Ilikuwa wiki ya aina yake, wiki ya mipasho na kila mmoja
ameshuhudia kile kinacholiliwa katika kukabiliana na ufisadi katika
Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo kila mmoja alitamani kuona mwisho wake.
Ni mlolongo mpana hasa baada ya Ripoti ya CAG
kubaini ‘shimo’ lililokuwa limejaaa noti lililokuwa kimbilio la kila
mmoja anayeweza kulifikia. Hatimaye uamuzi wa nini kifanyike umetolewa.
Sitaki kuingia sana kwenye escrow kwa kuwa
timbwili lake linafahamika na kila mmoja anasubiri nini kitafuata baada
ya taarifa ya mwisho.
Japokuwa nimechelewa kuisemea, lakini ninaamini
bado niko kwenye mstari, hili la vito vya tanzanite. kwamba nchi
nyingine zinajivunia ‘ujiko’ wa Tanzania kwa kuongoza duniani kwa madini
yetu wakati sisi wenyewe ni hohehahe.
Wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya vito mjini
Arusha, naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava
na Kamishina wa Madini nchini, Paul Masanja walisema Tanzania inauza
asilimia 20 pekee ya madini ya tanzanite na asilimia 80 iliyosalia
ikiuzwa na Kenya na India.
Tulielezwa kuwa Kenya iliuza tanzanite yenye
thamani ya zaidi ya Sh173 bilioni, India Sh509 bilioni, Tanzania iliuza
Sh48.5 bilioni pekee katika soko la dunia. Kwa kweli nilipigwa na butwaa
kwa hili. Nilishangaa na pengine wapo wanaonishangaa ninaposhangaa.
Lakini sitaacha kusema.
Nilishangazwa na taarifa nyingine ya baadaye kuwa
eti Serikali itatumia Polisi wa Kimataifa (Interpol), kukabiliana na
utoroshaji madini ya tanzanite nje ya nchi.
Haya sasa yanasemwa na mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri wa Madini, Richard Kasesela ambaye anasema Serikali imefikia
hatua hiyo baada ya kuchunguza na kubaini njia na mbinu zote
zinazotumika kutorosha madini hayo nje ya nchi.
“Kuanzia sasa, yeyote atakayekutwa akiuza
tanzanite nje ya nchi bila cheti cha uhalisia kinachothibitishwa
yametoka Tanzania kupitia njia halali, atakamatwa na kurejeshwa nchini
na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi”, ni kauli ya Kasesela
Nilijiuliza, hivi siku zote walikuwa wapi hadi leo
kukumbuka hayo ya Interpol? Inawezekana pia Interpol wakawa hawajui a,
b, c ya kinachoendelea pamoja na kauli za kutia matumaini kutolewa na
ikawa siasa tu.
Kwa jinsi ninavyoamini, hawajaambiwa waanzie wapi,
na si kwa madini hayo pekee, kuna madini mengi yanatoroshwa. Kuna tani
na tani za mchanga wa madini tunaambiwa zinakwenda kupembuliwa huko,
sisi tunabaki na mashimo.
Hivi mtu avune mpunga shambani kwako, halafu anakwambia atafanya kazi ya kukoboa kisha akuletee mchele, si utaletewa pumba?
- Mwananchi
- Mwananchi

إرسال تعليق