Baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
kuwasilisha bungeni ripoti kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow juzi,
tunapenda kulipongeza Bunge kwa kuipa kamati hiyo ya PAC, chini ya
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jukumu la kuchunguza na kupata
ukweli kuhusu Sh306 bilioni zinazodaiwa kuchotwa katika mazingira ya
kutatanisha kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa katika Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Tunaipongeza pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), kwa kuiwezesha PAC kupata taarifa muhimu katika
kukusanya na kuandika ripoti iliyoiwasilisha bungeni.
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), nayo inastahili pongezi kwa kuandaa na kutoa taarifa za
kina kwa PAC kuhusu Akaunti hiyo ya Tegete Escrow.
Kama wengi wanavyofahamu, ofisi hiyo ya CAG, kwa
muda mrefu sasa imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuanika wizi na
ubadhirifu wa fedha za umma, ingawa kazi yake hiyo imekuwa ikikwazwa na
mamlaka husika kutotekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti zake,
ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha wote wahusika.
Hapa hatuwezi kusahau pia kuipongeza Mamlaka ya
Kodi Tanzania (TRA), kwani ripoti ya PAC imethibitisha kwamba tatizo la
muda mrefu la upotevu wa fedha za Serikali kutokana na misamaha holela
ya kodi limechochewa na wanasiasa kuingilia kazi za mamlaka hiyo.
Pengine yafaa tujiulize hapa kama ripoti ya PAC
imeeleza ukweli, ukweli mtupu? Je, ni kweli kwamba fedha zilizowekwa
katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa fedha za umma kama baadhi ya
viongozi serikalini wamekuwa wakidai, licha ya vielelezo vilivyotolewa
katika ripoti ya PAC?
Je, kuna watu watawajibishwa? Kuna viongozi watajiuzulu kutokana na ripoti hiyo kali iliyowasilishwa bungeni?
Tunauliza maswali hayo kutokana na kuwapo orodha
ndefu ya watu wenye hadhi katika jamii ambao PAC imesema walilipwa fedha
nyingi inayosemekana ilitoka katika akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
Kama itagundulika kwamba fedha walizolipwa
zilikuwa za umma, kwamba zilipaswa kupelekwa Tanesco, waliolipwa fedha
hizo watalazimishwa kuzirudisha? Maswali haya na mengine bila shaka
yanaumiza vichwa vya Watanzania, hasa wakati huu ambao kuna mjadala
mkali kuhusu jambo hilo ndani na nje ya Bunge.
PAC imetoa mapendekezo yake, hivyo mjadala wa
mapendekezo hayo utakapomalizika, Bunge litajadili utetezi wa watu wote
waliotuhumiwa katika ripoti hiyo na kufanya uamuzi. Wananchi wengi bila
shaka watafuatilia maazimio ya Bunge kwa shauku kubwa.
Jambo la msingi hapa ni jinsi Serikali
itakavyoipokea ripoti hiyo ya PAC na mapendekezo yake, hasa baada ya
baadhi ya watendaji wake kupewa taswira hasi na kuonekana mbele ya jamii
kama maadui wa taifa na wananchi, ambao wanapaswa kuwatumikia kwa
uzalendo na moyo mkubwa? Hili ni jambo muhimu sana kwa Serikali, kwani
mpira tayari umepigwa golini kwake.
Pamoja na kwamba jana bungeni Serikali ilipewa
fursa ya kujibu hoja na tuhuma zilizoelekezwa kwake na ripoti ya PAC,
ukweli ni kwamba hadhi na heshima yake ni kitu muhimu sasa pengine
kuliko wakati wowote. Hadhi ya baadhi ya viongozi wa Serikali kwa namna
moja ama nyingine imeguswa.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment