MAELEZO YA
SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA
KATIKA AKAUNTI YA “ESCROW” YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
1.
Historia ya Mradi
Mheshimiwa Spika, Katika miaka ya tisini (1990s), Tanzania ilikuwa
ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali
iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya
kiuchumi na kijamii nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilichukua
hatua za dharura za kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha
Megawati (MW) 100.
2.
Upatikanaji wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Mwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa
Kampuni ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania iliyokuwa na Asilimia 30 na MECHMAR Corporation ya Malaysia (MECHMAR) iliyokuwa na Asilimia 70.
Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) Mtambo wenye uwezo wa
kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala,
Dar Es Salaam.
Katika
Ukurasa wa 52 Aya ya 2, ya Taarifa ya
PAC, Kamati imependekeza Mtambo huo utaifishwe.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mkataba wa PPA kati ya TANESCO na IPTL, majukumu ya IPTL
yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO).
Hivyo, kutaifisha Mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika Mkataba wa PPA wa
tarehe 26 Mei 1995, ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali
katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za
kibiashara za kimataifa. Aidha utaifishaji wa miradi ya uwekezaji
binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza
wawekezaji binafsi
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba
wa PPA kwa muda wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme utakaozalishwa
na IPTL. Kwa mujibu wa Mkataba huo, IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme
usiopungua Asilimia 85 ya uwezo wa Mtambo (minimum
off take). Hata hivyo, uzalishaji wa umeme haukuanza mara moja kutokana na
mgogoro uliotokea kati ya TANESCO na IPTL kuhusu gharama halisi za uwekezaji na
namna ya kukokotoa Capacity Charges.
Hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002. Kutokana na hali
hiyo muda wa miaka 20 ya Mkataba ulianza kuhesabiwa tarehe 15 Januari, 2002
baada ya kuanza uzalishaji (Commercial Operation
Date).
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mengine muhimu yaliyokuwemo katika
PPA, Kifungu Na. 6 cha Mkataba huo kinaipa TANESCO wajibu wa kulipa malipo
yaliyotajwa hapo juu na kwamba endapo kutakuwa na mgogoro wowote kuhusiana na
malipo hayo (Disputed Amount),
itafunguliwa Akaunti maalum (Escrow
Account) ya kuhifadhi fedha hizo hadi pale pande mbili zitakapokubaliana
juu ya uhalali wa malipo yanayobishaniwa. Aidha, chini ya PPA, migogoro yote
kuhusiana na masuala ya utekelezaji wa Mkataba huo ilitakiwa kuwasilishwa na
kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID) ya London. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la kila mhusika katika Mkataba huu
kuwasilisha malalamiko yake ICSID yanapotokea.
Katika Ukurasa wa 8 Aya
ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa mwaka 2004 TANESCO ilifungua shauri la
ICSID 2 kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya Capacity
Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa
hiyo siyo kweli. TANESCO haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au
Mahakama yo yote dhidi ya IPTL kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa katika Taarifa
ya PAC. Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa tarehe 31 Oktoba 2010 na Standard Chatered
Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana
na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika Shauri hilo la ICSID 2 ni
SCBHK na TANESCO na wala siyo TANESCO na IPTL.
Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Februari, 2014 ICSID
ilitoa uamuzi kuhusiana na Shauri la SCBHK na TANESCO na kuwashauri wakae
kukokotoa upya malipo ya Capacity
Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana
na pande hizo kutokuwa na Mkataba wa kibiashara baina yao. Vile vile, kupitia
Shauri la Madai Na. 60/2014, lililofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na IPTL
tarehe 4 Aprili, 2014 ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo.
|
3.
Mgogoro kati ya IPTL na TANESCO
Mheshimiwa Spika, Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza muda
mfupi baada ya PPA kusainiwa tarehe 26 Mei, 1995. IPTL waliitaka TANESCO
wakubaliane bei za kununua umeme kwa kuzingatia gharama za uwekezaji. Pande
hizo mbili zilishindwa kukubaliana gharama za Capacity Charge kwa vile TANESCO walidai kuwa gharama
zilizoainishwa na IPTL ni kubwa kuliko gharama halisi za uwekezaji. Mwaka 1998,
TANESCO iliajiri Kampuni ya Mawakili ya Mkono
& Co. Advocates kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani.
Kutokana na tofauti za gharama za Uwekezaji, Mawakili hawa waliishauri TANESCO
ifungue Kesi ICSID nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia ushauri huo wa Mawakili, TANESCO
ilifungua Kesi Na.ARB/98/8 ya Mwezi Agosti, 1998 ikidai kuwa gharama halisi za uwekezaji
ni Dola za Marekani milioni 90 na siyo milioni 163.53 kama ilivyodaiwa na IPTL.
Aidha, IPTL ilidai kuwa kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ni Asilimia 23.10 ambacho pia
kilipingwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Julai, 2001, ICSID ilitoa uamuzi wa Kesi
hiyo pamoja na mambo mengine kwamba:-
i. Gharama halisi za uwekezaji zikiwemo Mtambo na
nyumba za wafanyakazi wa IPTL zilizoainishwa katika hesabu ya IPTL zilikuwa ni
Dola za Marekani milioni 163.53 lakini ICSID iliona kuwa gharama halisi ni Dola za Marekani milioni 127.20;
ii. Kiwango cha
marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of
Return-IRR) ilikuwa Asilimia
22.31 badala ya Asilimia 23.10 iliyodaiwa na IPTL; na
iii. TANESCO na IPTL wakubaliane mfumo wa malipo ya
kununua umeme ukizingatia gharama halisi za uwekezaji na kiwango cha marejesho
ya uwekezaji (IRR) cha Asilimia 22.31 kwa kutumia financial model iliyokubalika na ICSID.
