Kamati Kuu Chadema yaitwa kujadili uchaguzi

http://api.ning.com/files/u325ipbpd7r-kGNxS-ZQtkx4eFXm5fWrwUJn*8gpHLPpR70VW9*zKkNj770Nsry*zxxADjyAkhvcr9fnzNHhiStkEYnYUyz2/chadema.pngDar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema, inatarajia kukutana kwa dharura kujadili uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hatua hiyo inatokana na malalamiko kutoka kwa wapigakura, wagombea na vyama mbalimbali vya siasa kuhusu kuvurugika na kutofanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo kutokana na kasoro mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema jana kuwa baada ya hujuma na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi huo, kamati kuu itakuja na mapendekezo ya nini cha kufanya.
“Kikao hicho kitakuja na maazimio juu ya hatua za kuchukua dhidi ya Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) mwenye dhamana ya Tamisemi ambao wamevuruga uchaguzi huu. Hata katika maeneo ambayo uchaguzi umeahirishwa kama Ukawa tutashirikiana kuhakikisha tunaiondoa CCM licha ya vitendo vya kuhujumu uchaguzi unaofanywa na viongozi wa CCM na wakati mwingine kwa kulitumia Jeshi la Polisi,” alidai Mnyika.
Ushindi wa Chadema
Kuhusu ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo, Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Tumefanya vizuri nchi nzima. Kwa mfano, mwaka 2009 Dar es Salaam yote tulikuwa na mitaa saba tu lakini leo hii mpaka sasa jimbo moja tu la Ubungo tumeshinda mitaa 23, unaweza kuona tunavyopiga hatua.
“Mwaka 2009, CCM walishinda kwa asilimia 96 na upinzani tulikuwa tunagawana asilimia nne, sasa leo hii katika maeneo mbalimbali tumefanya vizuri licha ya hujuma na hila zinazofanywa na CCM. Baadhi ya maeneo ambayo wanatoka mawaziri, Chadema tumeshinda hivyo wakitaka kutatuliwa matatizo yao tutawatatulia na tunawaahidi kuwatumikia vizuri bila upendeleo.
“Jimbo la Tundu Lissu la Singida Mashariki ambalo CCM wamekuwa wakisema watalichukua, kati ya vijiji 43, vijiji 41 tumevichukua na CCM wameambulia viwili, Kyela mwaka 2009, tulikuwa na mitaa miwili lakini leo tuna mitaa zaidi ya 28.”
Vyama vingine
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema licha ya uchaguzi huo kutawaliwa na hila na kila aina ya uchakachuaji wa matokeo, bado vyama vya upinzani vimefanya vizuri.

Post a Comment

أحدث أقدم