Maalim Seif : Ukawa ndiyo wa kuing'oa CCM Madarakani

 Katibu Mkuu wa CUF akipandisha bendera baada ya kuzindua tawi la Ufukoni Stand, Kata ya Ufukoni mjini Mtwara
Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara mjini Mtwara.

Na Khamis Haji, Mtwara
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema ushirikiano wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa) ndio jibu sahihi kwa wananchi wengi waliokuwa wakihoji iwapo CCM itang’olewa nani atachukua nafasi hiyo na kukamilisha ndoto za Watanzania kuwa na maisha mazuri.
 
Maalim Seif amesema hayo wakati akihutubia mikutano ya hadhara, akiwa katika ziara ya kichama mkoani Mtwara, ambapo amekuwa akizindua matawi mapya ya CUF na kuhimiza wananchi kujiandikisha katika daftari la kura na kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa Disemba 14 mwaka huu kukiweka upande CCM.
 
Katibu Mkuu wa CUF amesema kwa miaka mingi wananchi walikuwa wakijiuliza nani atachukua nafasi ya CCM kuongoza dola, lakini sasa wananchi hawana hofu tena baada ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR Mageuzi na NLD kuamua kushirikiana kukiondoa madarakani CCM.
 
Amesema CCM baada ya kuongoza nchi kwa miaka 53 tokea uhuru kimeshachoka na hakina jipya tena kinaloweza kuwafanyia wananchi na kimebaki kuonesha kibri na utawala wa mabavu dhidi ya wananchi.
 
Amewataka wananchi wasidanganyike kuwa CCM inaweza kutoa mgombea bora wa Urais kwa sababu viongozi wote wa CCM wanafuata mfumo mmoja wa chama chao ambao kwa sasa hauwezi kuwaletea mabadiko ya msingi wananchi wa Tanzania.
 
“Wala msidanganywe na Rais Kikwete kuwa atakuja mtu mwengine kutoka CCM ambaye atakuleteeni maendeleo, CCM waje na mgombea kama hariri lakini chini ya mfumo wao hataweza kufanya kitu chochote kipya”, amesema.
 
Akizindua baada ya kuzindua tawi jipya la CUF Kata ya Ufukoni, Manispaa ya Mtwara, Maalim Seif amesema wananchi wamechoka kwa bakora za CCM.
 
Amesema sera za CCM zimewadhoofisha wananchi walio wengi hasa vijana kiasi kwamba vijana wengi wanaonekana ni wazee na unatamani kuwaamkia kutokana na maisha duni chini ya sera za CCM.
 
“Nyinyi hapa Mtwara sio wageni na hilo nahikaka bakora za CCM zimewatosha tuungane kuiondoa madarakani CCM na kwa hili chini ya ushirikiano tuliouanzisha, CCM itang’oka tu”, amesema Katibu Mkuu wa CUF.
 
Maalim Seif amesema kazi iliyo mbele ya wananchi hivi sasa ni kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha katika zoezi linaloendelea ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi ujao na kukipa salamu CCM muda wao wa kuondoka umefika.
 
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya amesema kama kuna watu wanapaswa kupelekewa magari ya deraya na kuadhibiwa ni viongozi wa CCM wanaochota fedha za wananchi kwa njia ya ufisadi na sio wananchi wa Mtwara.
 
Kambaya amesema hivi sasa taifa liko njia panda na kamwe wananchi hawawezi kunyamaza kutokana na wizi na ufisadi unaofanywa ambao unasababisha madhara makubwa kwa wananchi wanyonge.
 
“Hiki ni chama kisichotekeleza ahadi, katika awamu hii walisema watashughulikia hali mbaya magerezani, matatizo ya hospitali ya Muhimbili, wauza dawa za kulevya, rushwa mahakamni na baadaye wakaahidi Katiba mpya, yote hayakutekelezwa”, alisema Kambaya

Post a Comment

Previous Post Next Post