Mtambo wa kuchakata gesi kuchukua miaka 7

Statoil Tanzania
Ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asili kwa ajili ya matumizi mbalimbali (LNG) mjini Mtwara unakadiriwa kuchukua miaka saba.
Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Statoil Tanzania, Thomas Mannes, amesema mambo yakienda kama yalivyopangwa, mtambo huo utakuwa tayari kwa uchakataji kati ya mwaka 2022 au 2023.
 
Akizungumza na viongozi wa dini wa Tanzania waliotembelea mtambo wa uchakataji gesi wa Statoil uliopo Karsto, Norway, Mannes amesema kuwa mradi huo mkubwa utagharimu mabilioni ya dola za Marekani.
Mannes alisema tayari wameshapendekeza maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mtambo huo na hivi sasa wabia wa mradi wanateua timu ya pamoja itakayosimamia mradi huo.
 
Mradi huo utakuwa wa pamoja kati ya Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC) na kampuni za Statoil, BG, ExxonMobil, Ophir na Pavilion. Mradi huo utaenda sambamba na miradi mingine ya mafuta ya vitalu 1, 3 na 4 inayoshirikisha TPDC, BG, Ophir na Pavilion na mradi wa gesi wa kitalu 2 wenye ubia kati ya TPDC, Statoil na ExxonMobil.
 
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwani kutaongeza mapato na nafsi za ajira, kutachochea biashara za bidhaa na huduma, kutoongeza mchango katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na kutaleta uwiano mzuri wa biashara.
 
Naye Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo,  Ove Tungesvik, alisema kuwa mtambo wa Karsto ndio mkubwa kuliko yote barani Ulaya.
 
Kwa upande wao, viongozi hao wa dini wameishauri kampuni ya Statoil kuwajengea uwezo watanzania, kupitia mafunzo na programu nyingine, kama Wanorway walivyosaidiwa na Wamarekani katika miaka ya 1970, ili Watanzania nao waweze kuisimamia sekta ndogo ya mafuta na gesi katika miaka michache ijayo.
 
Viongozi hao wa dini wapo mjini Stavanger, nchini Norway katika ziara ya mafunzo ya sekta ndogo ya mafuta na gesi. Ziara hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Serikali ya Norway kupitia kwa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم