
MENGI yamesemwa kuhusu muungano wa vyama vya CHADEMA (CDM), CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Umoja wa kutetea Katiba ya Wananchi
(UKAWA). Kama mara mbili hivi huko nyuma niliandika makala za kuwataka
wapinzani waunganishe nguvu zao ili kukiondoa CCM madarakani kwenye
Uchaguzi Mkuu ujao.
Nilipendekeza waachiane majimbo ya uchaguzi kwa vyama vyenye wafuasi
wengi zaidi ya vingine. Ndivyo ilivyokubaliwa hivi karibuni kwenye
mkutano wa hadhara pale Jangwani jijini Dar es Salaam. Viongozi wa vyama
nilivyovitaja hapo juu walitia saini makubaliano ya kudumisha sera za
vyama vyao na kuchukua mambo yanayofanana ili viwe na kauli ya pamoja.
Ni hamu ya Watanzania kuona jinsi vyama hivyo vitakavyotekeleza ahadi
walizowekeana mbele ya maelfu ya watu waliokuwa Jangwani na mamilioni
walioshuhudia tukio hilo kupitia ITV. Wanataka utekelezaji wa dhati na
si ngonjera walizozoea kutoka kwa wanasiasa wakati hali zao zikizidi
kudidimia (rudi nyuma kimaendeleo) kila uchao. Twajua mwanzo ni mgumu
lakini wakikusudia kuwakwamua wananchi katika uduni walionao,
watafanikiwa Inshallah.
Katika makubaliano saba ya UKAWA, mawili ndio yatakayothibitisha kama
kweli vyama hivyo vimedhamiria kuwa na umoja wa dhati utakaoitoa nchi
katika umasikini ingawa tuna utajiri mkubwa wa maliasili. Muhimu ni
vyama hivyo kuweka kando tofauti zao ili kuwa na itikadi moja kwa
manufaa ya nchi.
Suala la wagombea, hasa urais, nalo lapaswa kuamuliwa kwa tahadhari
kubwa kwani kuna hatari au tamaa ya vyama viwili kati ya vinne
vilivyokubaliana, kutaka mgombea wao apendekezwe katika nafasi hiyo.
Lazima viongozi wawe tayari kukubaliana kutokubaliana kama alivyosema
Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) kuwa hawakuungana kutafuta urais bali ni
kuweka ‘silaha’ (nguvu) zao pamoja kwa lengo la kuwapatia wananchi
Katiba bora. “Wanaodhani tutagombana kwa sababu ya urais, hawafahamu
dhamira yetu. Kuhusu nani atakuwa Rais, Profesa Lipumba anasema si hoja
kwani hoja ni kuwa na Katiba bora.
Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) amegombea urais mara nne tangu uchaguzi
wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi mwaka 1995. Katika uchaguzi ule
alipata kura 418,973 (asilimia 6.43) na kushika nafasi ya tatu nyuma ya
Augustine Lyatonga Mrema (aliyekuwa NCCR-Mageuzi) kwa kupata silimia 40
ya kura. Mgombea wa CCM alishinda kwa kura 4,026,422 (asilimia 61.82).
Uchaguzi wa mwaka 2000 Lipumba alishika nafasi ya pili alipopata kura
1,329,077 (asilimia 16.26) wakati mgombea wa CCM alipata kura
5,863,201(asilimia 71.74).
Mwaka 2005 Lipumba alipata kura 1,327,125 (asilimia 11.68), Freeman
Mbowe (CHADEMA) alipata kura 668,756 (asilimia 5.88) akishika nafasi ya
tatu wakati Dk. Emmanuel Makaidi (NLD) alipata kura 21,574 (asilimia
0.19) na mwenzao wa CCM kupata kura 9,123,952 (asilimia 80.28). Uchaguzi
wa mwaka 2010, Dk Willibrod Slaa (CHADEMA) aliyeingia kwa mara ya
kwanza alipata kura 2,271,941 (asilimia 26.34) na Lipumba alipata kura
695,667 (asilimia 8.06) wakati mgombea wa CCM akipata kura 5,276,827
(asilimia 61.17).
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa anasema wamefungua ukurasa
mpya na wanaosema watasambaratika wacha waseme ila wao wanasonga mbele.
Kilichowaunganisha ni kile kinachotakiwa na wananchi … kupata Katiba
Mpya yenye masilahi kwao. Anasema hawatakuwa kama Samweli Sitta na rais
wake , Jakaya Kikwete, waliotumia madaraka ya umma kwa masilahi binafsi.
Wamekubaliana kusimamisha wagombea wa pamoja katika chaguzi zote.
Vyama hivyo vitasambaza mwongozo mikoani kuwaelekeza viongozi wao mambo
yanayotakiwa. Lengo ni kusema ‘hapana’ katika kura ya maoni ya Katiba
Inayopendekezwa kwa vile haikuzingatia maoni ya wananchi.
Wanatakiwa kumweka mgombea wa urais anayekubalika, ‘anayeuzika’ na
mwenye uwezo wa kukabiliana na mgombea wa CCM. Bila inda wala unafiki,
atakayependekezwa afanyiwe kampeni ya kiungwana kwa hoja za maana.
Wajadili masuala ya maendeleo badala ya watu na hulka zao. Twamtaka Rais
atakayethibitisha maneno ya Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ziarani
China kuwa ana hakika nchi yetu itapata kiongozi (Rais) mwingine bora
kuliko yeye atakayeiongoza vizuri nchi yetu. Mwaona? Kikwete mwenyewe
anakiri yeye si bora. Kila kunapokuwa na tatizo kubwa nchini yeye huruka
kwenda ughaibuni!
Katika chaguzi za Serikali za Mitaa, Madiwani, Wabunge na Wawakilishi
(Zanzibar), vyama visiwe na tamaa ya kuweka wagombea katika maeneo
ambayo havifahamiki kwa wakazi wa huko. Kwa mfano, itakuwa kukipa CCM
ushindi kule Zanzibar (Unguja na Pemba) kuwasimamisha wagombea wa vyama
vingine ambako yajulikana wazi kuwa ngome ya CUF.
Vivyo hivyo kwa Tanzania Bara kuna maeneo yanayofahamika fika kuwa
ngome za vyama tofauti. Hapa ni muhimu vyama viache choyo na tamaa ya
kutaka kuweka wagombea hata kama havifahamiki vizuri. Twasikia sasa
kwenye baadhi ya mikutano ya CHADEMA wananchi wanaambiwa wakichague
chama hicho! Hapana. Waambiwe kumchagua mgombea atakayependekezwa na
UKAWA kutoka chama chochote. Huo ndio umoja na si vinginevyo.
Msomaji fulani alinitumia ujumbe mfupi wa simu akisema: “UKAWA
wanatakiwa kujiuza badala ya kutegemea kura za chuki dhidi ya CCM. Mara
nyingi ili kuking’oa chama tawala hupigiwa mfano wa Kenya. Mimi
hujiuliza kwani sasa Kenya chatawala chama gani? UKAWA haufanani na
umoja wa Kenya: Chaguzi za vyama vingi Tanzania zimefanyika mara nne.
Upinzani haujavuka asilimia 40, pia walopigia upinzani hawajafikia
milioni tatu.
“Kenya Daniel arap Moi alishinda kwa asilimia 40 hivyo upinzani
ulipoungana wakashinda kwa asilimia 60. Uhuru Kenyatta akabadili
‘configuration’ (sura; namna ya kupanga) akashinda. Mazingira ya Kenya
na Tanzania ni tofauti. UKAWA wasitegemee CCM kujifunga wenyewe!”
Msomaji huyo anakumbusha usemi wa Kiingereza uliotokana na Mrumi
Cicero (1578) aliyeandika ‘Birds of a feather flock together.’
Akaniambia pia katika Kemia (zamani alipokuwa anasoma), walifunzwa kuwa:
Muungano kwa ‘chemical reaction’ ni kwamba vilivyoungana huwa kitu
kipya na sifa mpya. Kwa ‘physical reaction’, vilivyoungana hubaki na
sifa zao; pia ni rahisi kuvitenganisha. Katika bayolojia, kukua kwa
‘intercalation’ hakurudi kama mwanzo. Kwa ‘crystalisation’ hakubadili
sifa zake za mwanzo. Katika bayolojia pia kuna ‘growth by
disintegration’. Huku ni kukua kwa kukatikakatika ambako ni udhaifu
kwani kikuacho hivyo mwisho hupotea kabisa. Wapinzani wapaswa kusoma
sehemu hii kwa tafakuri tunduizi ili wajitambue walivyo, walipo na
wanakoelekea.
Endapo wapinzani watafanikiwa katika ushirika wao, basi uwe wakati
mwafaka wa kuunda chama kimoja chenye nguvu zaidi badala ya kuwa na
wingi wa vyama visivyokuwa na malengo wala mwelekeo. Husemwa katika
msafara wa mamba kenge nao huwamo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nnape Nnauye anasema makubalino ya
ushirika wa UKAWA ni kaburi la vyama hivyo. “UKAWA ni bomu
litakalowalipukia … sijaona jambo jema katika ushirikiano wao. Huo ni
mwanzo wa kumomonyoka kwa vyama vya upinzani na vitapoteza utambulisho
wao …” Ushirikiano ni hali ya mchanganyiko wa watu katika kufanya jambo;
tangamano. Hata hivyo Nnape asema hajaona jambo jema katika ushirikiano
wao! Hajui kuwa ‘umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu?” Wahenga walisema
“Akuchukiae hakosi ila (kasoro katika umbo au tabia; hitilafu) ya
kukutia.”
Hadharani ni lazima Nnape na wenzake waseme hivyo kuwazubaisha
wananchi. Wanapokuwa kwenye mikutano yao ya ndani, ushirikiano wa UKAWA
na hatima ya CCM ni mambo yanayowaumiza vichwa. Aidha kashfa ya rushwa
miongoni mwa waliotangaza kugombea urais, ufisadi na ubadhirifu mkubwa
serikalini pia ni mambo yanayowanyima usingizi na kuwakatisha tamaa.
Chama hicho sasa chatafuta chama cha kufa nacho. Baadhi ya vyama
vinavyojiita vya ‘upinzani’ vyahoji ushirikiano wa UKAWA kwa madai kuwa
vinavunja sheria! Vingine vyasema kazi kubwa iliyo mbele yao ni kukipiga
vita CHADEMA! Kwao, huo ndio ‘upinzani!’
“Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana, naam, viko saba vilivyo
chukizo kwake: macho ya kiburi, ulimi wa uongo, na mikono imwagayo damu
isiyo na hatia; moyo uwazao mawazo mabaya; miguu iliyo myepesi
kukimbilia maovu; shahidi wa uongo asemaye uongo; naye apandaye mbegu za
fitina kati ya ndugu.” (Mithali 6:16-19)
- Tz Daima
إرسال تعليق