![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhfVupog7c62b_sw5RPVKCDeo84UtS82h_hkDOPk7pzLTQSDDk9CR3z0IbkzeELcWBpM6rTX4JGBHTTVuc1JpNCIS76uzopoqJVO2PWaEQ8t_tbAKdsUay5EreSyIW3u1r9rGfMhribvU0/s1600/wpid-Prime-Minister-Mizengo-Pinda.jpg)
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kuunda timu ya watu 10 kutoka kada
tofauti wakiwemo viongozi wa dini ambao watapewa jukumu la kufanya kazi ya usuluhishi
kwenye vijiji vyenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto
mkoani Manyara.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili,
Novemba 23, 2014) wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwenye ibada ya
kumweka wakfu Askofu wa sita wa Dayosisi ya Central Tanganyika ya Kanisa la
Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la
Roho Mtakatifu, mjini Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye kwenye ibada
hiyo alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi
kwa matibabu alisema: “Hali ya Kiteto ni changamoto kama alivyosema Askofu
Mkuu, Dk. Chimeledya lakini inahitaji ufumbuzi kutoka kwa wadau tofauti na siyo
Serikali peke yake... inataka Serikali, wananchi, vyombo vya dola lakini pia na
Kanisa lazima lihusishwe ili kujenga upya maadili ya jamii.
“Ukiwa na kundi kubwa la watu ambao
hawamwogopi Mungu ni tatizo. Na hii ndiyo iliyoko kule. Watu wanauana kwa
sababu ya hasira, ni hasira gani hiyo inayokufanya usiogope kutoa roho ya
mwenzako,” alihoji.
Alisema timu itakayoundwa itapewa
jukumu la kufanya usuluhishi na kupata maridhiano (reconciliation) kijiji kwa
kijiji huku ikipeleka ujumbe wa amani. “Tunataka kutumia Kiteto kama mradi wa
majaribio (pilot project) kwenye suala la kutafuta amani kwenye maeneo kama
haya,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema wilaya ya Kiteto
inaingiliana na mikoa mitano ambayo ni Tanga (Kilindi), Morogoro (Gairo);
Dodoma (Kongwa) Manyara (Simanjiro) na Arusha (Monduli) hali ambayo inachangia
kuwepo na muingilianio mkubwa wa kijamii.
Waziri Mkuu alitaja hatua nyingine
zitakazochukuliwa na Serikali kuwa ni kupima ardhi inayogombewa yenye ukubwa wa
hekta 133,000 na kuigawa kwa wafugaji ili wafuge kwa mtindo wa ranchi na
inayobakia igawiwe kwa wakulima. Vilevile, Waziri Mkuu alisema idadi ya vituo
vya polisi itaongezwa kwenye miji midogo badala kutegemea kituo kimoja tu cha
polisi kilichopo Kibaya.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Jacob Chimeledya ambaye alisema Serikali ina
wajibu wa kulinda maisha ya kila Mtanzania na kutoa mfano wa wilaya ya Kiteto
ambako alisema hakuna amani kwa sababu watu wanauana hovyo.
Katika hotuba yake ya kumkaribisha
Waziri Mkuu, Askofu Chilongani alisema ameanza kukosa usingizi kutokana suala
la umaskini na kukosekana mfumo wa pensheni miongoni mwa wachungaji na makasisi
wa kanisa hilo hasa wa vijijini ambao alisema hawana kipto cha uhakika.
“Makasisi na wachungaji hawa wanahudumia
Watanzania wote, wanachopata ni kiasi kidogo mno kuweza kuweka kwenye mifuko
kama NSSF, bado pia wana mahitaji yao, wanatakiwa wawasomeshe watoto wao...
natamani kuwe na mfumo ambao utawawezesha kupata pensheni ili wanapostaafu
wajikute hata wana vibanda vya uhakika vya kuishi na familia zao,” alisema na
kushangiliwa na mamia ya wachungaji waliohudhuria ibada hiyo.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa Serikali
za Mitaa, Dk. Chilongani aliiomba Serikali isimamie zoezi hilo liwe huru na la haki
na kuhakikisha linaisha kwa amani. “Niwasihi pia Watanzania wenzangu, wawachague
viongozi waadilifu, wasiwachague viongozi ambao wanakimbilia uongozi au wenye
kudhani kuwa ubunge au udiwani ni halali yao na siyo dhamana kutoka kwa
wananchi,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, NOVEMBA 23, 2014.
إرسال تعليق