
Viongozi hao walifika kiwandani hapo baada ya
wafanyakazi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na mwekezaji mwenye asili
ya China kugoma kufanya kazi wakidai kuongezewa mshahara.
Katibu msaidizi anayeshughulikia sekta ya viwanda
wa Tuico, Thomas Mkolokoti alisema wameshindwa kufikia makubaliano
kutokana na dharau waliyo onyeshwa na Wachina hao.
Alisema walifika kiwandani hapo kwa lengo la
kuonana na uongozi wa kiwanda ambao haukuonyesha ushirikiano na
kuwaambia wafanye wanachokitaka.
“Tulichofanya, tumezungumza na wafanyakazi warejee
kazini na madai yao ikiwamo kuomba nyongeza ya mishahara tunayafanyia
kazi, ” alisema Mkolokoti.
Baadhi ya wafanyakazi ambao hawakuwa tayari kutaja
majina yao walisema kuna mchezo unachezwa na Wachina hao, kwani
waliahidiwa kulipwa Sh180, 000, badala ya 100,000 wanayolipwa sasa.
“Waziri wa Viwanda wa China alikuja miezi kadhaa
iliyopita na alifanya mkutano hapa hapa kiwandani. Ahadi aliyoitoa ni ya
kutaka tulipwe Sh180,000 lakini cha kushangaza hadi sasa tunalipwa
Sh100,000 kwa mwezi, ” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Ofisa rasilimali watu wa kiwanda hicho, Rigobert Masawe alikataa kuzungumzia suala hilo akidai kuwa afuatwe wakati mwingine.
Wakati viongozi wa Tuico wakitaka kuondoka baada
ya kumaliza kuzungumza na wafanyakazi, mmiliki wa kiwanda aliwafuata na
kuwataka wamwandikie malalamiko hayo kwa maandishi kile walichokubaliana
na wafanyakazi, kitu ambacho kilipingwa na viongozi hao.
Huku akitafsiriwa kile kilichokuwa kikizungumzwa
na Masawe, Mchina huyo alisema lazima aweke kwenye maandishi huku
akimtaka mlinzi aandike kwa madai kuwa anapotakiwa kuwaeleza viongozi
wake wa juu, awaeleze kwa maandishi.
“Hatuwezi kukuandikia chochote kwa sababu wakati
tunakutaka ukae na sisi kuzungumza, ulikuwa unachezea simu na kutuambia
tufanye tunachotaka. Ina maana ulikuwa huna haja ya maelewano.
Tumewarudisha wafanyakazi kazini, lakini tunachukua hatua stahiki,”
alisema Mkolokoti aliyekuwa akijibizana na Mchina huyo.
إرسال تعليق