaribu kupingana na mawazo haya na ujiweke huru. 

Hakuna anayeshikilia pumzi ya mwingine, akikuacha huyo uliyenaye maisha yako yatayumba kwa muda tu kisha utampata mwingine na maisha yako yataendelea wala hutakufa kama baadhi wanavyofikiria!
Fanya maamuzi
Ukweli unabaki palepale kwamba, kumuacha mtu ambaye ulitokea kumpenda sana si kazi ndogo. Ni kazi inayohitaji ujasiri wa hali ya juu. Ifike mahali basi useme, inatosha na amua kumuacha. Potelea mbali ilimradi upate uhuru wa kuishi maisha ya raha mustarehe.

Amini kuwa, huenda Mungu hakukupangia ufurahie maisha na huyo uliyenaye sasa kwa kuwa yule wako aliyekupangia yuko njiani na utasahau maumivu yote.
Naishia hapo kwa leo, tukutane wiki ijayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post