Katika
Ukurasa wa 11 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa mtaji
wa uwekezaji katika Mtambo wa IPTL ni Shilingi 50,000/= na kwamba huo ndio
ungetumika kukokotoa Capacity Charges ili
kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Maelezo hayo siyo sahihi. Ukweli ni kwamba
kutokana na maamuzi ya ICSID 1 ya tarehe 12 Julai, 2001, gharama za ujenzi wa
Mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.20 kama ilivyoelezwa katika Ukurasa
wa 47 Aya ya 4 ya Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika Taarifa hiyo, pia
imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30. Hii
ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani milioni 89.04 na mtaji ni
Dola za Marekani milioni 38.16. Uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yo yote
au mtu ye yote.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana kwamba fedha iliyopokelewa
kutoka Mabenki ya Ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani milioni
85.86. Kati ya Dola za Marekani milioni 105 zilizokuwa zimeidhinishwa. Swali
la kujiuliza, je Mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 85.86, huku
gharama halisi ya ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani milioni
127.20?
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi
ya Dola za Marekani milioni 38.16 ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji.
Taarifa ya Kamati ya PAC haikuonesha fedha hiyo kuwa sehemu ya uwekezaji.
|
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, Kampuni ya Mawakili
iliyokuwa ikiiwakilisha TANESCO katika kesi ya kwanza ya usuluhishi, Kampuni ya
Mkono & Co Advocates, iliishauri TANESCO iendelee kupinga kiwango cha
malipo ya Capacity Charge kilichokuwa
kimeafikiwa tarehe 12 Julai, 2001 na pande hizi
mbili katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara
(ICSID) ya London. Hii ilikuwa ni miaka miwili tu baada ya usuluhishi
uliochukua miaka minne kukamilika na Mtambo kuanza kuzalisha umeme tarehe 15
Januari, 2002.
Mheshimiwa Spika, Hata
hivyo, baada ya ushauri huu, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates)
hawakuishauri TANESCO ifungue kesi katika Mahakama za Tanzania wala katika
Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICSID) ya London.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 wakati Mheshimiwa
Jaji Utamwa anatoa hukumu yake juu ya mgogoro wa WanaHisa wa IPTL hapakuwepo na
kesi yo yote kwenye Mahakama yo yote ya kupinga
gharama za Capacity Charge kati ya TANESCO na IPTL, iwe katika Mahakama za
ndani au za nje. Kwa kutokuwepo Msuluhishi (Broker)
katika suala hili, madai yo yote ya TANESCO yanakuwa ni madai ya upande mmoja
ambayo kisheria hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo madai halisi. Kwa sababu hiyo haikuwepo formula rasmi ya
kuutatua mgogoro huo zaidi ya majadiliano na maafikiano kati ya pande mbili
(TANESCO na IPTL).
4.
Uuzaji wa Hisa za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na VIP Engineering and Marketing Limited
(VIP) kuona kuwa hainufaiki na ubia wake katika IPTL, ilikusudia kuuza Hisa
zake kwa MECHMAR. Hata hivyo, MECHMAR haikuweza kununua Hisa hizo kwa sababu
ilitaka thamani ya Hisa za VIP zitokane na ripoti ya ukaguzi ya mwaka (Audited Financial Report) na taratibu za
kihasibu za kimataifa (International
Accounting Rules), VIP haikukubaliana na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na kutokubaliana, MECHMAR iliishauri VIP ifungue
Shauri la madai hayo kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Uingereza (LCIA)
kulingana na Mkataba wa Wanahisa wa IPTL. Hata hivyo, VIP haikufungua Shauri
katika Mahakama ya usuluhishi kama ilivyoshauriwa na MECHMAR badala yake tarehe
25 Februari, 2002 VIP ikafungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania
(Miscellaneous Civil Application No. 49/2002) ikiomba Kampuni ya IPTL ifilisiwe
ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuanza uzalishaji.
5.
Uamuzi kuhusu Ufilisi wa IPTL
Mheshimiwa Spika, Shauri lililofunguliwa na VIP tarehe 25 Februari,
2002 liliendelea kuwa Mahakamani hadi ilipofika tarehe 16 Desemba, 2008.
Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jaji Oriyo, J ilitoa uamuzi wa kuiweka IPTL
katika Ufilisi wa Muda (Provisional Liquidation) chini ya Kabidhi Wasii Mkuu
(Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini - RITA). Mfilisi wa Muda alipewa
majukumu maalum yafuatayo:
i.
Kulinda mali zote za
IPTL katika kipindi chote cha Ufilisi wa Muda; na
ii.
Kufanya uchunguzi wa
tuhuma zote zilizotolewa na VIP dhidi ya MECHMAR na kutoa ripoti za uchunguzi
huo ili Mahakama iweze kutoa uamuzi.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 15 Julai, 2011, Mahakama Kuu ya Tanzania
(Kaijage, J) ilitoa uamuzi kwamba, IPTL iwekwe kwenye Ufilisi Kamili (Full
Liquidation) na RITA ilithibitishwa kuwa Mfilisi wa IPTL.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK) iliyokuwa imenunua deni la IPTL
kutoka kwa DANHARTA, ilipinga na kuiomba Mahakama ya Rufaa ifanye mapitio ya
uamuzi wa Mahakama Kuu (Application for Revision – Civil Revision No. 1/2012)
ikiainisha dosari katika uamuzi wa Mahakama Kuu ulioamuru kufilisiwa kwa IPTL.
SCBHK ilibainisha dosari za maombi ya kutaka IPTL kufilisiwa kwa kuwa maombi ya
SCBHK ya kutaka Mahakama iteue msimamizi (Administrator) wa kuisimamia IPTL
(kwa niaba ya SCBHK) yalikuwa hayajasikilizwa.
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana na hoja
za SCBHK na hivyo kuamuru shauri hilo lirejeshwe Mahakama Kuu ili IPTL irudi
mikononi mwa Mfilisi wa Muda (Provisional Liquidator) ambaye alipewa majukumu
yafuatayo:-
i.
Kukusanya mali na
madeni yote ya IPTL;
ii.
Kupokea na kusajili
madeni yote dhidi ya IPTL;
iii.
Kusuluhisha migogoro
kati ya wanahisa wa IPTL; na
iv.
Kusimamia na kuendesha
Mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL kwa niaba ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kuteuliwa, Mfilisi wa Muda (Provisional
Liquidator) alifanya juhudi ya kumaliza mgogoro huo wa IPTL nje ya Mahakama kwa
kushirikisha wadau mbalimbali (Stakeholders) wa IPTL kupitia kikao chake cha
tarehe 9 Novemba, 2011. (Kiambatisho Na.1). Juhudi hizo
hazikufanikiwa na ikalazimu shauri liendelee Mahakamani.
6.
Uhalali wa
uhamishwaji wa Asilimia 70 za Hisa za
MECHMAR
kwenda PAP
Mheshimiwa Spika, Suala la
uhalali wa umiliki wa Hisa katika Kampuni hizi linahusu wanahisa wa Kampuni
wenyewe. Serikali haiwajibiki kuingilia
mahusiano ya kibiashara ya wanahisa katika Kampuni Binafsi.
Hata hivyo, kulingana na Sheria za nchi ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 172 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212), mauziano ya Hisa
yaliyofanyika nje ya nchi yatatambuliwa tu, endapo usajili wa Hisa hizo
utafanyika hapa nchini. Kwa mujibu wa taarifa za BRELA za tarehe 31
Desemba, 2013, zinaonesha kuwa uhamishaji wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL
kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa Asilimia
70 za IPTL.
Katika
ukurasa wa 44 Aya ya 1 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa PAP siyo mmiliki
halali wa Hisa 7 za MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, katika maelezo ya Kamati
ukurasa wa 30, Kamati imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya
MECHMAR na Piper Link zilipokelewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye
mmiliki wa PAP. Kwa uthibitisho huo, Kamati inakubali kuwa Hisa za MECHMAR katika
IPTL zinamilikiwa na PAP.
|
Katika Ukurasa wa 25
Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa hakuna ushahidi wa PAP kumiliki Asilimia
70 ya Hisa zilizokuwa zikimilikiwa na MECHMAR katika IPTL.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge
lako Tukufu kuwa umiliki wa Hisa 7 za IPTL unatambuliwa hata na SCBHK ambayo
ilisaini makubaliano tarehe 25 Novemba, 2011 na PAP ya kulipwa deni la mkopo
wa fedha za kununua deni la ujenzi wa Mtambo wa Tegeta. Kiambatisho Na 2.
|
7.
Majadiliano ya mikopo ya IPTL na Wadai
Mheshimiwa Spika, Kutokana na Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania
iliyotolewa tarehe 5 Septemba, 2013, Kampuni ya PAP ilijadiliana na wadai halali wa mikopo ya IPTL na kuingia Mkataba
wa kuwalipa wadai wote wa IPTL. SCBHK inayodai kuidai IPTL mikopo katika ujenzi
wa Mtambo wa Tegeta haikuwasilisha madai ya aina yo yote ili iweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba, SCBHK iliyokuwa ikiidai IPTL
fedha ilizotumia kununua deni lililotokana na kufilisiwa kwa MECHMAR kule
Malaysia (siyo Tanzania) haijawahi kujadiliana na IPTL kuhusu malipo ya mkopo
wake kama upo. Mvutano huu unaendelea ICSID kati ya TANESCO na SCBHK, ukiitaka
TANESCO ilipe gharama za kununua umeme ikijumuisha deni la IPTL. Madai ya SCBHK
dhidi ya TANESCO yanatokana na madai ya kuwepo kwa Deed of Assignment ya MECHMAR kuhusiana na Mkopo
wa IPTL ambapo Mtambo wa IPTL uliwekwa kama dhamana ya Mkopo.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo Deed
of Assignment hiyo haikuwahi kusajiliwa hapa nchini kama inavyotakiwa
katika Kifungu Na. 172 cha Sheria za Makampuni Sura. 212 zinavyoelekeza.
Kutokana na kutokusajili Assignment Deed
hiyo, SCBHK ilikosa sifa za kufungua
madai yake hapa nchini badala yake ilifungua madai haya ICSID nchini Uingereza.
Kitendo hicho kinaonesha kudharau Mahakama zetu na PAC inataka tuziamini
Mahakama za nje kuliko za kwetu.
8. Jitihada za Makampuni mbali mbali kununua Hisa za VIP
Mheshimiwa Spika, Kutokana na tofauti
zilizokuwepo kati ya MECHMAR na VIP kuanzia mwanzo wa mradi, VIP iliamua kuuza Hisa
zake zilizoko IPTL kwa makampuni mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwemo MECHMAR
kama mwanahisa mwenzake, NSSF, Camel
Oil, Great White Shark Opportunity Fund pamoja na SYMBION lakini haikuwezekana
kutokana na kutoafikiana katika bei.
Mheshimiwa Spika, Baadaye VIP chini ya
usuluhishi ya RITA, iliuza Hisa zake kwa PAP kwa thamani ya Dola za Marekani
milioni sabini na tano (US$ 75,000,000/=). Ununuzi wa Hisa Asilimia 30 za VIP
uliofanywa na PAP ndiyo uliyomaliza mgogoro wa Wanahisa uliyokuwa Mahakamani na
kuufanya Mtambo wa IPTL kumilikiwa na PAP kwa kuwa ndiyo iliyomiliki Hisa zote Asilimia
100 za IPTL.
Taarifa ya PAC: Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa
ya PAC imeelezwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekuwa Dalali Mkuu
aliyewakutanisha Bw. Harbinder Sethi na Bw James Rugemalira
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Taarifa hii siyo sahihi kwa
kuwa tangu tarehe 9 Novemba, 2011, RITA aliitisha mkutano na kuwakutanisha
wadau wote wa IPTL. Wakati huo, Waziri wa Nishati na Madini aliyeko sasa
alikuwa bado hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
|
9.
Kufungua ESCROW Akaunti
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, TANESCO kwa ushauri wa Mkono & Co Advocates walitoa hoja
kuwa gharama za kununua umeme zilikokotolewa kwa kutumia IRR ya Asilimia 23.10
na makadirio ya gharama za mtaji wa Asilimia 30
ambao ni Dola za Marekani milioni 38.16, wakati mtaji halisi (equity) wa IPTL ni chini ya Dola za
Marekani 100. Hivyo, TANESCO walikuwa wakitoa notisi (Dispute Notice) kwa kila Ankara ya malipo kupinga gharama hiyo
kulingana na Kifungu Na. 6.8 cha Mkataba wa PPA. Kifungu hicho kinaeleza kuwa
ikiwa upande wote haukubaliani na usahihi wa malipo katika Ankara
zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi
(Invoice Dispute Notice) kwa upande
mwingine. Vile vile, Mawakili wa TANESCO (Mkono & Co Advocates) walishauri
kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa ajili ya kuhifadhi
fedha ambazo zilitokana na Ankara zilizokuwa zinapingwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ushauri wa Mkono Co. & Advocates tarehe 5 Julai, 2006,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisaini Mkataba wa kufungua
Akaunti Maalum (Escrow Account) kwa
ajili ya kuweka fedha zote za Ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL.
10.
Mmiliki wa Fedha za
Akaunti ya Escrow:
Mheshimiwa
Spika, katika Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 22 imeelezwa kuwa Akaunti ya Escrow ilipaswa kuwa na Shilingi bilioni 306.70 ambazo
zingekuwa zimewekwa na TANESCO. Hata hivyo, katika mapendekezo ya Kamati ya PAC
ukurasa wa 50, Kamati imeeleza
kwamba imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha
katika Akaunti ya Escrow umegubikwa na mchezo mchafu na kwamba Mfumo mzima wa
Serikali ulipata ganzi ili kuwezesha zaidi ya Shilingi bilioni 306 kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania na
kutakatishwa kupitia benki mbili hapa nchini.
11. Tahadhari iliyochukuliwa na Serikali wakati wa
kutoa
fedha kwenye akaunti ya Escrow
Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa kwamba kunaweza kukatokea madai kwa
IPTL, na kwa kuwa Serikali ilitoa dhamana kwa TANESCO ya kununua umeme wa IPTL,
Serikali ilihakikisha inachukua KINGA (Indemnity)
kutoka IPTL katika maeneo yote muhimu. Kwa mujibu wa KINGA hiyo, kama
kutajitokeza madai yo yote yale, IPTL yenyewe itawajibika. Ikumbukwe kuwa kabla
ya kusaini, KINGA hiyo ilipitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
kuthibitisha kwamba inakidhi matakwa ya kulinda maslahi ya Taifa. KINGA hii ilitolewa
tarehe 27 Oktoba, 2013. Inasema, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to
INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and
severally) against all present and future claims, actions and legal
proceedings that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and
expenses the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent
upon the release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part
thereof to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
KatikaUkurasa wa 48 wa Taarifa ya PAC, imeelezwa
kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine
yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya Escrow.
Ufafanuzi
Mheshimiwa
Spika, KINGA iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia
athari yo yote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha
katika Akaunti ya Escrow. Kwa hiyo siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua
tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.
|
12. Dhana ya Madai ya
Shilingi Bilioni 321
Mheshimiwa Spika, Madai ya kwamba
TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa
IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/- kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola
za Marekani milion 38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya
TANESCO imekana kuyatambua madai hayo ya Shilingi
bilioni 321. Kimsingi hata Vitabu
vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havioneshi kuwepo
kwa deni hilo.
Mheshimiwa Spika, Madai ya Shilingi
bilioni 321 yaliyowasilishwa kwa Mfilisi na Mwanasheria wa TANESCO (Mkono
& Co. Advocates) ulihitaji kuhakikiwa kabla ya kukubaliwa na Mfilisi kama
madai halali. Hata hivyo, uhakiki huo haukufanyika kwa sababu ya Hukumu ya
Mahakama ya Rufaa katika Civil Revision
No. 1 ya Mwaka 2012, ambayo ilifuta maamuzi ya Mahakama Kuu ya kuiweka IPTL
katika Ufilisi na kuirudisha kwenye Ufilisi wa Muda. Hivyo, madai hayo ya Shilingi bilioni 321 na kiapo chake ambacho
hakitambuliwi na Bodi ya TANESCO hayakuwa tena na uhalali wo wote.
Kamati ya PAC: Katika ukurasa wa 47 Aya ya 2 Kamati
imejiridhisha kuwa madai ya TANESCO ya Shilingi Billioni 321 yana uhalali japo
usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na
TANESCO na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge.
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika, Madai ya
kwamba TANESCO inaidai IPTL Shilingi bilioni 321 msingi wake ni dhana kwamba
mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Shilingi za Tanzania 50,000/-
kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani milion
38.16 ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta. Aidha, Bodi ya TANESCO imekana
kuyatambua madai hayo ya Shilingi bilioni 321. Kimsingi
hata Vitabu vya Hesabu vya TANESCO ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG,
havioneshi kuwepo kwa deni hilo.
|
13. TANESCO na IPTL kufanya Reconcillation
ya fedha iliyokuwa kwenye Akaunti ya Escrow
Mheshimiwa Spika, TANESCO
kwa kushirikiana na IPTL ilifanya uhakiki (reconciliation)
tarehe 9 Oktoba, 2013 ili kujua madai halali ya IPTL kabla ya kufanya malipo. Takwimu za Mfilisi wa Muda wa IPTL
(RITA) wakati akikabidhi mali na madeni ya IPTL, ilionesha kwamba deni lote
alilokuwa akidaiwa TANESCO na IPTL kama Capacity
Charges ni Shilingi bilioni 370.70,
sawa na Dola za Marekani milioni 224.30. Katika majadiliano kati ya TANESCO na
IPTL, gharama zilizokubaliwa kama Capacity
Charges zilizokuwa zinadaiwa ni Shilingi
bilioni 275.20. Fedha hizi ni pungufu kwa Shilingi bilioni 95.50 ya madai ya IPTL. Hadi kufikia tarehe 25
Novemba, 2013, fedha iliyokuwa katika Akaunti ya Escrow ilikuwa jumla ya Dola
za Marekani milioni 22.20, sawa na Shilingi bilioni 36.72 na Shilingi bilioni
161.39.
Mheshimiwa
Spika, ukaguzi maalum umeonesha pia kuwa fedha zilizokuwa kwenye
Akaunti ya Escrow wakati wa kuifunga ni Shilingi
bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 wa madai ya
IPTL.
14. Iwapo Serikali ilistahili kutoa fedha katika
Akaunti
ya
Escrow wakati Shauri la ICSID, London inaendelea.
Mheshimiwa Spika, Kesi
iliyopo ICSID, London ilihusu madai ya Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong yaliyotokana
na kununua deni lililotokana na uwekezaji katika Mtambo wa IPTL wa Tegeta. Katika Mkopo huo, Mkataba wa kuuziana umeme (PPA)
na Mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta viliwekwa kama dhamana.
Mheshimiwa Spika, TANESCO haikuhusishwa kwenye majadiliano ya
dhamana hiyo. IPTL ilishindwa kumaliza marejesho ya Mkopo huo
na hivyo Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong kuanza kuidai TANESCO madeni
yaliyotokana na Mkopo huo. Hata hivyo, fedha katika Akaunti ya Escrow ilitokana
na Ankara za Capacity Charges zilizokuwa
zikibishaniwa kati ya TANESCO na IPTL kuhusu viwango vilivyotumika kukokotoa malipo hayo na siyo
mikopo ya IPTL.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo,
Standard Chartered Bank Hong Kong siyo
mhusika (not a party) katika Mkataba wa
tarehe 26 Mei, 1995 wa PPA kati ya TANESCO na IPTL. Kwa mujibu wa Sheria za
Tanzania, madai yo yote yaliyotokea nje ya nchi yakihusu uwekezaji ulioko
nchini ni lazima yasajiliwe hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kwa
mantiki hiyo, Shauri lililoko ICSID, London halihusiani na fedha
za Akaunti ya Escrow bali mikopo ya IPTL. Hata hivyo, wadai wa IPTL waliamriwa
na Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 5 Septemba, 2013 kuwasilisha
madai yao kwa PAP. Benki ya Standard Chatered ya Hong Kong haijafanya hivyo.
15. Ulipwaji wa Madai na Madeni
Mheshimiwa Spika, Kuhusu
madai na madeni dhidi ya IPTL ikiwemo VAT, Serikali na BOT ziliitaka IPTL iweke
KINGA (Indemnity) ili kuihakikishia Serikali kuwa endapo
kutakuwa na madai au madeni ya aina yo yote, IPTL itawajibika kuyalipa. Tarehe 27
Oktoba, 2013, IPTL ilitoa KINGA hiyo, nanukuu:
“IPTL do hereby agree to
INDEMNIFY and keep INDEMNIFIED the Government and the Escrow Agent (jointly and
severally) against all present and future claims, actions and legal proceedings
that may arise in respect of and/or all losses, charges, costs, and expenses
the Government and the Escrow Agent may suffer or incur consequent upon the
release and payment of the funds in the Tegeta Escrow Account or part thereof
to IPTL pursuant to the Agreement for Delivery of Funds”.
