KOCHA wa Simba, Patrick Phiri, aliondoka Dar es Salaam jana
Alhamisi usiku kwenda kwao Zambia, lakini akautaka uongozi wake kumwacha
huru straika wake Mrundi Amissi Tambwe ili ajiunge na timu nyingine.
Hata hivyo mchezaji huyo amegoma.
Phiri aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa kipindi
alichokaa na Tambwe amemuona ni mchezaji mzuri lakini hana furaha
kuichezea timu hiyo tangu kuwepo na taarifa zilizokuwa zikimhusisha
kuihujumu timu na ujio wa mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi huku
akitajwa yeye kuondoka kwenye usajili uliopita.
Alisema kuwa Tambwe ameathirika kisaikolojia na
ameonyesha kutokuwa na furaha ndani ya Simba hivyo ni vyema viongozi wa
klabu hiyo wakafanya uamuzi sahihi wa kumruhusu kwenda kuichezea timu
nyingine ambayo ataona inamfaa ili kunusuru kiwango chake.
“Niliwahi kuzungumza na Tambwe na aliniambia kuna
timu nyingi zinamtaka, hayo yalitokea baada ya kuwepo na maneno mengi
juu yake, mpaka sasa Tambwe bado hajakaa sawa kisaikolojia na hana
furaha ndani ya timu, mimi kama kocha nafahamu tatizo linaloweza kutokea
kwamba anaweza kushindwa kucheza kabisa,” Phiri alisema.
“Ni vyema viongozi wamruhusu kwenda timu nyingine
kama atapata kuliko kumlazimisha kuwepo ndani ya Simba, hali hiyo
itamshusha kiwango chake kabisa, raha ya kazi ufanye pale ambapo unaona
una furaha napo.
“Tambwe bado ni kijana mdogo na uwezo wake ni
mkubwa ila kwa sasa kavurugikiwa. Kuendelea kumbakiza Simba ni sawa na
kutaka kuua kipaji chake, siwezi kushauri hivyo.”
Lakini kwa upande wake, Tambwe aliliambia
Mwanaspoti akiwa Burundi kwa kusema: “Bado nina mkataba na Simba ambao
umebaki muda mfupi kumalizika, sijafanya mazungumzo yoyote na viongozi
wangu juu ya kuongeza mkataba mpya, hivyo nitarudi huko Novemba 30
kumalizia mkataba wangu na mengine yatafuata.”
Phiri alipeleka ripoti yake ambayo ilijadiliwa na
kupitishwa huku akipendekeza wachezaji kutoka Mtibwa Sugar; Ame Ally na
Hussein Kessy, Danny Mrwanda (Polisi Moro) na Mganda Dan Sserunkuma wa
Gor Mahia ya Kenya.
Hata hivyo Phiri alitoa baraka kwa viongozi wake
kumsaidia kusaka wachezaji watakaoisaidia Simba katika safu ya
ushambuliaji, kiungo, beki ya kati na pembeni ambapo alihitaji mchezaji
mmoja mmoja kila safu kwa maelezo kwamba sio rahisi kwake kuwafahamu
wachezaji wote kwani mechi walizocheza ni chache.
Viongozi wa Simba walianza mchakato wa kusaka
wachezaji ambapo tayari wamefanya mazungumzo na Emeh Izuchukwu
anayeelezwa kuwa ameomba mwenyewe kurudi Simba, mabeki Salum Kimenya,
Nurdin Chona (Prisons), kiungo Deus Kaseke (Mbeya City), Said Morad
(Azam) na kipa Juma Kaseja (Yanga).
Aidha, kuna habari kwamba Sserunkuma anaweza
kuziba nafasi ya Tambwe ingawa Mkenya Raphael Kiongera ambaye anatarajia
kwenda kufanyiwa upasuaji wa goti na kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu
jambo ambalo Phiri amesema linaweza kuigharimu timu.
Wengine wanaotajwa kutemwa ni Amri Kiemba ambaya
anaandaliwa mpango wa kupelekwa kwa mkopo Azam kama watafikia
makubaliano, Nassoro Masoud ‘Chollo’, Uhuru Seleman, Harun Chanongo, Ivo
Mapunda, Joram Mgeveke na Pierre Kwizera.
- MwanaSpot
- MwanaSpot
Post a Comment