Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Profesa Mussa Assad amesema ataanza kazi
kwa moto uleule ulioachwa na mtangulizi wake, Ludovick Utouh
aliyestaafu.
Akizungumza jana mara baada ya kuapishwa na Rais
Jakaya Kikwete Ikulu, Profesa Assad aliyeteuliwa Novemba 5 kushika
wadhifa huo alisema: “Ninasubiri niingie ofisini nianze kazi…
nitaendeleza yote yaliyoachwa na mwenzangu, sitatoka nje ya mstari.”
Profesa Assad alisema yuko tayari kusimamia
utendaji kazi wa kisasa kwa kusimamia misingi ya ofisi yake, ili kulinda
hadhi na heshima aliyopewa na Rais katika uteuzi huo.
Kuhusu Ripoti ya Akaunti ya Escrow, Profesa Asaad
alisema anasubiri kukabidhiwa rasmi taarifa hiyo na maagizo yote
yaliyotolewa na Bunge kwa ajili ya kutekeleza yale yaliyopo chini ya
ofisi yake na kuendeleza yale ambayo yalishaanza kutekelezwa.
Alisema moja ya mambo ambayo atayafanyia tathmini
na kupatia majibu ni kutotajwa moja kwa moja katika Ripoti ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kama fedha za Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco na IPTL ni za umma au
vinginevyo.
Utoh anena
Akizungumza katika hafla hiyo, Utouh alisema kuwa
amemkabidhi Profesa Asaad ofisi yenye watendaji wanaofanya kazi kwa ari
na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.Alisema amefurahishwa na
uteuzi wake na kusema anaamini ataendeleza uwajibikaji na umadhubuti wa
ofisi hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Utouh alimkabidhi Profesa Asaad mwongozo maalumu
wenye kurasa 78 na kueleza kwamba utampa mwelekeo wa namna ofisi hiyo
ilivyo na iwapo kuna upungufu yuko tayari kutoa ushirikiano.
Spika Makinda
Akimzungumzia Profesa Asaad, Spika wa Bunge, Anne
Makinda alisema mtikisiko uliolikumba Taifa kutokana na Kashfa ya Escrow
umelifanya lijenge misingi mizuri zaidi ya kiutendaji na uwajibikaji
katika kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za umma.
Alisema anaamini CAG mpya ataingia na mfumo wa
kisasa zaidi na kusaidia kuweka miundo bora zaidi ya kuhakikisha
kunakuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kusimamia mapato na matumizi
ya Serikali
- Mwananchi
إرسال تعليق