Mlatha ahamaki wasichana kudhalilishwa

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlatha amemtaka Naibu Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri kuwaomba radhi wasichana nchini nzima kwa kuwadhalilisha.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la nyongeza.
“Uwatake radhi wasichana wote kwa kuwadhalilisha. Unasema kama wenyeviti wa Serikali za Mitaa wakikataa kuwa watoto huwa ‘hawapigwi’ mimba, itawezekana kupunguza mimba za utotoni. Viongozi wangapi kuanzia ngazi ya Taifa ambao wamechukua hatua kwa watoto waliopata tatizo hilo?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema suala la kuzuia mimba za utotoni ni la watu wote.
“Ukitembea barabarani unakutana na vibinti vidogo vinatembea saa 2.00 usiku. Maeneo mengine kuna sheria zinazokataza watoto wadogo kuingia katika vibanda vya sinema,”alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Riziki Said Lulida alihoji kwamba Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la mimba za utotoni kwa kuwa Lindi inaongoza kwa tatizo hilo, hali inayosababisha kufanya vibaya katika sekta ya elimu.
Akijibu, Mwanri alisema Serikali imekuwa ikihamasisha jamii kufuatilia mahudhurio ya watoto wao shuleni.
Alisema imeboresha somo la elimu rika kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi inayoendana na makuzi.
Naibu Waziri Mwari alisema watu wanaobainika kuwakatiza masomo watoto au kuwashawishi kuingia katika mahusiano ya kimapenzi, huchukuliwa hatua za kisheria .
“Lakini tumeandaa vipindi na programu mbalimbali zinazohimiza uzazi salama na kuepuka mimba za utotoni kupitia radio, machapisho, televisheni, warsha na semina,” alisema.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post