Mitambo ya IPTL itaifishwe - Serukamba

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba amewataka wabunge wenzake wamuunge mkono ili kuishinikiza Serikali itaifishe mitambo ya mmiliki wa PAP inayosimamia IPTL kwa sasa, Harbinder Singh Sethi.
Alisema anavyoamini yeye wakifanikiwa kufanya jambo hilo litawapa heshima, pia itawashtua wawekezaji wengine wenye lengo la kuhujumu nchi kwa kisingizio cha uwekezaji.
“Yaani mimi sitaki kumnyooshea mkono kiongozi yeyote lakini najiuliza jambo hili limewezekanaje, tuna kila sababu ya kutaifisha kwanza ameleta ‘document fake’ (nyaraka) feki, hivyo tuichukue ile mitambo tuikabidhi Tanesco, Serikali ituunge mkono,” alisema Serukamba.
Alisema pia fedha hizo zinaweza kurejeshwa iwapo Benki Kuu (BOT) watawaandikia Benki ya Stanbic kulipa fedha hizo kwa sababu hazikufuata taratibu za kibenki zinazotakiwa hasa kuruhusu fedha kiasi kikubwa zaidi ya milioni 10 kuchukuliwa taslimu.
Mbunge Ester Bulaya (Viti Maalumu CCM) aliliambia Bunge kuwa yupo tayari kuwachukua vijana waliokosa mikopo, wanawake wanaokosa huduma bora ya afya kuandamana, iwapo hatua za kisheria hazitachukuliwa dhidi ya waliohusika ufisadi kwenye akaunti ya Escrow.
Alisema kuwa wahusika wote wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kusababisha aibu kubwa kwa nchi na mateso kwa wananchi, ambapo aliitaka Serikali kuwa makini na wawekezaji ili kuepuka kupokea matapeli.
“Hawa viongozi waliopewa hizo fedha ambazo wanadai kwamba ni michango, wanashangaza, hii ni aibu kwa sababu mwingine aliyedai kuwa ni mchango taarifa zinaonyesha kwamba ziliingia kwenye akaunti ya shule hizo kwa saa 48 kisha zikatolewa zote bila hata bodi kuridhia,” alisema Bulaya.
Bulaya alisisitiza kuwa mazingira yanaonyesha kwamba viongozi waliopewa fedha hizo ilikuwa ni kama zawadi kwa kukamilisha dili.
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP) John Cheyo, alieleza kukerwa na viongozi wa Serikali wanaosimama kusisitiza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow hazikuwa za Serikali.
“Siyo lazima uwe na digrii kuelewa hili, viongozi hao wanaposimama hapa na kukana kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali wananchi wanakasirika, nataka hata kulia ‘it’s not possible’ Serikali maskini inayotegemea wafadhili kukataa fedha namna hiyo,” alisema Cheyo.
Alisema mbaya zaidi ni kwamba fedha hizo zilizopaswa kulipwa kwa IPTL zimelipwa kwa mtu wa tatu.
“Mungu wangu, Mungu wangu, huyo mtu kwa ujanja ujanga alipokea hiyo fedha, kisha akafunga akaunti husika ‘we can’t see the money has gone’, hatua zichukuliwe kwa wote waliohusika IPTL ni kidonda ndugu kwa miaka 20,” alisema Cheyo.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم