Wabelgiji waja juu kompyuta kupotelea wizarani

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara kati ya Tanzania na Ubelgiji,Otieno Igogo, akipokea zawadi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza mara baada ya mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ubelgiji uliofanyika mjini Bagamoyo. Wanaoshuhudia ni balozi wa Tanzania nchini humo, Dk. Deodorus Kamala na Kamishna wa Biashara kutoka ubalozi wa Ubelgiji nchini, Ivan Korsak (Picha na Mpiga Picha Wetu)
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  inadaiwa kuikwamisha shule ya sekondari  ya mchepuo wa Sayansi ya Miono iliyopo wilayani hapa mkoa wa Pwani kupata msaada wa Sh. milioni 200 baada ya kompyuta zaidi ya 10 ilizopatiwa na kampuni ya nchini Ubelgiji kutojulikana ziliko.
Taarifa za kupotea kwa kompyuta hizo zilitolewa jana na Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Deodorus Kamala wakati wa ziara ya wafanyabishara kutoka nchini humo kwenye maeneo ya uwekezaji  EPZ wilayani hapa.

  Dk. Kamala alisema amesikitishwa na watendaji na viongozi wanaokiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwakosesha wananchi fursa ya kupata maendeleo kutoka kwa wahisani wanaojitolea kuwasaidia.

Alisema kampuni hiyo ya  Wakefield  and Cushman kwa kushirikiana na Serikali imejenga shule hiyo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Pwani na kutoa misaada.
Alisema  kutokana na   kompyuta  kutofikishwa shuleni hapo, kampuni hiyo imesitisha kuisaidia shule hiyo kwa muda usiojulikana.

Kamalla alisema baada ya Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza (pichani)  kuteuliwa kushika wadhifa huo mkoani Pwani, alimuita ofisini kwake na kumueleza  kampuni hiyo kati ya fedha  ilizoahidi kutoa, kilibaki  kiasi hicho ambacho alitakiwa kufuatilia Ubelgiji.

“Juzi kabla ya kuja Tanzania  nilikwenda  ofisini kwao  kujua wamefikia hatua ipi kumalizia hizo fedha zilizobaki nikaelezwa  hivi karibuni walikuja nchini  hadi sekondari  ya Miono na kukuta  imeanza na wamefurahi, lakini  kompyuta walizotuma  wamekuta hazipo kwa hiyo hawatatoa   fedha hizo zilizobakia hadi kompyuta hizo zifikishwe shuleni hapo,” alisema.

 Alisema walimwambia walipenda kuipatia kiasi hicho cha fedha  shule hiyo kwa ajili ya matumizi mbalimbalim ikiwamo ya  Internet na ya mawasiliano kwa mtandao wa kompyuta, lakini hawawezi kumpatia hadi kompyuta hizo zipelekwe shuleni hapo.

 Alisema aliwaahidi akiwa nchini atazungumza na Mahiza, serikali na wizara ili kujua ziliko kompyuta hizo.

Kwa upande wake,  Mahiza aliahidi  kufuatilia wizarani ili kubaini kompyuta hizo ziliko na kuonya  kama kuna ofisa  alizipokea na kuziweka ofisini au kwenye  shule nyingine, azisalimishe ofisini kwake lasivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post