Tuweke propaganda pembeni, tuelekeze nguvu kujenga Taifa

Tuliambiwa kwamba Abdulrahman Kinana ni mtu hatari sana kwa mbinu za kisiasa, anaweza kuviyumbisha vyama vya upinzani na hata kuvifuta kabisa. Dalili zimeanza kujitokeza.
Asiyefahamu historia ya Taifa letu ya enzi za chama kimoja na imani kubwa tuliyokuwa nayo kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ndiye anaweza kushangaa kuwakuta watu wengi wana kadi za Chama cha Mapinduzi (CCM).
Swali ni je watu hawa bado ni wanachama hai wa CCM? Binafsi sikumbuki kadi hii iko wapi? Na wala sina kumbukumbu nimeilipia kadi hii hadi lini?
Uhodari wa Kinana, unaelekea kulenga kuviyumbisha vyama vya upinzani kwa lengo la kukipatia chama chake uhai mpya.
Pia, kwa bahati mbaya watu wetu bado wanakwenda kwa mkumbo bila kukaa chini na kutafakari kwa kina.
CCM imelitawala Taifa letu miaka yote na leo tuna zaidi ya miaka 50 ya uhuru lakini Tanzania bado ni nchi ya watu maskini kupindukia, Serikali ya CCM imeshindwa kutuletea Tanzania yenye neema na maisha bora kwa kila mwananchi. Hivyo tunapojadili sifa za viongozi tujadili mambo ya msingi na siyo vinginevyo.
Inaweza ikawastaajabisha baadhi kusikia kuwa tujadili mambo ya msingi wakati ambapo taifa letu lina miaka zaidi ya hamsini tangia liwe huru.
Baadhi wanaweza kufikiri kuwa tumeshachelewa. Bado kuna nafasi kubwa kuangalia tulipo sasa miaka hamsini baada ya uhuru na kurekebisha sehemu muhimu ili kuwawezesha Watanzania kuwa na ‘kesho bora’.
Tuwekeze kwenye afya
Tukianza na afya, haihitaji fizikia ya roketi kufahamu kwamba wananchi wenye afya watafanya kazi kwa nguvu zao zote ili kuongeza tija na hatimaye pato la taifa. Kinyume chake ni maafa.
Ni muhimu kwa Serikali ya awamu ya nne kuweka kipaumbele na kufanya jitihada za makusudi kuboresha huduma za afya kwa wananchi siyo tu kwa kujenga majengo mengi ya hospitali, bali kuboresha mazingira ya watumishi wake na upatikanaji wa dawa.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم