Dawasco yaidai Serikali Sh15bilioni

Dar es Salaam. Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amezishambulia mamlaka za maji, Dawasco na Dawasa kwamba zimekuwa vinara wa kupoteza maji kwa asilimia 56 kutokana na uchakavu wa miundombinu yao jambo ambalo linawaathiri wananchi.
Kauli hii imekuja huku kukiwa na taarifa kwamba Mamlaka za Maji nchini zinaidai serikali Sh15 bilioni,fedha ambazo zingelipwa zingeweza kusaidia katika kukarabati miundombinu chakavu.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Maji ya Kitaifa ya mwaka 2013/2014, Prof Maghembe  anasema ili umefika wakati ambapo mamlaka zote zibadilike katika utendaji wake wa kazi, huku zikitafuta vyanzo vipya vya maji ili kuhakikisha wanawahudumia wateja wengi  hasa jijini Dar es Salaam ambako kuna wahitaji zaidi ya milioni 3.6 ambapo kwa sasa wanafikia watu 100,000.
Profesa Maghembe ameziagiza mamlaka hizo kuhakikisha kuwa inatafuta mbinu mbadala wa kudhibiti upotevu wa maji ambayo wananchi wanayalipia bila kupatikana jambo ambalo alisema kuwa ni wizi wa mchana kweupe.
“Upotevu wa maji unafikia asilimia 56, hii ni rekodi mbaya,  tutachukua hatua ya kuhakikisha kwamba mashirika haya yanabadilika kabisa, Dawasa liwe shirika la uzalishaji wa maji na usafirishaji wa maji, kutoka kwenye vyanzo mpaka yafike kwenye Wilaya za Dawasco,” alisema na kuongeza:
“Dawasco ikishapokea maji kwenye Wilaya zake na yenyewe itakuwa kazi yake kubwa ni kuyasambaza maji hayo kwa wateja, kuhakikisha kwamba  wateja wanaohitaji maji wanayapata. Anasema Profesa Maghembe
Aidha Maghembe alikubaliana na deni la Serikali la Sh15bilioni inayodaiwa na Mamlaka za maji na kusema kuwa suala hilo linashughulikiwa ili kuzipunguzia mzigo Mamlaka hizo.
“Tumejaribu sana kulishughulikia suala hili lakini inaonekana kama hakuna mtu anayetusikiliza, mamlaka hizi ni ndogo ndogo sana na biashara hii wanayoifanya kwa nchi nzima kwa mwaka mmoja haifikii Sh100 bilioni,” anasema Prof Maghembe

Post a Comment

أحدث أقدم