Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo nchini yalikosa
umeme kwa siku nzima ya jana, kitendo kilichotafsiriwa na wengi kwamba
ni hujuma ili kuwafanya wasione mjadala wa kashfa ya IPTL uliokuwa
ukiendelea bungeni Dodoma jana.
Taarifa zilizokifikia chumba cha habari, zilieleza
kuwa maeneo mengi katika miji ya Mwanza, Arusha, Tanga na baadhi mikoa
mingine hayakuwa na huduma hiyo.
Pia, baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam na Morogoro
hayakuwa na umeme kwa kutwa nzima ya jana na kusababisha malalamiko
mengi ya wananchi.
Chumba cha habari cha Mwananchi, kutwa nzima jana
kilikuwa kikipokea simu mbalimbali za wananchi wakitaka kufahamu sababu
za kukatika kwa umeme wakati ikifahamika kuwapo kwa mjadala huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba
alithibitisha kukatika umeme katika maeneo mengi ya nchi lakini
alikanusha kuwa siyo hujuma kuwafanya wananchi wasipate matangazo ya
moja kwa moja kutoka Dodoma.
Alisema kukatika kwa umeme kunatokana na matatizo
ya moja kati ya mitambo mitatu ya kuzalisha umeme kwenye Bwawa la
Kidatu, Morogoro.
Alisema mtambo huo una matatizo ya kifaa muhimu kiitwacho gavana ambacho kilikuwa kinafanyiwa ukarabati.
“Matatizo ya mtambo huo yako wazi na
tulishatangaza kwenye vyombo vya habari kuhusu tatizo hilo na kwamba
baadhi ya maeneo yatakosa umeme leo kwa sababu ya matengenezo ya mtambo
huo.
“Hata hivi ninavyozungumza, mafundi wako kwenye
matengenezo, hata ukitaka kuhakikisha unaweza kutuma mwakilishi wako
atawakuta mafundi wakiendelea na matengenezo,” alisema.
Hata hivyo, Mramba hakutaka kuelezea wala
hakufafanua maeneo yaliyopaswa kukosa umeme kutokana na matengenezo ya
mtambo huo muhimu unaochangia katika gridi ya taifa, akieleza kwamba
tayari walishatoa matangazo kwenye vyombo vya habari.
Alisisitiza kupuuza taarifa kwamba kukatika huko
kwa umeme ni sehemu ya hujuma ili kuwanyima wananchi fursa ya kufuatilia
matukio yanayoendelea bungeni hasa kuhusu mjadala huo IPTL ambao
unaigusa Tanesco.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment