TLS kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi

Chama cha Sheria Tanganyika (TLS)
 Chama cha Sheria Tanganyika (TLS), kimekusudia kutoa huduma zake bure kwa Watanzania kama njia ya kuwasaidia kujua njia ya kutetea haki zao na kuwajengea uwezo wa kufahamu masuala mbalimbali ya sheria.  
 
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho Charles Rwechingura, alisema huduma hizo zitaanza kutolewa rasmi Desemba mosi hadi 13.
 
Huduma hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya saba ya chama hicho ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma, Desemba 6.
 
Alisema kupitia kitengo cha msaada wa kisheria wananchi wasio na uwezo wa kukidhi gharama za kuendesha kesi watasaidiwa kupata ushuri wa kisheria sanjari na Mawakili wa kuwawakilisha mahakamani bila gharama yoyote.
 
Alifafanua huduma hizo zitatolewa katika maeneo tofauti ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, kama vituo vya Magereza, Polisi, Masokoni, Vyuoni, Hospitalini na Mahakamani, lengo ni kusimamia, kuhakikisha Watanzania  wanapata uelewa juu sheria. Aliitaja mikoa itakayotoa huduma hiyo kupitia vituo vilivyopangwa ni mkoa wa Arusha, Dodoma, Mwanza, Iringa, Mbeya, Tanga, Tabora, Mtwara, Songea, Mara ikiwamo Dar es Salaam.
 
“Tutaanza mwezi wa msaada wa kisheria ambapo tutatoa msaada huo kwa njia mbalimbali katika mikoa 12, ni vyema kueleza kuwa katika kipindi hiki cha miaka 60, tumehakikisha tunasimamia haki na utawala wa sheria nchini,” alisema Rwechungura.
 
Mhaziri wa chama hicho, John Seka, alisema chama kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Watoto (Unicef), kimeanzisha mradi ambao umejenga mahakama ya watoto mkoani Mbeya, itakayosimamia kesi zao.
 
“Hatufurahishwi na adhabu ya watoto kulazwa mahabusu, kisheria hatakiwi kulala bali  kusomewa kesi yake na kuondoka mahakamani, hivyo tumejenga kituo, tutaweka na  mawakili wawili watakaowasaidia watoto walio katika ukinzani na sheria bure,” alisema Seka.
 
Pia, chama hicho kimejipanga kuboresha matawi yake ili huduma zitakazotolewa ziendane na matakwa ya wananchi, vilevile kitarekebisha sheria ya uwakili na ile ya TLS, ili kupambana na utovu wa maadili kwa Mawakili.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم