Phiri ameiongoza Simba katika michezo sita ya ligi kuu na kutoa sare yote.
Akizungumza na Championi Jumamosi, kocha huyo alisema kuwa atahakikisha anashinda mchezo huo kwa faida ya klabu na pia ili ahakikishe kuwa anarejea nyumbani, Zambia akiwa na walau ushindi mmoja alioupata katika Ligi Kuu Bara.
Phiri aliyasema hayo alipokuwa anapitia gazeti la Championi Ijumaa na kukutana na makala juu ya ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire na kusema kuwa atahakikisha anamnyamazisha mtu huyo anayetamba kuwa wataibuka na ushindi dhidi ya Simba watakapokutana kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Phiri atakwenda nchini kwao kwa mapumziko baada ya mchezo huo, kipindi ligi itakaposimama kupisha usajili wa dirisha dogo.
“Ni lazima tuibuke na ushindi katika mchezo huo ili Wanasimba wawe katika hali nzuri, maana wanataka kuiona timu ikishinda lakini pia na mimi nataka nirudi mapumzikoni nikiwa na ushindi katika mechi za ligi kuu,” alisema Phiri.
إرسال تعليق