Muziki wa kitanzania na changamoto zake (1)

Licha ya kufariki miongo kadhaa iliyopita, wanamuziki kama Marijani Rajab, Mbaraka Mwishehe, Juma Kilaza, Muhidin Maalim Gurumo na wengine wengi, kazi zao bado zinaendelea kuishi.
Kinachofurahisha zaidi ni kwamba, ladha ya muziki wa wakongwe hao ya awali, bado ipo kwa kiwango kile kile. Hakuna ubishi kwamba kila unaposikiliza tungo za mashairi yao, unapata ujumbe ule ule uliokusudiwa sanjari na burudani yake.
Takribani miongo miwili sasa kumekuwapo na mfumko wa wanamuziki wanaojiita wa kizazi kipya. Wanamuziki hawa wamekuwa wakipiga muziki katika mahadhi yanayojulikana kama Bongo Fleva.
Muziki wa zamani uliopigwa na wakongwe niliowataja hapo juu na wengine kama hao una tofauti kubwa na ule wa Bongo Fleva. Tofauti hiyo ipo kimaudhui, kimuundo, hata uwasilishwaji wake.
Lakini kubwa zaidi ni kwamba muziki  wa Bongo Fleva  umeondoa kwa kiwango kikubwa utambulisho wa awali wa muziki wa kitanzania.
Kwa kiasi kikubwa jambo hilo limechangia kupoteza umaarufu wa muziki wa kitanzania kwenye medani za kimataifa.
Je, nini chimbuko la tatizo?
Kuna changamoto nyingi zinazoukabili muziki wa kitanzania. Kwa kiasi kikubwa, changamoto hizo zimechangia kupotea kwa muziki wa asili. Siyo hivyo tu, bali pia zimechangia kudunisha muziki nchini.
Charles Mohamed Kayoka ni mwalimu wa sanaa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na utandawazi.
Anasema kuwa ujio wa teknolojia, umerahisisha mambo mengi kasa katika masuala ya muziki.
Anafafanua kwamba hali hiyo imesababisha vyombo vilivyohitaji kupigwa na kundi la wanamuziki, sasa kufanywa na mtu mmoja kwa kutumia kinanda kimoja tu.
“Msaada wa kompyuta, unatosha kabisa kumwezesha msanii kutengeneza wimbo anaoutaka kwa saut ya ala anayoitaka, hatimaye akaingiza muziki huo sokoni. Jambo hili limechangia uvivu na kutojituma kwa wanamuziki wetu,” anasema - (Mwananchi)

Post a Comment

أحدث أقدم