![]() |
| Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Dk Rashid Seif akizungumza na waandishi wa habari Dodoma Hoteli leo |
TATIZO la ukosefu wa dawa katika hospitali kadhaa nchini, limekuzwa mno
kuliko hali halisi na serikali itatoa taarifa rasmi kesho kuelezea tatizo
hilo na hatua ambazo imechukua.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Rashid Seif
wakati akijibu hoja za waandishi wa habari baada ya kufungua Kongamano la
Wanahabari na NHIF mjini hapa.
Dk Seif alisema deni lililopo kwa sasa asilimia 80 ni kulipia gharama za
dawa zilizoletwa kama msaada, lakini ununuzi wa dawa ni asilimia 20 pekee.
Dawa hizo ni kama za ukimwi, kifua kikuu na dawa za malaria.
Alisema kusema hali ni mbaya ni kulinganisha na lipi na dawa za aina gani
na kusema zipo njia tatu za kupata dawa ambazo zimewezesha halmashauri kama
Iramba kuwa na dawa wakati wowote.
Alisema vyombo vya habari vimekuwa vinakuza tatizo hilo ambalo kimsingi si
kubwa hivyo.
Alisema hata hivyo kuwa ni kweli MSD inaidai serikali na ni kweli kuwa kuna
shida ya madaktari, lakini tatizo la dawa sivyo lilivyo.
Alisema kwamba kama Iramba hawana tatizo la dawa kwa nini kwingine kuwa na
tatizo la dawa kama MSD ni ile ile moja.
Awali akifungua kongamano hilo, aliwataka waandishi wa habari kuwa jicho la
tatu la sekta ya afya ili kubainisha changamoto za huduma za afya katika maeneo mbalimbali ambako wanachama wa NHIF na Watanzania kwa ujumla
wanapata huduma hizo.
Aidha aliwataka waandishi wa habari kutumia vyema kongamano hilo kujijenga
na kuelewa masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya kwa lengo la kuhabarisha wananchi ili waelewe.
“Mojawapo ya mambo ya kuzungumzia ni ule mradi wa Udom ambao ukikamilika
utakuwa umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za matibabu nchini
kwa maana ya vipimo vya kisasa na matibabu ya hali ya juu kabisa, na
kuipunguzia Serikali gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu,
‘ alisema na kuongeza kuwa wananchi wanastahili kujua kinachofanywa na
wadau wa afya wakishirikiana na serikali.
Source:Sifa Lubasi, Habarileo Dodoma

إرسال تعليق