Kipa Mwadin Ali
Mara tu baada ya kumalizika kwa VPL msimu uliopita, uongozi wa Azam FC uliwasajili Kavumbagu aliyekuwa amemaliza mkataba wake na Yanga na Domayo aliyekuwa amegoma kuongeza mkataba wa kubaki Jangwani, usajili ambao ulitikisa uga wa michezo nchini huku Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akimteua mwanasheria kuchunguza usajili wa kiungo huyo uliofanywa kwenye kambi ya Taifa Stars mjini Tukuyu, Mbeya.
NIPASHE imebaini Yanga iko mbioni kunasa saini ya Mwadini ambaye kwa sasa ni chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Mcameroon Joseph Omog cha Azam FC kwa dau la Sh. milioni 60 katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga (jina tunalihifadhi), zimeeleza kuwa kamati hiyo bado ipo katika mazungumzo na kipa huyo wakimshawishi kujiunga na mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara ili kuziba nafasi ya Juma Kaseja anayehusishwa kutaka kurudi katika timu yake ya zamani, Simba.
Mwadini alikiri juzi kuzungumza na Yanga na kuweka wazi kwamba endapo ataridhika na maslahi, atakuwa tayari kujiunga na timu hiyo yenye upinzani mkubwa na timu yake ya sasa Azam FC.
Yanga wana kipa chaguo la kwanza kikosini mwao na Taifa Stars kwa sasa Deogratius Munishi 'Dida' ambaye walimchukua pia kutoka Azam FC muda mfupi baada ya kumalizika kwa tuhuma za kutumiwa na klabu kongwe nchini, Simba na Yanga zilizokuwa zikimkabili nyota huyo aliyefungwa mabao matano katika mechi saba zilizopita za VPL msimu huu.
Mkataba wa Mwadini unamalizika Oktoba 2015 na kipa huyo amesema miaka minne aliyoichezea timu hiyo akitokea Mafunzo ya Zanzibar inatosha na anataka kusaka changamoto mpya.
Azam FC inajivunia kuwa na kipa 'yosso' Aishi Manula, ambaye ni wazi ndiye aliyeinyima Yanga ubingwa wa VPL msimu uliopita baada ya kudaka penalti ya mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza katika mechi ya mzunguko wa pili iliyomalizika kwa sare ya bao moja kwenye Uwanja wa Taifa jijini na kufuta matumaini ya Yanga kuikamata Azam kileleni.
Mzunguko wa kwanza msimu uliopita Yanga ilifungwa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC kwenye uwanja huo.
NIPASHE liliutafuta uongozi wa Azam FC jijini Dar es Salaam jana ambapo msemaji wake, Jaffari Idd Maganga alisema muda wa kuweka wazi majina ya nyota wanaowauza na kuwatoa kwa mkopo kipindi hiki cha dirisha dogo bado haujafika.
"Hakuna kiongozi wa Azam FC aliyezungumza juu ya suala hilo na mtandao rasmi wa klabu yetu haujaweka taarifa hiyo. Muda wa kutoa taarifa rasmi juu ya wachezaji wanaoachwa bado haujafika, subirini," alisema Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alipotafutwa na gazeti hili jijini juzi, alisema: "masuala yote ya usajili yako chini ya 'Coach' (Marcio) Maximo, atakapowasili Jumatano (leo) ataeleza kuhusu suala hilo."
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق