Vurugu hizi za machinga Mwanza zitafutiwe dawa

Katuni
Vurugu kubwa zilitokea katika maeneo mbalimbali ya katikati ya jiji la Mwanza juzi kufuatia mgogoro baina ya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama 'Wamachinga' na mamlaka za jiji hilo.
Maduka kadhaa yalilazimika kufungwa. Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walilazimika kutumia nguvu ya ziada kutuliza hali iliyokuwapo. Wakapiga mabomu kadhaa ya machozi, hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwa vurugu ya Lumumba, Rwagasore, Market, Pamba, Nyerere, Kituo cha Chai na Soko Kuu.

Ilielezwa katika moja ya taarifa zilizoripotiwa na gazeti hili jana kuwa vurugu hizo zilianza saa 6:30 mchana baada ya FFU kuingia mitaani kuwaondosha Wamachinga waliokuwa wamekaidi amri ya jiji ya kuwataka wasifanye biashara katika mitaa wasiyoruhusiwa na pia kuwazidi nguvu mgambo wa jiji hilo.

Wamachinga walilazimika kukimbia huku na huko. Makundi ya wananchi waliokuwa wakipita ama kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato wakawa miongoni mwa waathirika. Nao walikimbia kunusuru maisha yao, huku wengine wakipoteza mali zao mbalimbali.

Sisi tunasikitishwa na taarifa za kuwapo kwa vurugu za aina hii. Tunapinga kuwapo kwa matukio ya aina hii kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa jamii. Vurugu zinawaletea usumbufu watu wengi wakiwamo wale wasiokuwa na hatia kama wanafunzi. Zinaathiri shughuli za kibiashara na mbaya zaidi, zinatangaza vibaya jiji la Mwanza na hivyo kutishia shughuli za uwekezaji katika maeneo ya kati ya jiji hilo.

NIPASHE tunatambua kuwa mbali na kutishia usalama wa raia na mali zao, vurugu kama za juzi jijini Mwanza zitakuwa zimesababisha athari kubwa kwa uchumi wa jiji hilo.

Maduka makubwa yaliyolazimika kufungwa yalipoteza fursa za kuingiza kipato ambacho mwisho wa siku kingeongeza makusanyo ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Cha kusitikisha zaidi, vurugu za aina hii jijini Mwanza zinaelekea kuwa ni jambo la kawaida. Baadhi ya watu sasa wanazichukulia kuwa ni sehemu ya maisha ya jiji hilo. Kwamba, kila baada ya muda fulani kupita, ni lazima kuwe na vurugu jijini humo; na tena ni lazima ziwahusishe Wamachinga na uongozi wa mamlaka ya jiji.

Siku tano tu kabla ya tukio la juzi, kulitokea pia vurugu nyingine baina ya Wamachinga na mamlaka za jiji la Mwanza. Na kabla ya hapo, kulishatokea vurugu nyingine kadhaa za namna hiyo, zote zikihusisha ubishani uliopo kuhusu mahala pa kufanyia biashara Wamachinga.    

Sisi tunaamini kwamba vurugu za aina hii, ambazo kuna wakati hutokea pia jijini Dar es Salaam na kwenye miji mingine nchini hazipaswi kuachwa zitokee. Ni lazima sasa itafutwe njia ya kudumu kuhakikisha kwamba watu wa jiji la Mwanza hawahatarishiwi maisha yao na mali zao kutokana na uwapo wa vurugu hizi.

Mambo mengi ya maendeleo hurudi nyuma kwa kasi pindi vurugu zinapokuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku.Kwa sababu hiyo, uongozi wa jiji la Mwanza, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo jijini humo wanapaswa kushirikiana katika kupata jibu sahihi la namna bora ya kujiepusha na hali hiyo.

Sisi tunadhani kwamba mkakati mmojawapo uwe ni kushughulikia matatizo yao kisayansi, kwa maana ya kutafuta chanzo cha vurugu hizo za mara kwa mara na kutoa majawabu yatakayofuta uwezekano wa kutokea vurugu nyingine katika siku chache zijazo.

Ikumbukwe kuwa amani ni muhimu kwa ustawi wa jiji hilo lenye shughuli nyingi za kiuchumi. Kutembeza virungu na kupiga mabomu hakutoshi kuwa suluhu ya vurugu hizi. Bali, matumizi hayo ya nguvu yanapaswa kutumiwa kwa dharura tu ili kutoa nafasi ya kutafutwa kwa suluhisho ka kudumu.

Mathalan, sisi tunadhani kwamba njia mojawapo ya kujiepusha na vurugu za aina hii ni kuhakikisha kwamba jiji linatenga maeneo maalum kwa ajili ya Wamachinga. Katika kutekeleza jambo hili, uongozi wa jiji uwashirikishe Wamachinga ili mwisho wa siku, mradi wowote wa aina hiyo uwe kwa manufaa ya walengwa na siyo matajiri wachache kuhodhi maeneo kama ilivyowahi kutokea katika baadhi ya maeneo.  

Na baada ya yote hayo kufanyika, mamlaka ya jiji la Mwanza iweke ulinzi madhubuti katika maeneo yote yasiyoruhusiwa kufanyika biashara za Wamachinga na wote watakaokiuka agizo wachukuliwe hatua za kisheria kungali mapema. Kamwe wasiachwe waweke makazi, wazoee na kisha waondoshwe kwa kutegemea operesheni za dharura. Itafutwe suluhu ya kudumu.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post