Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema, inatarajia kukutana kwa dharura kujadili uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hatua hiyo inatokana na malalamiko kutoka kwa
wapigakura, wagombea na vyama mbalimbali vya siasa kuhusu kuvurugika na
kutofanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo kutokana na kasoro
mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika
alisema jana kuwa baada ya hujuma na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi
huo, kamati kuu itakuja na mapendekezo ya nini cha kufanya.
“Kikao hicho kitakuja na maazimio juu ya hatua za
kuchukua dhidi ya Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) mwenye dhamana ya Tamisemi
ambao wamevuruga uchaguzi huu. Hata katika maeneo ambayo uchaguzi
umeahirishwa kama Ukawa tutashirikiana kuhakikisha tunaiondoa CCM licha
ya vitendo vya kuhujumu uchaguzi unaofanywa na viongozi wa CCM na wakati
mwingine kwa kulitumia Jeshi la Polisi,” alidai Mnyika.
Ushindi wa Chadema
Kuhusu ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo,
Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Tumefanya vizuri
nchi nzima. Kwa mfano, mwaka 2009 Dar es Salaam yote tulikuwa na mitaa
saba tu lakini leo hii mpaka sasa jimbo moja tu la Ubungo tumeshinda
mitaa 23, unaweza kuona tunavyopiga hatua.
“Mwaka 2009, CCM walishinda kwa asilimia 96 na
upinzani tulikuwa tunagawana asilimia nne, sasa leo hii katika maeneo
mbalimbali tumefanya vizuri licha ya hujuma na hila zinazofanywa na CCM.
Baadhi ya maeneo ambayo wanatoka mawaziri, Chadema tumeshinda hivyo
wakitaka kutatuliwa matatizo yao tutawatatulia na tunawaahidi
kuwatumikia vizuri bila upendeleo.
“Jimbo la Tundu Lissu la Singida Mashariki ambalo
CCM wamekuwa wakisema watalichukua, kati ya vijiji 43, vijiji 41
tumevichukua na CCM wameambulia viwili, Kyela mwaka 2009, tulikuwa na
mitaa miwili lakini leo tuna mitaa zaidi ya 28.”
Vyama vingine
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
licha ya uchaguzi huo kutawaliwa na hila na kila aina ya uchakachuaji
wa matokeo, bado vyama vya upinzani vimefanya vizuri.
Post a Comment