Miraji Mtaturu; Maendeleo ni Mchakato

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Miraji Mtaturu
Na Mathias Canal, Mufindi
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Miraji Mtaturu, amasema kuwa maendeleo ni mchakato na mipango sio kudanganya wananchi kwa jambo lisilowezekana.
Aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa kuimarisha chama Kijijini Kiyowela, Wilayani Mufindi.
"Maendeleo ni mchakato mi sidhani kama kuna watu hapa ambao wamekamilisha kila jambo katika familia zao, ila kila siku mnapanga na mnatekeleza jambo moja baada ya jingine, sasa watakuja watu hapa watasema watawaletea kila kitu kijijini kwenu, sasa kwa mtazamo wenu jambo hilo linawezekana kweli? wananchi wakaitikia HAPANA"
Mtaturu alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wakazi hao kwa kumpitisha Endru Kapita, kwenye kura za maoni za chama hicho ili kuiwakilisha Ccm kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Disemba 14 mwaka huu.
Aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi ili waweze kupiga kura kwani hiyo ni haki yao kikatiba kwa kila mtu mwenye sifa na vigezo vya kupiga kura.(P.T)
"Ninawapongeza kwa kufanya uchaguzi lakini leo tumempokea kijana mmoja kutoka Chadema kwani Mwenda tezi na omo marejeo ngamani, hivyo kwa kuwa CCM ni nyumbani tumpokee kwa heshima na taadhima kwakuwa sisi hatuna ubaguzi" Alisema Mtaturu
Aidha aliwataka wananchi hao kuwaepuka baadhi ya watu ambao wanapita mitaani kuwapotosha ili wasiikubali katiba mpya, ambayo imekidhi matakwa ya wananchi wote kuanzia wafugaji, wakulima na nyanja zingine nyingi.
"Kila mwenye macho haambiwi tazama hivyo ninawaomba kuisoma katiba na kuielewa ndipo muipigie kura ya ndio kwa kuwa imekidhi matakwa ya watanzania, Kumbukeni mnaweza kujaribu nguo,chakula,malazi na mavazi lakini uongozi haujaribiwi ni kama kujaribu kuonja sumu" Alisisitiza Mtaturu
Akijibu swali la Andrea Simwiche aliyetaka kujua juu vijana waliomaliza kidato cha nne kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, Mtaturu alisema kila mtanzania ana haki ya kufanya kazi kama ana uwezo wa kufanya kazi endapo tu kama atakuwa hajavunja sheria za kazi.
"Jambo hili nimelichukua nitalifanyia kazi ili kila mmoja apate ajira kwa mujibu wa sheria, lakini nimesikia watu wakisema sema kuhusu wagombea, naomba niwatoe wasiwasi kwamba mgombea atakaye shinda kura za maoni ndiye atakayepigiwa kura tarehe 14 Disemba, hivyo mimi sitambadilisha mjumbe yeyote yule kwa matakwa yangu ama ya mtu mwingine"
Hata hivyo Mtaturu aliwasihi viongozi wanaomaliza muda wao serikalini kupitia Chama Cha Mapinduzi, kushirikiana na kila mgombea sambamba na wananchi ili waweze kupata kiongozi anayependwa na kukubalika na jamii yake kwa ajili ya maendeleo ya kijiji na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

أحدث أقدم