Licha ya kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wa Kitanzania na pia kupunguza tatizo la usafiri mijini litokanalo na foleni, usafiri wa pikipiki maarufu kama 'bodaboda' umeendelea kuua watu kimyakimya na kuwasababishia ulemavu wa kudumu maelfu ya manusura wa ajali za vyombo hivyo kila uchao.
Uchunguzi
uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa mbali na vifo na ulemavu, bodaboda
zimeathiri pia utoaji wa huduma katika hospitali zinazopokea majeruhi wa
vyombo hivyo, kwani wodi zimefurika kupita kiasi na kusababisha
wagonjwa wengi kulala chini.
Kamanda
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, ameiambia
NIPASHE kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 peke yake, pikipiki 8,241
zilihusika katika ajali 6,831 na kusababisha vifo vya watu 1,098 na
kuwajeruhi wengine 6,578; huku baadhi yao wakiishia kupata ulemavu wa
kudumu. Idadi hiyo ni sawa na wastani wa vifo vya watu watatu kila uchao
na majeruhi 18.
DAR, MORO, PWANI VINARA
Akieleza
zaidi, Kamanda Mpinga anasema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi
Agosti mwaka huu, pikipiki 3,998 zilihusika kwenye ajali 3,777 na
kusababisha vifo vya watu 608 na majeruhi 2,883.
Aidha,
takwimu za mikoa zinaonyesha kuwa jiji la Dar es Salaam ndilo
linaloongoza kwa kuwa na matukio ya ajali za bodaboda. Mwaka jana,
bodaboda 3,970 zilihusika katika ajali 3,405 jijini Dar es Salaam na
kusababisha vifo vya watu 172 na majeruhi 3,541.
Kadhalika,
katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, jiji la Dar es Salaam
lilikuwa na ajali 1,687 zilizohusisha pikipiki 2,280 na kusababisha
vifo vya watu 113 na majeruhi 1,539.
Kamanda
Mpinga anasema mkoa unaoshika nafasi ya pili kwa ajali za bodaboda ni
Morogoro; uliokuwa na ajali 657 na kuhusisha pikipiki 866
zilizosababisha vifo 73 na majeruhi 557 kwa mwaka 2013
Mwaka
huu, kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, Morogoro kulikuwa na ajali
191 zilizohusisha pikipiki 264 na kusababisha vifo vya watu 41 na
majeruhi 202.
Mpinga
anautaja mkoa unaoshika nafasi ya tatu kuwa ni Pwani, wenye matukio 428
ya ajali zilizohusisha pikipiki 589, vifo vya watu 84 na majeruhi 466
kwa mwaka 2013, huku kwa kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu mkoa
huo ukiwa na matukio 121 yaliyohusisha pikipiki 164 na kusababisha vifo
vya watu 40 na majeruhi 172.
Kilimanjaro
unashikilia nafasi ya nne katika janga hilo. Ulikuwa na ajali 372
zilizohusisha pikipiki 409 na kusababisha vifo vya watu 74 na majeruhi
343 kwa mwaka 2013. Kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, mkoa huo
ulikuwa na ajali 104 zilizohusisha pikipiki 121 na kusababisha vifo vya
watu 22 na majeruhi 88.
Mikoa
mingine na idadi ya ajali za bodaboda katika kipindi cha mwaka 2013
kwenye mabano ni Ruvuma (213), Katavi (190), Arusha (180), Manyara
(154), Tabora (128), Dodoma (123), Rukwa (110), Mwanza (96), Mbeya (90),
Kigoma ( 82), Shinyanga (81) na Kanda Maalum ya Tarime/Rorya ajali 80.
Mingine
ni Mtwara (77), Lindi (59), Singida (54), Geita (50), Kagera (43), Mara
(42), Tanga (35), Njombe (27) na Simiyu ikiwa na matukio machache zaidi
ya ajali za bodaboda yaliyoripotiwa Polisi baada ya kukumbwa na ajali
18 katika kipindi chote cha mwaka 2013.
Akielezea
kuhusu hatua zitakazosaidia kupunguza zaidi ajali za bodaboda nchini,
Mpinga anasema elimu ndiyo nguzo ya kumaliza ajali za bodaboda na kwamba
tangu mwaka 2010, wamekuwa wakitoa elimu na wanaamini kuwa walau
kiwango cha ajali za bodaboda kimekuwa kikipungua.
Kamanda
Mpinga anasema katika utafiti wao, wamebaini vyanzo vya ajali nyingi ni
makosa ya kibinadamu ambayo ni pamoja na kutoheshimu sheria, mwendo wa
kasi, ulevi wa madereva (ukiwamo wa unywaji wa viroba kabla ya
kuendesha), pikipiki kupakiza abiria wengi zaidi ya uwezo wake maarufu
kama mishkaki na madereva kutokuwa na leseni zinazothibitisha kuwa na
uwezo wa kutumia vyombo hivyo vya moto.
Anataja
vyanzo vingine kuwa ni ubovu wa miundombinu kama mashimo, utelezi na
kona kali barabarani na watumiaji kutovaa kofia ngumu (helmet) huchangia
kuongeza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za pikipiki.
REKODI YAWEKWA MOI
Uchunguzi
wa NIPASHE umebaini kuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) peke yake
hupokea wastani wa majeruhi 77 kwa wiki wanaotokana na ajali za
bodaboda, hiyo ikiwa ni sawa na wastani wa majeruhi 11 kwa siku.
Dk.
Mwanga Joseph wa Moi anasema asilimia 55 ya majeruhi wote wanaofikishwa
kwao kutokana na matukio ya ajali jijini Dar es Salaam huwa ni kutokana
na bodaboda.
Anasema
wingi huo wa majeruhi wa bodaboda husababisha mrundikano wa wagonjwa
wodini kiasi cha kuzidi idadi ya vitanda na hivyo wengi hulazimika
kulala chini.Anasema licha ya changamoto zilizopo sasa, wao wanaendelea
kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma na wanaamini kuwa ufumbuzi wa
tatizo la mrundikano uliopo sasa Muhimbili ni kuwa na matawi zaidi ya
Moi kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya ili kupunguza idadi ya wagonjwa
wanaofikishwa hapo kila uchao.
Msemaji
wa Moi, Patrick Mvungi, anasema kwa mwezi mmoja, wagonjwa wa ajali ni
600 na kati yao, 330 sawa na asilimia 55, ni wa ajali za bodaboda.
Mvungi
anasema kuwa licha ya majeruhi wa pikipiki kuwa wengi kiasi cha kuzidi
uwezo wa wodi zao, bado wanapowapokea huwachukulia kuwa ni sawa na
majeruhi wengine na wala hawawatengi kwenye wodi maalum kama ambavyo
imekuwa ikivumishwa na baadhi ya watu.
"
Kuna uvumi kuwa (Moi) tumetenga wodi kwa ajili ya majeruhi wa ajali za
pikipiki... (hili) siyo kweli. Hata viongozi wa waendesha pikipiki wa
Temeke kupitia umoja wao walishafika kuuliza hilo, tukawahakikishia
kwamba majeruhi wote wanalazwa kwenye wodi moja bila kubaguliwa na hivyo
hakuna sehemu maalum kwa ajili yao," alisema.
Akieleza
zaidi, Mvungi anasema kuwa kwa ujumla hali siyo nzuri kutokana na
msongamano wa wagonjwa unaotokana na ajali nyingi za bodaboda.
"Wodi
ina uwezo wa kulaza wagonjwa 33 kwa maana ya vitanda vilivyopo, lakini
wagonjwa huongezeka na kufikia 90. Hali hii siyo nzuri. Tunalazimika
kuweka magodoro chini na kuwapa huduma kwa sababu sisi ni hospitali ya
umma, hatuwezi kumkataa mgonjwa anapofikishwa (kwetu) akiwa katika hali
yoyote ile," anasema.
Mvungi
anasema kuwa mbali na mipango mingine kadhaa waliyo nayo, lakini njia
mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa wagonjwa kwenye
wodi zao ni kukamilika kwa jengo la ghorofa saba hivi karibuni
litakalokuwa na vitanda 380 na vifaa vingine vingi vya kisasa.
"Licha ya hali ngumu iliyopo sasa, (sisi) tunaendelea kuwa taasisi bora inayotoa huduma kwa wagonjwa," anasema.
"Ndani
ya jengo hilo tutaboresha zaidi kwa kuwa tunatumia mfumo wa kompyuta na
kuachana na mafaili (ya makaratasi) katika kuhifadhi taarifa za
mgonjwa. Madaktari watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wenzao waliopo
nje katika uboreshaji wa huduma za afya," anasema na kuongeza kuwa
taasisi yao imetunukiwa cheti cha ubora Afrika Mashariki.
GHARAMA BADO NAFUU
Mvungi
anasema gharama za upasuaji ni Sh. 200,000 na za kupokewa kwa huduma za
awali ni Sh. 50,000, hiyo ikiwa ni nusu ya gharama halisi.
Anasema
katika ajali nyingi za bodaboda, majeruhi huvunjika mfupa mrefu wa mguu
ambao hutakiwa kuwekwa vifaa maalum vinavyouzwa nje ya nchi kwa dola
300 za Marekani (Sh. 480,000).
Anasema
kwa ujumla, gharama anazolipa mgonjwa ni ndogo kwa kuwa serikali hutoa
ruzuku na kwamba, kwa kawaida huwa kuna wagonjwa wa aina mbili; ambao ni
wanaolipiwa na Moi baada ya kushindwa kumudu na wengine wanaojilipia
wenyewe.
MAJERUHI KUTELEKEZWA WODINI
Anaongeza
kuwa majeruhi wengi wa bodaboda hawana uwezo wa kumudu gharama za
matibabu na kwamba umoja wao (waendesha bodaboda) huonekana siku
wanayoletwa hospitalini, lakini baadaye wenzao wote hupotea na mgonjwa
kukosa wa kumhudumia, labda itokee bahati mbaya kwamba mgonjwa apoteze
maisha na ndipo hapo waliomleta na kumsaidia katika siku za awali
huonekana tena.
"Wengi
wa vijana hawa ni wale ambao wanategemea bodaboda kwa ajili ya
kujipatia kipato. Wengine ni za kwao na wengine za matajiri... hawa,
wengi hutelekezwa na Moi hulazimika kuwagharimia," anasema Mvungi.
Mvungi
anaelezea changamoto nyingine kuwa ni kutelekezwa hospitali kwa
majeruhi wa bodaboda. Anasema kundi la waendesha pikipiki au watembea
kwa miguu huokotwa kama wagonjwa wasiofahamika na kwamba wanapofikishwa
kwao, hutibiwa kwa matarajio kuwa wakizinduka ndugu zao watajitokeza au
wakipona watalipia gharama wenyewe; lakini kwa baadhi yao hali huwa
tofauti kwani hushindwa kulipia kutokana na vipato vyao kuwa duni.
"Ni
mzigo kwa taasisi kumlisha mgonjwa, kumtunza na kumuwekea vifaa maalum
ili arejee katika hali yake ya kawaida. Lakini kupitia sera ya msamaha
wa matibabu, wagonjwa wa aina hii huwa wanasamehewa," anasema na
kuwashauri madereva wa bodaboda kujiunga na bima ya afya ili wanapopata
ajali au kuugua iwe rahisi zaidi kwao kupata matibabu.
MTAALAM WA USAFIRISHAJI ANENA
Mkufunzi
wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Injinia Hans Mwaipopo, anasema vyanzo
vya ajali ni vitatu ambavyo ni binadamu anayechangia kwa asilimia 76,
chombo anachotumia asilimia 16 na mazingira asilimia nane.
Anasema
binadamu anachangi kwa asilimia hiyo kutokana na ukosefu wa elimu ya
usalama barabarani kwa vile wengi hawajui sheria zinazowaongoza wawapo
barabarani.
Mwaipopo
anasema pia tabia ya kupuuza sheria kwa wanaofahamu huchangia ongezeko
la ajali; kuporomoka kwa maadili kwani sasa ni rahisi mtu kupata cheti
kwamba amesomea na kukionyesha hata kama hajawahi kusomea udereva.
Aidha,
Mwaipopo anaongeza kuwa lipo pia tatizo la watu kupewa vyombo vya moto
bila kujihakikishia kuwa ni wazima kiakili kwani upo uwezekano kwa watu
wenye matatizo ya akili kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki na hivyo
kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia.
Mkufunzi
huyo anasema katika nchi nyingi zilizoendelea, kabla ya mtu kukabidhiwa
leseni anapimwa akili na hilo pia linapaswa kuzingatiwa ili kupunguza
ajali.
Mwaipopo
anasema sheria namba 30 ya 1973 na marekebisho yake inasema dereva
mwenye leseni halali anatakiwa kuwa na sifa kuu tatu, ambazo ni pamoja
na kusomea udereva katika chuo kilichosajiliwa na chenye walimu na macho
yake yawe yanaona vizuri.
Sifa
nyingine ni kutokuwa na ulemavu unaoweza kuathiri chombo cha moto
anachoendesha, kuwa na akili timamu, awe na afya njema na asiwe na
maradhi yenye kuathiri chombo anachoendesha kama ugonjwa wa moyo, sukari
na kifafa.
"
Leo hii wapo madereva wana matatizo ya kifafa. Tukifanya ukaguzi,
tutabaini kwamba wapo wengi wana matatizo ya macho, kifafa, moyo na
sukari lakini wanaendesha vyombo vya moto. Hii ni hatari," anasema.
Anasema
chombo kinachangia kwa asilimia 16 kwa maana ya matumizi mabaya, ikiwa
ni pamoja na chombo kwisha muda wake wa matumizi, lakini bado
kinaendelea kubaki barabarani.
Anasema
mazingira yanachangia kwa asilimia nane, ikitokana na miundombinu
mibovu na kukosekana kwa alama muhimu katika barabara na pia barabara
kulazimishwa kona pasipostahili na nyingi kujengwa chini ya kiwango.
Anasema
changamoto iliyopo kwa watu wa bodaboda, ni tabia ya wengi wao
kufundishana wao kwa wao. Hawajifunzi sheria za usalama barabarani na
hivyo hujiona wenye haki kuliko watumiaji wengine.
"Mara
kwa mara huwa tunawaona... mtu anatakiwa kupita kushoto, yeye anapita
kulia na hawana kofia ngumu... katika hili hatuwezi kutafuta mchawi, ni
lazima ajali zitaendelea kutokea na vifo na majeruhi kuongezeka,"
anasema.
AJIRA NA FOLENI
Bodaboda
zimekuwa zikisaidia kupunguza tatizo la usafiri katika maeneo mengi
nchini. Katika maeneo ya mijini kama Dar es Salaam ambako tatizo la
foleni limekosa suluhu ya haraka, bodaboda ndiyo kimbilio.
Kwenye
maeneo yasiyofikika kirahisi kwa usafiri wa gari, hasa vijijini,
bodaboda pia zimetwaa nafasi. Vyombo hivi ni mkombozi pia wa Watanzania,
hasa vijana wanaokabiliwa na tatizo la ajira.
Dereva
Sudi Hassan wa Mbagala Charambe anasema kuwa kwa wastani, kila siku
huwa hakosi kuingiza Sh. 20,000, sawa na Sh. 600,000 kwa mwezi na kiasi
hiki ni kikubwa mno kulinganisha na wastani wa pato la Mtanzania kwa
mwaka (2013) ambalo ni Sh. 1,186,424, sawa na Sh. 98, 868.67 kwa mwezi,
au Sh. 3,295.62 kwa siku; hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya
serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwenye Mkutano Mkuu wa
30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika jijini Tanga Mei
14, 2014.
Hata
hivyo, vifo vya ajali za vyombo hivi vinavyosababisha kuongezeka kwa
idadi ya wajane na watoto yatima nchini huhalalisha hisia kwamba pamoja
na faida zake, bodaboda ni "muuaji wa kimyakimya".
Ajali
za bodaboda zimekuwa zikichangia ongezeko la yatima. Takwimu zilizowahi
kutolewa mwaka 2011 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, zilionyesha kuwa Tanzania ilikuwa na watoto yatima
milioni 2.4 hadi kufikia mwaka 2011; kati yao wasichana wakiwa 1,055,000
na wavulana 1,345,000.
Aidha,
ajali za bodaboda zinaathiri uchumi wa watu mmoja mmoja na taifa. Kwa
mujibu wa Kamanda Mpinga, idadi ya pikipiki zilizohusika katika ajali
mwaka 2013 peke yake ni 8,241. Hivyo, ikiwa kila pikipiki hununuliwa kwa
wastani wa Sh. milioni 2 na kisha kuharibika kabisa baada ya kupata
ajali, maana yake jumla ya Sh. bilioni 16.48 zilipotea katika kipindi
cha mwaka 2013.
Kadhalika,
vipato vya watu wanaotegemea pikipiki hizo kwa shughuli za kibiashara
viliathirika kwa kiasi kikubwa kwani, kama kila dereva wa bodaboda
alitarajia kuingiza wastani wa Sh. 600,000 kwa mwezi (kama ilivyo kwa
dereva Hassan wa Mbagala Charambe), maana yake ni kwamba pato la jumla
ya Sh. 7,200,000 lilipotea kwa kila pikipiki kwa mwaka 2013. Hivyo, kwa
taifa zima (pikipiki 8,242), kiasi kilichopotea kutokana na bodaboda
zilizohusika katika ajali ni Sh. bilioni 4.94. Kwa makadirio ya jumla,
hasara iliyotokana na gharama za kuharibika kwa pikipiki hizo pamoja na
kipato kilichopotea kwa kutokuwapo barabarani kwa pikipiki hizo kwa
mwaka wa 2013 ni takriban Sh. bilioni 21.
UZOEFU WA UGANDA
Changamoto
zitokanazo na ajali za bodaboda zipo pia katika nchi nyingine za
Afrika, Mashariki. Kwa mfano, nchini Uganda, mwaka 2011 pekee, madereva
wa bodaboda 570 walifariki dunia. Wodi ya dharura katika Hospitali ya
Rufaa ya Mulago jijini Kampala imepachikwa jina la "bodaboda" kutokana
na kuwa na majeruhi wengi wa ajali za bodaboda. Hospitali hii peke yake,
kwa mwaka hupokea wastani wa majeruhi 7,280, sawa na majeruhi 20 kwa
siku.
KAULI ZA MADEREVA
Frank
Chungu aliyefanya kazi ya kuendesha pikipiki kwa miaka mitano katika
kijiwe cha Mwenge jijini Dar es Salaam anasema chanzo cha ajali nyingi
za bodaboda ni matumizi ya vilevi kama bangi na pombe kali za kwenye
vipakiti ambayo hutumiwa na waendesha pikipiki wengi.
Anasema
wengine hujifunza kwa muda mfupi na kuingia barabarani kama madereva
kamili na matokeo yake, wengi kati ya hao hawafuati sheria za usalama
barabarani na kujiweka katika hatari kubwa ya kupata ajali.
"Wengi
hawaheshimu taa za barabarani, Wanapita upande ambao siyo sahihi.
Hawako makini, wanatumia pombe … na kuvuta bangi. Kwa hali kama hii ni
lazima kutakuwa na ongezeko la ajali," anasema.
Chungu
anasema hivi sasa walau kuna mabadiliko kidogo ukilinganisha na miaka
michache iliyopita hasa kutokana na wengi wa madereva kuingiwa woga
baada ya kushuhudia wenzao wengi wanavyojeruhiwa na kupata ulemavu wa
kudumu na wengine kupoteza maisha huku wakiacha wake na watoto zao.
Kuhusu
leseni, anasema kwa sasa wengi wao wana leseni, lakini tatizo ni
kwamba, hawajifunzi kwa umakini kwani wapo wanaokwenda kujifunza
uwanjani siku ya kwanza na ya pili yake wanaingia barabarani kupakia
abiria.
Anasema
wengine huendesha kwa kasi kubwa kwa sababu tu ya kutaka wasifiwe kuwa
wao ni mahiri na kwa bahati mbaya, kadri pikipiki inavyozidishwa mwendo
ndivyo inavyokuwa nyepesi kuiendesha na hivyo dereva kusahau kuwa
tofauti na gari, wao wakipata ajali ni miili yao ndiyo hujigonga na
hivyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha au kuwa
walemavu.
NINI CHA KUFANYA
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mpinga, anasema kwa mujibu wa
sheria ya usalama barabarani, sura ya 168 kama iliyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002, mtu yeyote, ili apate leseni ni lazima kwanza apate mafunzo
kwenye vyuo vya udereva.
Kuhusu
madereva pikipiki anasema Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), wanaendesha
programu ya mafunzo kwa madereva pikipiki, lakini kinachosikitisha wengi
hawapendi kwenda kujifunza.
Anasema
wengine wanaotoa mafunzo ni wadau mbalimbali wa masuala ya usalama
barabarani ambao hupita kwenye maeneo ya vijiwe vya madereva wa bodaboda
kwa ajili ya kufundisha matumizi ya pikipiki yanayozingatia usalama wa
waendeshaji wa vyombo hivyo na abiria wao.
Kutokana
na kasi ya utoaji wa mafunzo kwa sasa, kati ya waendesha pikipiki
700,000 waliopo nchini kote, asilimia 70 tayari wamepata leseni.
Injinia
Mwaipopo anasema ni lazima serikali ichukue hatua madhubuti za
kuwafundisha waendesha pikipiki wote ambao wanategemea kazi hiyo kama
ajira yao ya kila siku katika kujiingizia kipato.
"Ukitaka
kukamua jipu huwezi kulikanda. Lazima ukamue usaha wote utoke, na ndiyo
pona ya mgonjwa... ajali nyingi, wengi hawajui sheria na hawataki
kujifunza. Lazima tuchukue hatua mapema vinginevyo idadi ya walemavu
itaongezeka siku hadi siku," anasema.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment