Dar es Salaam. Tanzania ni nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki
katika kuvutia uwekezaji kutokana na sera iliyopo ikiwamo kudhibiti
mfumuko wa bei.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa
Bodi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Umoja (UTT), Profesa Joseph Kuzilwa,
wakati akifungua Mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa wawekezaji wa Mfuko wa
Umoja.
Alisema mbali na Tanzania kushika nafasi ya kwanza, pia ni ya nane kwa Ukanda wa Jangwa la Sahara kwa uwekezaji.
Katika mkutano huo, Profesa Kuzilwa alisema mfuko
huo umekua kwa kiwango cha asilimia 51.2 kutoka Sh118.3 bilioni mwaka
2012/13 hadi kufikia Sh178.9 bilioni mwaka huu.
“Idadi ya wawekezaji kwenye mfuko huu imeongezeka
na kufikia 117,471 kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, mwaka huu na
kwamba Mfuko wa Umoja pekee umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 51.3
kutoka Sh107.20 bilioni hadi kufikia Sh162.2 bilioni na wawekezaji
kwenye mfuko huo walioongezeka kutoka 106,266 hadi 107,376,” alisema
Profesa.
Aliitaja changamoto inayowakabili kuwa ni
mabadiliko ya teknolojia yaliyosababisha meneja wa mfuko kuendelea
kuwekeza katika tehama ili kuendana na ukuaji wa soko na kufikia
matarajio ya wawekezaji.
Alisema utekelezaji wa malengo ya uendeshaji wa
mifuko umekamilisha mpango mkakati wa miaka mitano na unatoa vipaumbile
na mikakati ya uendeshaji wa mifuko.
“Mikakati iliyopo ni kuendeleza uwekezaji katika
Tehama ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji pamoja na kuwafikia
wawekezaji wengi zaidi na kuendelea kufanya upembuzi wa fursa katika
soko la Ukanda wa Afrika Mashariki”aliongeza.
Alisema mfuko ya uwekezaji una aina tano ambazo ni
mfuko wa Umoja, Mfuko wa wekeza maisha, mfuko wa watoto, mfuko wa
kujikimu na mfuko wa Ukwasi.
Alisema Dhamana ya uwekezaji Tanzania inaendelea kufanya utafiti juu ya njia bora, rahisi na
zilizo na ufanisi katika kuwawezesha wawekezaji
katika mfuko wa umoja kupata gawio na matokeo ya utafiti na maandalizi
yatawasilishwa kwa wawekezaji pindi itakapokamilika
- Mwananchi
إرسال تعليق