16. Gharama za Mawakili (Mkono & Co.
Advocates na
Hunton
& Williams ya Marekani) Katika Kuendesha Kesi za IPTL
Mheshimiwa Spika, Hadi Hukumu
ya Mheshimiwa Jaji Utamwa inatolewa tarehe 5
Septemba mwaka 2013, TANESCO na Serikali zilikuwa zimewalipa Mawakili (Mkono
& Co. Advocates na
Hunton & Williams) jumla ya Shilingi
za Tanzania bilioni 62.90 na bado Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates
na Hunton & Williams) wanaidai TANESCO Dola za Marekani milioni 4.50. Katika ushauri wao walikuwa wamependekeza
kwa Serikali wapewe kazi nyingine ya kwenda kutetea Guarantee ya Serikali pamoja na kupinga Hukumu ya tarehe 12 Februari, 2014 iliyotolewa
katika uamuzi wa ICSID-2. Ushauri wao upo katika Memorandum ya tarehe 9 Oktoba, 2013 waliyowasilisha TANESCO.
Mheshimiwa
Spika, Wakati
ambapo hatukujua ni kiasi gani Serikali na TANESCO ingeweza kupata kwa
kuendelea kupinga Capacity Charges za IPTL, tunajua fika ni hasara
gani tumepata kupitia malipo ya Mawakili (Mkono
& Co. Advocates na Hunton & Williams) yaani ya Shilingi bilioni 62.9 na bado wanadai Dola za Marekani milioni 4.5.
Mheshimiwa Spika, kumalizika kwa mgogoro huu wa IPTL si tu
kwamba kumetuondoa kwenye hatari ya kuendelea kukamuliwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) hawa bali pia katika mazungumzo yaliyofanywa kati ya TANESCO na IPTL tumeweza
kuokoa takribani Shilingi bilioni 95 katika madai ya awali ya IPTL.
17. Ushauri wa Mawakili (Mkono & Co.
Advocates na
Hunton
& Williams) wa TANESCO wa Tarehe 4
Oktoba, 2012
Mheshimiwa
Spika, Mawakili wa TANESCO na Serikali yaani Kampuni za Mkono &
Co Advocates na Hunton & Williams waliandika ushauri wa pamoja wa tarehe 4
Oktoba, 2012 ambapo walifafanua kwa kina juu ya Shauri
lililokuwa likiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro
ya Kibiashara (ICSID) ya London. Katika Ushauri wao walionyesha wazi kwamba
TANESCO ilikuwa na nafasi finyu mno ya kushinda katika Kesi iliyokuwa
ikiendelea kati ya TANESCO na SCBHK.
Mheshimiwa
Spika, katika ushauri wao walieleza mambo muhimu ambayo ni vema
Bunge lako Tukufu likayaelewa hasa kwa ajili ya watu wanaodhani kwamba ilikuwa
ni makosa kwa TANESCO kukaa na IPTL baada ya Hukumu ya Mahakama Kuu ya tarehe 5
Septemba, 2013. Baadhi ya maeneo walioshauri TANESCO ikae na IPTL kujadiliana
kwa kile kilichoelezwa na Mawakili (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) kuwa uwezekano wa kushinda kesi ni mdogo ni pamoja na:-
18. Ushauri wa Mawakili unaokinzana
Mheshimiwa Spika, tarehe 4
Oktoba, 2012, Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton
& Williams) walitoa ushauri kwamba, kwa
kuzingatia utetezi walioutoa kwa TANESCO kwenye kesi hii kule ICSID, London
kiasi cha chini kabisa kinachoweza kuidhinishwa na Mahakama ya ICSID, London kama
malipo ya Capacity Charges kwa IPTL ni kati ya Dola za Marekani milioni 85
hadi 90 na Mawakili wetu (Mkono & Co. Advocates na Hunton &
Williams) wakasema, nanukuu, “This
could be considered TANESCO’s Best Case
Scenario”. Hata hivyo waliendelea kusema “This best Case Scenario is
overly optimistic”
Mheshimiwa
Spika, katika
maelezo yao mengine ya tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili hawa (Mkono & Co.
Advocates na Hunton & Williams) wanasema,
“In
these circumstances, SCBHK may recover 100% of its claimed
damages of USD 130 milion even if substantially TANESCO prevails on a portion
of its equity defense”.
Kwa lugha nyingine Mheshimiwa Spika Mawakili hawa (Mkono
& Co. Advocates na Hunton & Williams) wanasema kiasi cha chini kabisa ambacho
TANESCO ingedaiwa na SCBHK kingekuwa Dola za
Marekani milioni 130 bila kujumuisha gharama nyingine za moja kwa moja kwa
IPTL.
Mheshimiwa Spika, Katika
majumuisho yao ya tarehe 4 Oktoba, 2012, Mawakili (Mkono & Co. Advocates na
Hunton & Williams) waliishauri TANESCO ikae na SCBHK na kukubaliana nje ya Mahakama
na kumlipa Dola za Marekani kati ya milioni 75 na milioni
90 na kiasi kitakachobaki kikidaiwa kilipwe kwa
wadai wengine, wakiwemo IPTL, Law
Associates na Kampuni ya Mafuta ya TOTAL.
Mheshimiwa
Spika, Kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 kwa mujibu wa Taarifa ya Mfilisi (RITA), ilionesha
kuwa Kampuni ya IPTL ilikuwa ikiidai
TANESCO zaidi ya Dola za Marekani milioni
224.30, sawa na Shilingi bilioni
370.70. Majadiliano yaliyofanyika kati ya TANESCO na IPTL tarehe 9 Oktoba,
2013 yaliwezesha kukubaliana kuwa malipo stahiki kwa IPTL ni jumla ya Dola za Marekani milioni 166, sawa na Shilingi bilioni 274.56. Kati ya hizo,
Dola za Marekani milioni 121, sawa
na Shilingi bilioni 220.13 zilikuwa
kwenye Akaunti ya ESCROW na Dola za Marekani milioni 45, sawa na Shilingi bilioni 74.43 zitalipwa kwa
kipindi cha muda mrefu usiozidi miaka mitano.
19. Kama
fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni za Umma
Katika ukurasa wa 58 wa Taarifa ya PAC imeelezwa
kuwa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow zilikuwa za Serikali.
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika, Huu si
ukweli zipo sababu kuu zinazothibitisha kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.
1.
TANESCO ilikuwa inapata huduma ya umeme
bila kulipa moja kwa moja IPTL, lakini ikawa inapeleka fedha hizo katika
Akaunti ya Escrow.
2.
TANESCO ilisimamisha kupeleka malipo kwenye
Akaunti ya Escrow na wala kulipa IPTL kuanzia tarehe 30 Oktoba, 2010.
Pamoja na kutokulipa, TANESCO iliendelea kupata huduma ya
umeme kwa kadri ilivyohitaji kutoka IPTL.
Mheshimiwa
Spika, katika Ukurasa
wa 36 hadi 42 wa Taarifa ya
Ukaguzi Maalum ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo
tumekabidhiwa inaonesha kiasi ambacho TANESCO inadaiwa na IPTL.
Mheshimiwa
Spika, Kulingana na Taarifa hiyo ukurasa
wa 36 hadi 42 imeonesha kuwa
kiasi ambacho kilipaswa kuwekwa kwenye Escrow Account kwa mujibu wa Ankara za
IPTL ni Shilingi bilioni 306.68. hata
hivyo, kwa mujibu wa Ukaguzi huo fedha zilizokuwa kwenye Akaunti wakati wa kuifunga ni Shilingi bilioni 182.77 na kuwa na upungufu wa Shilingi bilioni 123.90 ikiwa ni deni ambalo TANESCO bado wanadaiwa
na IPTL.
Mheshimiwa
Spika, Kwa msingi huo fedha zote zilizokuwa kwenye
Akaunti ya Escrow ni mali ya IPTL na IPTL kama Wakala wa Kodi anastahili
kudaiwa na mwisho kulipa kodi yo yote ambayo hajalipa.
Kwa
msingi huo, Taarifa ya PAC haisemi ukweli kuhusu fedha zilizowekwa katika
Akaunti ya Escrow kuwa ni fedha za umma.
|
Mheshimiwa
spika, ili kuthibitisha kwamba fedha hizi siyo za Umma, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wake wa Hesabu za
TANESCO wa tarehe 31 Desemba, 2012 alielekeza kutoa fedha za Escrow kwenye
Vitabu vya Hesabu vya TANESCO na kupunguza deni kwa kiasi hicho hicho kwa
maelezo yafuatayo:
“As a result, the deposit balance
in Escrow account does not meets the definition of an asset of the Company and
therefore an adjustment has been made to de-recognize the asset and related
liability to the tune of the amounts available in the Escrow account”.
20. Iwapo kwa mujibu wa Mkataba wa PPA TANESCO na IPTL
walilazimika kutumia Mtaalamu wa Upatanishi (Mediation Expert) katika utatuzi wa
mgogoro kabla ya kutolewa fedha zilizopo kwenye Akaunti ya Escrow.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati ya PAC ukurasa wa 9, imeeleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa PPA, TANESCO na IPTL walipaswa
kutumia Mtaalam wa Upatanishi katika mgogoro wa Capacity Charge.
Mheshimiwa Spika,
tunapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 18.1 ya Mkataba
wa PPA, wahusika wa Mkataba huo ambao ni TANESCO na IPTL wanatakiwa kwanza
kumaliza mgogoro baina yao kwa njia ya upatanishi (amicable settlement). Iwapo watashindwa kufikia makubaliano ndipo
watalazimika kutumia Mtaalam wa Upatanishi kutatua mgogoro huo. TANESCO na IPTL
walimaliza mgogoro baina yao kwa njia upatanishi kwa kufanya uhakiki wa kiasi
ambacho kila upande ulikuwa unastahili kulipwa katika Akaunti ya ESCROW kabla
ya akaunti hiyo kufungwa. Kwa msingi huo, hapakuwa na sababu ya kutumia Mtaalam
wa Usuluhishi kama ilivyoelezwa katika Taarifa ya PAC.
21. Kama muda wote wa Mkataba wa TANESCO na IPTL
hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji
Mheshimiwa Spika,
taarifa ya PAC inaeleza kuwa hapakuwahi kuwa na Kamati ya Uendeshaji kwa
kipindi chote cha Mkataba wa PPA. Ukweli ni kwamba, Kamati ya Uendeshaji
iliundwa kabla ya kuanza uzalishaji wa Mtambo hapo 2002 na imeendelea kuwepo
hadi leo. Kamati hiyo ina wajumbe sita.
Wajumbe watatu kati ya hao wanatoka TANESCO. Wajumbe watatu waliobakia wanatoka
IPTL. Wajumbe wa TANESCO walikuwa ni kama ifuatavyo:
1.
Mhandisi Masanyiwa
Malale;
2.
Mhandisi Christian
Msyani; na
3.
Mhandisi James Mtei.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo si kweli kwamba Kamati ya
Uendeshaji haikuundwa kama ilivyoelezwa na Kamati ya PAC katika ukurasa wa 10.
22. Wizara
kutambua Hati za Hisa za Makampuni
Mheshimiwa
Spika, katika ukurasa
wa 27 wa Taarifa ya Kamati ya PAC, Kamati hiyo imeitaka Wizara ya Nishati
na Madini kutambua usajili wa Hati za Hisa za Makampuni. Tunaomba ieleweke kuwa
siyo majukumu ya Wizara kutambua na wala kujishughulisha na Hati za Hisa za
Makampuni Binafsi. Aidha, katika ukurasa
wa 45, imeelezwa kwamba “Waziri wa Nishati na Madini ndiyo Mamlaka ya
kuthibitisha uhamishaji wa umiliki wa Kampuni katika sekta yake”.
Ningependa kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba jukumu hilo pia siyo la Wizara
ya Nishati na Madini ni vizuri majukumu ya Wizara yakaangaliwa vizuri na
kutoleta mkanganyiko na kuwadanganya wananchi wetu. Hii inaonesha kuwa kamati
haikupitia vizuri majukumu ya Wizara.
Mheshimiwa
Spika, katika Taarifa ya PAC, ukurasa wa 30 Aya ya 2, imeelezwa nanukuu “nilishuhudia nyaraka kwamba Piper Link ilinunua Hisa za MECHMAR na
katika mauziano hayo Kampuni hiyo iliwakilishwa na Bw. Harbinder Singh Sethi
hivyo huyu bwana ndiye Piper Link na ndiye PAP”. Kwa maneno haya ya Kamati
ya PAC, aliyekuwa na hati za Piper Link ni Bw. Sethi na aliyenunua Piper Link ni
Bw. Sethi anayemiliki PAP. Kwa kuzingatia maelezo haya ya kamati ya PAC,
inaonesha kwamba hakuna tatizo la uhamishaji wa Hisa Asilimia 70 kwenda kwa
PAP.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na maelezo ya Aya iliyotangulia, bado
Kamati ya PAC ukurasa 44 wa taarifa yake,
inaonesha kuwa Hisa hizo zinashikiwa na Martha Renju huko BVI lakini Martha
Renju amefungua kesi mara mbili Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutumiwa na SCBHK
akiwa na lengo la kutaka kujipatia fedha za Escrow bila uhalali. Hata hivyo,
amekuwa akiziondoa kesi hizo mahakamani.
23. Mikutano ya Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO
Mheshimiwa
Spika, katika ukurasa wa 29 wa Taarifa ya PAC,
inasema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilifanya mikutano miwili mfulilizo
kati ya tarehe 16 na tarehe 19 Septemba, 2013 na kwamba uharaka huo unatia
mashaka kwamba kulikuwa na njama.
Mheshimiwa
Spika, muda wa siku 3 kwa Bodi kukutana si jambo la kutiliwa
mashaka kwani Bodi haikutani kwa ajenda moja tu. Napenda kulijulisha Bunge lako
Tukufu kuwa tarehe 16 Septemba, 2013 hapakuwa na kikao cha Bodi isipokuwa kikao cha Bodi kilifanyika tarehe 19
Septemba, 2013. Hivyo si sahihi kusema kuwa Bodi ya TANESCO ilikuwa ina njama
katika kushughulikia na kulitolea maamuzi suala la Akaunti ya Escrow na kwamba
ilikutana ndani ya siku tatu.
24. Hoja ya Mwanasheria wa TANESCO Kufukuzwa Kazi
Mheshimiwa
Spika, katika ukurasa wa 30
wa Taarifa ya PAC kuna hoja kuwa Mwanasheria wa TANESCO kwa wakati huo Bw.
Godwin Ngwilimi aliagizwa na TANESCO kwenda Malaysia kufanya Due Diligence ya Kampuni ya MECHMAR
Corporation na kwamba taarifa hiyo ya Due
Diligence ilifikishwa katika Bodi na Bodi iliipuuza na kinyume chake
Mwanasheria huyo aliachishwa kazi.
Mheshimiwa
Spika, Taarifa hizi si za kweli na ni uongo uliokithiri kwa
aliyekuwa Mtumishi wa Umma kuudanganya umma wa Watanzania kwa kiasi cha kutisha
na Kamati inatoa taarifa ya uongo ndani ya Bunge.
Mheshimiwa
Spika, ukweli wa jambo hili ni kama ifuatavyo:
1.
Mwanasheria huyo Bw. Ngwilimi alileta ombi la
kusafiri kwenda Malaysia kwa kumdanganya Mwajiri wake kwa kudai kuwa alipewa ushauri
wa kwenda Malaysia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika barua ya kuomba
ruhusa alisema kuwa alikuwa aende na Mwanasheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliruhusiwa.
Hata hivyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali haikutoa Ofisa huyo na
hivyo kuamua kwenda peke yake.
2.
Bw. Ngwilimi hakufukuzwa
kazi na Bodi kama ilivyodaiwa katika Taarifa ya kamati ya PAC katika ukurasa wa 30, bali aliomba kuacha kazi
mwenyewe kwa kutoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa barua ya yenye Kumb na.
SEC.215/Conf/2/2014 ya tarehe 27 Februari, 2014 iliyokuwa inasomeka “Notice to Terminate my Service with TANESCO”
akitoa notisi ya siku 90 kwa mujibu wa Mkataba wake wa kazi.
3.
Katika ombi lake alidai
kuwa anaacha kazi kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa anahitaji kufanya shughuli
nyingine na akaushukuru uongozi wa TANESCO kwa ushirikiano kwa kipindi chote
alichofanyakazi. Machi 10, 2014 Shirika lilimjibu Bw. Ngwilimi kwa barua yenye
Kumb. Na. N.837 kuwa Uongozi na Bodi ya TANESCO wamekubali ombi lake la kuacha
kazi.
إرسال تعليق