Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya Mkombozi imesema, haihusiki
na utakatishaji fedha zilizoibiwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow Sh306
bilioni.
Kauli ya Benki ya Mkombozi inakuja wakati Ripoti
ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuitaka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kuitangaza benki hiyo kama benki ya utakatishaji fedha nchini.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Benki ya Mkombozi
ilisema, “Benki ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na
utakatishaji wa fedha chafu.”
Kuhusu kufunguliwa kwa akaunti hiyo na Rugemalira
taarifa hiyo ilisema fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP
iliyopo kwenye benki hiyo zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na
PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Ilisema chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha
kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na
kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika Benki ya Mkombozi.
Kuhusu kuhamishwa fedha taarifa hiyo
ilisema,“Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili, fungu la kwanza
ilikuwa ni Sh73.6 bilioni zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu
namba 000000050720 ya Januari 23 mwaka huu na fungu la pili ni Dola 22
milioni zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba 000000050812 siku
hiyo hiyo.”
“Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa
yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania,
kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo
ni malipo halali na siyo fedha chafu,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza: “Benki inawataarifu wateja wake na
Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhuma hizo ambazo hazina ukweli
ndani yake, badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya
nchi yetu.”
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق