Komba adaiwa kuhujumu uchaguzi wa mitaa

Mbunge wa Mbinga Magharibi,mkoa wa Ruvuma, Kapteni John Komba.
Mbunge wa Mbinga Magharibi,, mkoa wa Ruvuma, Kapteni  John Komba, ametuhumiwa kuhujumu uchaguzi wa serikali za mitaa wilaya ya Nyasa ili Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiweze kushinda.
Afisa Uhamasishaji wa  Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fulgency Mapunda, aliwaaambia waandishi wa habari  kuwa Komba amekuwa akifanya vitendo vya kuhujumu uchaguzi huo na kusababisha watendaji kutoeleza tarehe ya kuajiandikisha pamoja na kuchelewesha kutoa kutoa fomu kwa wagombea.

Mwingine aliyetuhumiwa  ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Shaib Nnunduma, kwamba ameshirikiana na Komba kuhujumu uchaguzi kwa kuwanyima ushirikiano upinzani ili CCM kishinde katika nafasi hizo.

Mapunda alisema  maofisa watendaji wilaya ya Nyasa hawajatangaza tarehe ya kupiga kura wala taratibu za utoaji fomu  wamekuwa wakiendelea na maandalizi kimya kimya.

Aidha, Mapunda alisema wamekuwa wakiwatenga viongozi wa vyama vya upinzani na kutoa taarifa za upendeleo mkubwa kwa viongozi wa CCM pekee huku wakiwanyima taarifa viongozi wa upinzani.

Hata hivyo, Komba alikanusha madai hayo kwa kusema ni uongo na kwamba alifika Nyasa jana kuelimisha wananchi kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili chama chake kiweze kushinda na kuchukua nafasi nyingi.

Naye Mkurugenzi Nnunduma, alisema tuhuma hizo siyo za kweli na kwamba viongozi wote wa ngazi zote za wilaya wameshapewa maelekezo kuhusiana na uchaguzi pamoja na  ratiba.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم