Vurugu, ubabe kila kona

Mwanza/Dar es Salaam. Ligi Daraja la Kwanza imemaliza hatua ya kwanza, lakini nyuma yake imeacha simulizi mbaya zikiwamo za vurugu za baadhi ya timu zilizosababisha mechi kuvunjika, uzalendo uliokithiri umejitokeza kwa jina la upendeleo hasa kwa timu zinapocheza nyumbani.
Tuhuma hizo zimezihusisha zaidi timu kadhaa zinazomilikiwa majeshi nchini.
Katika tukio la karibuni, baadhi ya wachezaji wa Toto African ya Mwanza  wanadai kupigwa, kujeruhiwa na mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa timu ya Rhino Rangers ya Tabora.
Awali, matukio hayo yamewahi kuripotiwa katika vituo vya Musoma ambako Polisi Mara wamedaiwa kuhusika.
Mengine ni yale yaliyohusisha mashabiki wa Toto dhidi ya Geita Gold Sports jijini Mwanza pia Panone ya Kilimanjaro, ambayo ilidaiwa kuhusika na vurugu katika mchezo dhidi ya Polisi Mara mjini Musoma.
Kiungo wa Toto African, Emmanuel Swita amedai kupigwa kuumizwa mdomoni na kwenye mbavu na kulitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF) lisaidie kuweka ulinzi wa kutosha kwenye mechi za ligi hiyo.
Wachezaji wa Toto African na benchi lao la ufundi wamedai kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni mashabiki wa Rhino Rangers kwenye mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini humo.
Licha ya mashabiki kupigana wenyewe kwa wenyewe, lakini waamuzi waliochezesha mechi hizo nao wamekuwa wakihofia usalama wao, hasa pale mwenyeji anapofungwa, hali ya usalama huwa ndogo.
Swita ambaye amepata majeraha katika sehemu ya mdomoni na kichwani baada ya kupigwa na mashabiki hao alisema kama TFF itaendelea kuacha vitendo hivyo vifanyike,  ipo siku kutatokea maafa na kutia doa soka la Tanzania.
“Katika maisha yangu ya soka sijawahi kupigika namna ile, yaani unajua mwizi anavyopigwa, sisi tulishambuliwa  na wale jamaa wana roho mbaya sijawahi kuona. Inafaa  TFF waiangalie ligi hiyo, la sivyo itakuja kuleta mauaji nchini. ”
Alidai kuwa yeye alijinasua kwa kukimbilia kwenye gari  la wanajeshi waliomsaidia pia kumpatia huduma ya kwanza. “Hivi nimetoka hospitali,  bado nahisi maumivu makali mdomoni, meno yamelegea, kichwa bado kinauma,” alisema Swita.
Katika mchezo baina ya Geita Gold Sports na Toto African, mashabiki wa Geita walivunja lango la Uwanja wa CCM Kirumba na kusababisha vurugu kubwa. Mashabiki walichapana makonde na walinzi waliokuwa wakiwazuia kuingia bure uwanjani.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post