Rais Uhuru Kenyatta asaini sheria ya Usalama


Pamoja na kuwapo kwa vuta nikuvute jana katika Bunge la nchini Kenya Rais Uhuru Kenyatta, amesaini na kuiidhinisha sheria mpya ya usalama ambayo inawezesha majasusi kunasa mawasiliano kisiri au kufanya udukuzi pamoja na kuwazuia washukiwa wa ugaidi kwa mwaka mmoja kabla ya kuwafungulia mashitaka.
Kenyatta anasema sheria hiyo mpya ni muhimu nchini Kenya kwa sasa kwani inahitajika kwa ajili ya kukabiliana na tisho la ugaidi kutoka kwa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Al Shabaab.
Akisaini sharia hiyo mpya Kenyatta amesisitiza kuwa sheria hio haikiuki haki za binadamu wala kuwapokonya watu uhuru wa kujieleza.
Mnamo siku ya Alhamisi (jana), wabunge wa serikali na wale wa upinzani walipigana na kurushiana maneno makali bungeni wakijadili marekebisho kwenye mswaada huo kabla ya Rais kuupitisha kuwa sheria.
Katika vurugu hizo mmoja wa wabunge wa upinzani alimmwagia maji naibu spika.
Sheria hizo mpya zilipitishwa na bunge licha ya pingamizi kubwa na vurugu kutoka kwa wabunge hao wa upinzani.
Vyombo vya habari vimesema nchini humo pia vimepiga kelele vikieleza kuwa baadhi ya vipengee vya sheria hiyo vinabana uhuru wa vyombo vya habari na hata kutishia kwenda mahakamani .
Mswada huo kabla ya kutiwa saini na kufanywa sheria,ulifanyiwa mabadiliko kadhaa katika vipengee ambavyo vilionekana na baadhi ya wabunge kama vilivyokua vikali na kwenda kinyume na katiba.
Polisi sasa watakuwa na jukumu la kuidhinisha taarifa au picha za uchunguzi wa maswala ya usalama na hasa kuhusiana na ugaidi.
Polisi pia ndio watapaswa kuidhinisha picha za waathiriwa wa ugaidi kabla ya kuchapishwa au kuonyeshwa katika vyombo vya habari.
Vyombo vya habari vinasema haya yanakwenda kinyume na uhuru wa vyombo vya habari.

Post a Comment

أحدث أقدم