RC Dar afichua siri ya rushwa ya viwanja

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amesema rushwa miongoni mwa baadhi ya wataalamu wa mipango miji katika sekta ya ardhi ndiyo inayokwamisha maendeleo.
Akifungua mkutano wa bodi ya usajili wa wataalamu wa mipango miji jijini Dar es Salaam jana, Sadiki alisema sekta ya ardhi imegubikwa na urasimu  kutokana na kuwapo kwa baadhi ya watalaamu wasio waaminifu kushirikiana na baadhi ya viongozi kula njama ya kugawa viwanja kwa kupewa rushwa.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wataalamu hao wanakula njama na kukubali watu wenye fedha nyingi kuhodhi viwanja vinavyopimwa na halmashauri halafu wananchi wa kawaida wanakosa viwanja.

Aliongeza kuwa ipo minong`ono kwamba tatizo hilo la rushwa katika ardhi ni cheni ambayo imeanzia kwa viongozi wa chini hadi juu hususani kwa kamati za mipango miji ambao wamekuwa wakila njama ya kugawa viwanja kwa wingi kwa watu wachache wenye fedha ambao nao wamekuwa wakiviuza kwa bei ya juu.

“Ipo minong`ongo kwamba wataalamu hasa katika kamati za mipango miji wanashirikiana na baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya chini hadi juu, badala ya kuuza viwanja kwa kila mwananchi anayehitaji, lakini wao wanawapa viwanja vingi matajiri  halafu wao baadaye wanauza kwa bei ya juu,” alisema na kuongeza:

“Hii inauma sana na haiwezi kuvumilika kwa sababu lengo la serikali ni kuhakikisha inagawa viwanja kwa wananchi wote kwa bei ambayo imepangwa ili kila mmoja awe na makazi bora, kwa mwendo huu mipango miji yetu haitafikiwa, itakuwa ni kwa matajiri tu na tutazidi kuchelewesha maendeleo.”

Kadhalika,  alisema mpaka sasa baadhi ya maeneo ambayo matajiri hao walihodhi viwanja kwa nia ya kuja kuuza kwa bei ya juu, yamekuwa ni mapori baada ya kukosa wateja ambao wameshindwa kumudu gharama za kununua viwanja hivyo.

Alisema jambo hili halikubaliki na linatakiwa kukomeshwa mara moja ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watumishi wasio waaminifu.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم