
Katuni
Bingwa wa Ligi Kuu Bara huiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kungali mshindi wa pili akiipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika, michuano yote ikiandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, Caf.
Ligi Kuu imesimama kwa wiki saba kupisha mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Swaziland na Taifa Stars (iliyopigwa jana), michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha Timu B za Klabu za Ligi Kuu, na mashindano ya Kombe la Chalenji ambayo hata hivyo, huenda yasifanyike kutokana na kukosa nchi mwenyeji baada ya Ethiopia kujitoa dakika za mwisho.
Kingine kilichosababisha Ligi Kuu kusimama kwa siku hizo ni pamoja na kupisha usajili wa dirisha dogo, ambao umefunguliwa rasmi Jumamosi Novemba 15 na ukitarajiwa kudumu hadi Desemba 15, mwaka huu.
Ni kawaida kwa viongozi wa klabu zetu kuunda kamati zao za usajili ambazo huingia sokoni kusajili wachezaji iwe ni wakati wa usajili wa majira ya joto (dirisha kubwa) ama huu wa dirisha dogo.
Kwa ujumla tunazipongeza baadhi ya klabu ambazo zina utaratibu huo mzuri wa kuunda kamati za usajili na kwenda sokoni kufanya kazi hiyo ngumu kwani pasipo kuwa na jopo la usajili ni vigumu kupata wachezaji wanaokidhi viwango stahiki.
Mchakato kama huo haupo tu hapa nchini, kwani hata nchi zilizoendelea kisoka, klabu zao zina kamati kama hizo ambazo si tu kusajili bali zina wigo mpana zaidi kwa kuhusika pia kuvumbua vipaji vya makinda.
Pamoja na pongezi hizo, kwa muda mrefu NIPASHE kama mdau mkubwa wa michezo hapa nchini limebaini kamati hizo kufanya usajili kwa kutumia uzoefu, mapenzi yao kwa mchezaji na uelewa wao pasipo kutoa nafasi pana kwa kocha wa klabu husika.
Tunatambua wazi timu inapofanya vibaya wa kwanza kuwajibika ni kocha, mfano mzuri kwa msimu huu tu, tumeshuhudia mapema kocha wa Ndanda FC, Dennis Kitambi akiwa wa kwanza msimu huu kuwajibika kuachia ngazi kutokana na matokeo mabovu.
Mwishoni mwa wiki pia, Juma Mwambusi wa Mbeya City aliyepata mafanikio makubwa na timu hiyo msimu uliopita kwa kuipandisha daraja na kumaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu Bara, naye akiwajibika kwa kutangaza kuachia ngazi.
Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri kama si ushindi dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya ligi kwenda likizo, naye alikuwa amtarajiwa wa kutimuliwa kutokana na sare sita mfululizo.
Hao ni wachache tu katika wengi kwani ukirudi nyuma kidogo utakutana na Milovan Cirkovic, Patrick Leiwig wote wa Simba, huku Yanga ukimkuta Mholanzi Ernie Brandts, wote hao wakikumbana na matatizo kama hayo.
Takribani kila msimu makocha huwajibishwa kutokana na matokeo mabovu lakini wakibebeshwa mzigo huo huku wakiwa si wahusika wa kusajili wachezaji ambao ni wahusika wakuu wa matokeo uwanjani.
Ni vema sasa makocha wakafunguliwa milango kuweza kusajili ama mapendekezo wanayoyatoa kuhusu wachezaji wanaowataka yakafanyika kazi kwa asilimia 100 ili timu inapofanya vibaya watendewe haki kwa kuwajibishwa.
Tunatambua pia baadhi ya makocha wameanza kuzifundisha timu zao msimu huu huku zikiwa tayari zilishasajili, hivyo kuwapa nafasi ya kuziba mapengo yaliyojitokeza katika dirisha hili dogo kutasaidia kupunguza lawama kutoka kwao.
Kadhalika tunaamini huu si wakati wakufanya usajili mkubwa, bali mabadiliko yatakayofanywa yatazingatia mapendekezo ya makocha ambao kwa asilimia kubwa huangalia wingi wa majeruhi katika idara husika, idara zilizoshindwa kufanya vizuri na matatizo mengine ya msingi kiufundi.
Hicho ndicho kinachotufanya tuamini kwamba endapo makocha watapewa wigo mpana wa kwenda sokoni ama kutekelezewa mapendekezo yao kama walivyoagiza, basi viongozi watawatendea haki kwa kuwawajibisha pale timu zinapofanya vibaya.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق