Mwanza/Dar es Salaam. Ligi Daraja la Kwanza
imemaliza hatua ya kwanza, lakini nyuma yake imeacha simulizi mbaya
zikiwamo za vurugu za baadhi ya timu zilizosababisha mechi kuvunjika,
uzalendo uliokithiri umejitokeza kwa jina la upendeleo hasa kwa timu
zinapocheza nyumbani.
Tuhuma hizo zimezihusisha zaidi timu kadhaa zinazomilikiwa majeshi nchini.
Katika tukio la karibuni, baadhi ya wachezaji wa
Toto African ya Mwanza wanadai kupigwa, kujeruhiwa na mashabiki
wanaodhaniwa kuwa wa timu ya Rhino Rangers ya Tabora.
Awali, matukio hayo yamewahi kuripotiwa katika vituo vya Musoma ambako Polisi Mara wamedaiwa kuhusika.
Mengine ni yale yaliyohusisha mashabiki wa Toto
dhidi ya Geita Gold Sports jijini Mwanza pia Panone ya Kilimanjaro,
ambayo ilidaiwa kuhusika na vurugu katika mchezo dhidi ya Polisi Mara
mjini Musoma.
Kiungo wa Toto African, Emmanuel Swita amedai
kupigwa kuumizwa mdomoni na kwenye mbavu na kulitaka Shirikisho la Soka
nchini (TFF) lisaidie kuweka ulinzi wa kutosha kwenye mechi za ligi
hiyo.
Wachezaji wa Toto African na benchi lao la ufundi
wamedai kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni mashabiki wa Rhino
Rangers kwenye mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassani Mwinyi
mjini humo.
Licha ya mashabiki kupigana wenyewe kwa wenyewe,
lakini waamuzi waliochezesha mechi hizo nao wamekuwa wakihofia usalama
wao, hasa pale mwenyeji anapofungwa, hali ya usalama huwa ndogo.
Swita ambaye amepata majeraha katika sehemu ya
mdomoni na kichwani baada ya kupigwa na mashabiki hao alisema kama TFF
itaendelea kuacha vitendo hivyo vifanyike, ipo siku kutatokea maafa na
kutia doa soka la Tanzania.
“Katika maisha yangu ya soka sijawahi kupigika
namna ile, yaani unajua mwizi anavyopigwa, sisi tulishambuliwa na wale
jamaa wana roho mbaya sijawahi kuona. Inafaa TFF waiangalie ligi hiyo,
la sivyo itakuja kuleta mauaji nchini. ”
Alidai kuwa yeye alijinasua kwa kukimbilia kwenye
gari la wanajeshi waliomsaidia pia kumpatia huduma ya kwanza. “Hivi
nimetoka hospitali, bado nahisi maumivu makali mdomoni, meno yamelegea,
kichwa bado kinauma,” alisema Swita.
Katika mchezo baina ya Geita Gold Sports na Toto
African, mashabiki wa Geita walivunja lango la Uwanja wa CCM Kirumba na
kusababisha vurugu kubwa. Mashabiki walichapana makonde na walinzi
waliokuwa wakiwazuia kuingia bure uwanjani.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق