Dar na Mikoani. Hakufai. Pengine ni neno
linaloweza kuwakilisha uhalisi wa hali ilivyo katika baadhi ya hospitali
kadhaa za Serikali nchini, ambako mamia ya wagonjwa wanateseka kutokana
na uhaba wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambao umeendelea
kuzikumba.
Wengi wa wagonjwa waliohojiwa wanalalamikia
kushindwa kumudu gharama za dawa ambazo wanapaswa kuzinunua kwenye
maduka wakisema hali hiyo inazifanya afya za Watanzania wengi wenye
kipato cha chini wanaozitegemea kuwa shakani.
Gazeti hili katika uchunguzi wake limebaini kuwa, uhaba huo pia umesababisha
hospitali nyingi kuwabana wagonjwa kwa kuwatoza
fedha kwa ajili ya huduma, ili kujijengea uwezo wa kununua dawa chache,
pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya dharura.
Kwa jumla, hali ilivyo ni tofauti ya matarajio ya
wengi kwamba kungekuwa na mabadiliko, hasa baada ya Serikali kutangaza
kwamba imekwishalipa sehemu kubwa ya deni ililokuwa ikidaiwa na Bohari
Kuu ya Dawa (MSD).
Hivi karibuni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid alisema wizara yake imeilipa MSD Sh20 bilioni ili
kupunguza makali ya uhaba wa dawa. MSD inaidai wizara hiyo zaidi ya
Sh90bilioni za ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Jana, Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja
alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa sababu tayari waziri wangu
alishatoa tamko bungeni, kwa hiyo kauli yetu ndiyo hiyohiyo aliyotoa
mheshimiwa waziri.”
Sura halisi ya uhaba wa dawa inaonekana katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ambako hali imeendelea kuwa mbaya kwani ukosefu huo wa dawa
umesababisha baadhi ya wagonjwa kuzidiwa na wengine kupoteza maisha kwa
kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Hospitalini Ocean Road, mwandishi wetu alikutana
na mkazi wa Arusha, Ashura Iddi aliyefika kutibiwa na kufuatana naye
hadi katika duka alikokwenda kununua dawa alizoandikiwa.
Akisaidiwa na mwandishi huyo, Ashura ambaye
amekatwa mkono wake wa kushoto kutokana na saratani ya mkono iliyosambaa
hadi kifuani, aliambiwa na mfamasia katika Duka la Biomed lililo karibu
na ORCI kuwa dawa zake za mionzi zinagharimu Sh166,000.
Hata hivyo, mgonjwa huyo ambaye alikuwa akikohoa
mfululizo kiasi cha kutapika, hakuweza kununua dozi hiyo kwani hakuwa na
fedha hivyo kurudi wodini kuendelea kukaa akisubiri siku dawa
zitakapofika au kupata fedha.
Ashura amelazwa ORCI tangu Oktoba 27, mwaka huu na
anasema hajapata matibabu zaidi ya kupewa dawa za maumivu aina ya
diclofenac. “Nimekosa hata dawa ya allergy (mzio) ambayo inauzwa Sh1,000
nimeambiwa hakuna,” alisema Ashura.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق