BAADHI ya akinamama wanaowanywesha watoto wao maziwa aina ya
Lactojen1, wameingiwa na hofu kutokana na maziwa hayo kuadimika sokoni.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa nyakati tofauti, akina
mama hao walisema kuwa hivi sasa maziwa hayo yamekuwa bidhaa adimu
kupatikana kutokana na wauzaji wengi kutokuwa nayo.
Jacquline John alisema kuwa mtoto wake wa miezi mitano sasa amekuwa
akinywa maziwa hayo kutokana na yeye kuwa kazini lakini kwa anashindwa
la kufanya kwa kuwa kwa miezi miwili hayapatikani.
“Mimi nilimwanzisha mwanangu Lactogen I, hayajawahi kumletea madhara
yoyote lakini hivi sasa nachanganyikiwa kwani hayapatikani hata uzunguke
maduka yote katika maeneo ninayoishi ya Tabata,” alisema.
Naye Gracey Gibson, alisema kuwa amepata woga wa kumuanzishia mwanae
maziwa mengine kutokana na hofu ya kuweza kumletea madhara ikiwemo
kuharisha au kuishiwa maji mwilini.
Alisema kuwa wapo wanaompa ushauri wa kumtaka amwanzishie maziwa ya
ng’ombe lakini baadhi ya wataalam wamekuwa wakitoa angalizo juu ya
maziwa hayo hasa kutokana na kuwa na protini nyingi na yanaweza
kuchangia mtoto kupata pumu.
“Hivi kama kuna shida juu ya maziwa ya Lactojen 1, si bora Serikali
itujulishe maana haiwezekani wauzaji wote washindwe kuwa nayo bidhaa
hiyo,” alisema.
Mmoja wa wauzaji wa rejareja, Salum Issa alisema kuwa amejitaidi
kutafuta maziwa hayo kwa takribani mwezi mmoja sasa lakini hajaweza
kupata. “Mimi nina wateja wengi wanaotumia bidhaa hiyo, nimejaribu
kuzunguka kuanzia kule wanakouza jumla lakini kote huko unaelezwa maziwa
hayo hakuna kwa sasa,” alisema.
Dk. Namala Mkopi, alisema kuwa iwapo maziwa hayo hayapatikani sokoni
wazazi wanaofanya kazi wanaweza kuwaanzishia watoto wao maziwa mengine
ili kuhakikisha wanapata maziwa wakati wakiwa hawapo karibu nao.
“Mara nyingi kama kuna upungufu wa maziwa unaweza kumuanzisha maziwa
mengine, tunaamini kuwa hakuna madhara yanayoweza kuwapata ikiwa vyombo
anavyotumia vinaandaliwa katika mazingira mazuri,”alisema.
Via- Tanzania Daima

إرسال تعليق