Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema mambo yanayotokea
sasa nchini, kama viongozi kuwa na akaunti nje ya nchi na kudai ni
‘vijisenti’, Serikali kuingia mikataba yenye utata isiyohojiwa popote ni
matokeo ya nchi kuwa na Katiba yenye maswali mengi kuliko majibu.
Akizungumza katika mdahalo wa Katiba uliokuwa na
mvuto wa aina yake kwa watu kushangilia kila mjumbe aliyakuwa
anazungumza ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere uliofanyika jana
kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba huku
akitumia zaidi mifano alisema mambo hayo yanaweza kuendelea kwa sababu
hata Katiba Inayopendekezwa pia ‘imeyabariki’.
Katika mdahalo huo Jaji Warioba aligusia ufisadi
wa Sh306 bilioni za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa ajili ya
kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Ugavi wa Umeme
(Tanesco) kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, kuwa ni matokeo ya kuwa na
Katiba isiyo na majibu.
Huku akijinadi kuwa yeye ni mwanachama hai wa
Chama cha Mapinduzi (CCM), Jaji Warioba alisema kuna ‘CCM imara’ na ‘CCM
maslahi’ na kwamba tabia yake ya kutoa changamoto ya masuala mbalimbali
imetokana na kujengwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na mmoja
wa washiriki wa mdahalo huo kutoka Umoja wa Vijana wa CCM, Senga
Abubakar aliyetaka kujua kama Jaji Warioba ataiunga mkono Katiba
Inayopendekezwa, iwapo itapitishwa katika kura ya maoni.
Mdahalo huo ni wa tatu kufanywa na taasisi hiyo,
baada ya ule wa pili uliofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl Novemba 2
mwaka huu na kuvunjika kutokana na kuibuka vurugu, huku Jaji Warioba
akishambuliwa alipokuwa akihitimisha hotuba yake kwa kuhoji watu
wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Julius Nyerere kupitisha hoja zao
katika misingi isiyokubalika.
Tofauti na mdahalo wa pili, mdahalo wa jana
ulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na mamia ya washiriki walikaguliwa
kabla ya kuingia ukumbini na kutakiwa kuandika majina ili idadi yao
iweze kutambuliwa.
Katika mdahalo huo, Jaji Warioba aliambatana na
waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole,
Profesa Mwesiga Baregu, Joseph Butiku na Mohammed Yusufu Mshamba.
Huku akishangiliwa na mamia ya washiriki wa
mdahalo huo, Jaji Warioba alisema, “Tume ya Katiba ilipendekeza miiko na
kanuni za uongozi lakini Bunge Maalumu la Katiba limeyaondoa na
kuyaweka katika msingi wa utawala bora.
“Hivi huwezi kuwa mzalendo na mwadilifu mpaka uwe
kiongozi? Hii si misingi ya utawala bora ni misingi ya kitaifa na
inamhusu kila mmoja wetu.”
Alisema lengo la kuweka suala hilo ni kutaka
zawadi wanazopewa viongozi ziwe za taifa, “Maana yake kama umepewa
zawadi inakuwa ya taifa siyo ya kwako. Yaani kama umepewa dhamana ya
uongozi na unapata ‘vijisenti’ viwe vya taifa.”
Alisema kutokana na maoni waliyokusanya kutoka kwa
wananchi na utafiti uliofanywa na Tume walibaini kuwa masuala hayo
yakiwekwa katika sheria badala ya Katiba, sheria husika haitakuwa na
nguvu.
- Bofya Hapa kuendelea Mwananchi
- Bofya Hapa kuendelea Mwananchi
Post a Comment