
Mshambuliaji Dan Sserunkuma
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kutolewa ripoti zisizo rasmi za Sserunkuma kutua Simba, jana Gor Mahia ilitoa taarifa rasmi ikiweka wazi kwamba mkataba wake na klabu hiyo uko karibu kumalizika na amekataa kusaini mkataba mpya.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Gor Mahia, Chris Omondi, mshambuliaji huyo amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea na mabingwa hao wa KPL kwa vile amepata ofa nono kutoka Simba, ambayo Gor hawakuwa na jinsi ya kumpa zaidi ya kumwachia atue kwa klabu hiyo ya Tanzania.
Wakala wa Sserunkuma, Ken Joseph, ameshaweka wazi kuondoka Gor Mahia kwa mteja huyo na Omondi, katika mahojiano na mtandao rasmi wa KPL jana, ameeleza kuwa presha ya wakala wake pia imechangia kuondoka kwa mchezaji huyo katika klabu yao.
"Sserunkuma anaondoka na uzuri wake. Tumejitahidi kumshawishi aendelee kubaki na kufanya kazi hapa wakati tukiangalia namna ya kumpa mkataba mzuri lakini Simba wamempa ofa nzuri zaidi ambayo hatuwezi kuifikia kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayotukabili.
"Ukweli wa udhaifu wetu katika suala hili ni matatizo ya kiuchumi ambayo yametufikisha hapa tulipo kwa sasa. Tumejitahidi kunasa saini yake lakini kimefika kipindi ambacho hatuwezi kukubaliana naye.
"Anajua kilichokuwapo mezani na wakala wake alikuwa shingo upande kusaini ofa ya Simba; baadaye tumempoteza. Alisema alikuwa hajasaini Simba, lakini sikumuona kama alikuwa tayari kuikataa ofa yao," alisema.
Sserunkuma amekaa kwa miaka miwili na nusu Gor Mahia baada ya kujiunga nayo akitokea Nairobi City Stars.
Gor Mahia pia iko mbioni kumpoteza kiungo fundi Geofrey Kizito ambaye amesema ana mpango wa kutimkia Vietnam kucheza soka la kulipwa.
Ujio wa Sserunkuma Simba umesababisha kuondolewa kikosini kwa aliyekuwa mchezaji mwenzake Gor, mshambuliaji Mkenya Paul Kiongera kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata katika dakika ya 88 ya mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu waliyotoka sare ya mabao mawili dhidi ya Costal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Septemba 21, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق