Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema
kuwa fedha zote zilizopotea kutokana na ukwepaji wa kodi zaidi ya Sh26
bilioni kwenye sakata la escrow zitarudishwa na waliohusika
watachukuliwa hatua.
Pia, amemtaka kila mtu aliyepata mgawa wa fedha
hizo kuhakikisha analipa kodi ya mapato ya kiasi alichopokea kabla ya
Desemba 31, 2014 huku akipendekeza mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato
(TRA), aliyekosea kuandika kodi sahihi kufukuzwa kazi.
Akichangia taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC), kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) katika Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bungeni jana, Mwigulu
alisema kuwa iwapo kodi hizo zingekatwa kwenye chanzo kilichotakiwa
mambo yasingefika yalipo sasa.
Mwigulu alisema kuwa baada ya kugundua kwamba kuna
kodi ya wananchi haijakusanywa, TRA ilichukua hatua na kupata Sh4.12
bilioni na kwamba fedha hizo zimeshalipwa.
“TRA inaendelea na utaratibu kuhakikisha kuwa hela
hiyo inalipwa na mimi niwahakikishie kuwa hela hiyo italipwa. Kodi
iliyosalia lazima italipwa. Hatuwezi tukawa na mahitaji mengi namna hii,
halafu ikatokea tukaacha kukusanya kodi,” alisema Mwigulu.
Alisema Serikali haiwezi kuacha kodi kubwa namna
hiyo kwa tajiri, halafu ikakimbizana na mama mjane anayeuza mchicha
barabarani na kwamba kila anayehusika ajiandae kisaikolojia.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Tanzania Bara, alisema kwamba taifa litalipwa kodi iliyopotea kutokana
na kukosewa kwa hesabu na kwamba tayari TRA imeshachukua hatua za
kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa serikalini.
“Kuna mtu alipewa kazi yake, badala ya kuandika
Dola za Marekani 6 milioni, msomi aliyesoma kwa kodi za Watanzania
waliojinyima yeye akaenda shule akaandika Sh6 milioni.
Ili kuandika Dola za Marekani 20 milioni, msomi
aliyesoma kwa kodi za Watanzania akaandika Sh20 milioni,” alisema naibu
waziri huyo, huku akishangiliwa na wabunge:
“Namwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania,
kwanza achukue hatua za kinidhamu za ndani kwa waliohusika na kwenye
hili hakuna uchunguzi juu ya uchunguzi.
Uchunguzi umeshafanyika, ameandika Sh20 milioni
badala ya Dola za Marekani 20 milioni, Tanzania imekosa kodi… Hii huwezi
kusema amekosea; ni makusudi. Naagiza wafuate taratibu za ndani za TRA,
lakini na yeye atafute kazi nyingine,” alielekeza.
Mwigulu alisema kuwa kwa kukosekana kodi hiyo kuna
watu waliopoteza maisha kwa kukosekana dawa hospitalini na watoto wa
maskini waliokuwa wamefaulu kukosa mkopo wa kwenda vyuo vikuu.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق