Serikali inaweza kukitoa kafara CCM - Kinana

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulrahman Kinana, amesema Serikali inaweza kukitoa kafara chama hicho kwa sababu ya kuchelewesha fedha za miradi ya maendeleo ambayo iliahidi kuitekeleza kwa wananchi.

Bw. Kinana aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara na kusisitiza mbunge na madiwani wa chama hicho wapo katika wakati mgumu.

Alisema Serikali iliahidi mambo mengi kwenye Uchaguzi Mkuu 2010 lakini hadi sasa fedha zilizopelekwa kwenye Halmashauri ya Newala mwaka 2014/15 ni asilimia 13.

Aliongeza kuwa, madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri wameahidi mambo mengi kwa wananchi wakiamini watapata fedha zilizotengwa kwenye bajeti lakini matokeo yake zimepelekwa fedha kidogo.

"Kitendo cha Serikali kushindwa kuleta fedha za maendeleo ya wananchi kwa wakati au kutopeleka kabisa, kinawaumiza madiwani waliotoa ahadi kwenye kampeni zao mwaka 2010...nitakwenda kuwaleza walete fedha za miradi kwa wakati," alisema.

Bw. Kinana aliwajia juu watu wanaogawa pembejeo za kilimo na kudai wakulima hawapelekewi kwa wakati na wakati mwingine wanatoa pembejeo hizo kwa kujuana hivyo kukwamisha dhana nzima ya Kilimo Kwanza.

"Pembejeo hazipelekwi kwa wakati lakini wakati mwingine zinapelekwa kwa kujuana...hali hii inarudisha malengo ya Serikali kuwapatia wananchi pembejeo, kuna kuna wakati zinapelwekwa zikiwa hazifai kwa matumizi," alisema Bw. Kinana.

Post a Comment

Previous Post Next Post