Na Saleh Ally
Mshambuliaji
Mbwana Samatta anaondoka TP Mazembe ya DR Congo na hii si hadithi tena,
Meneja wake, Jamal Kisongo amethibitisha hilo.
Awali,
taarifa zilizolifikia gazeti hili na kufanya uchunguzi kwa wiki mbili,
zilionyesha Samatta alikuwa anawaniwa na timu tatu za Ulaya, mbili
kutoka nchini Ufaransa, tena zinashiriki ligi kuu nchini humo League 1.
Lakini
jana, Meneja wake, Jamal Kisongo akathibitisha hilo kwa kusema tayari
wamekuwa na mazungumzo marefu na uongozi wa TP Mazembe na mmiliki wake,
bilionea Moise Katumbi amekubali kutoa ruhusa.
“Yalikuwa
mazungumzo ya kina na marefu kiasi, lakini mwisho tumefikia mwafaka
kwamba Samatta anaondoka TP Mazembe na anakwenda Ulaya.
“Kumekuwa
na mtikisiko mkubwa ndani ya Mazembe, wengi hawakutaka aondoke. Lakini
mkataba tulioingia mwanzo umembana Katumbi, amekubali Samatta aondoke
Mazembe,” alisema Kasongo, akionyesha kujiamini.
Kasongo
ambaye aliongozana na Samatta hadi Lubumbashi, DR Congo ambako aliingia
mkataba na timu hiyo kwa mara ya kwanza, amesema hadi mwezi ujao
kitakuwa kimeeleweka.
“Suala la
kuwa majeruhi ndiyo limemchelewesha Samatta, lakini atalazimika
kusubiri wiki tano alizopewa na daktari. Ndiyo maana nilizuia asirudi
Mazembe, sikupenda atumike angeweza kuumia tena.
“Anatakiwa
kwenda Ulaya, nisisitize si majaribio na wakala wake ni mtu mkubwa tu
nchini Ufaransa, hivyo atalishughulikia suala hilo na kila kitu kinaenda
vizuri.”
Kama
ilivyo kwa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, Samatta amekuwa
mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Mazembe na kumekuwa kuna ugumu
kumng’oa Lubumbashi hadi juhudi za Kisongo zilipozaa matunda.
Alijiunga na Mazembe misimu mitatu iliyopita akitokea Simba ya Dar es Salaam.
Salehjembe.
إرسال تعليق