Tamisemi: Waliovuruga uchaguzi sasa kukiona

Dar es Salaam. Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), imeiagiza mikoa yote nchini kuwasilisha taarifa kuhusu kasoro zilizojitokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa juzi ili iwachukulie hatua watendaji watakaobainika kuhusika.
Imesema kushindwa kusimamia uchaguzi na kusababisha kasoro, ni moja ya makosa makubwa na kuwa watakaobainika, watachukuliwa hatua kali kulingana na uzito na kiwango cha kuhusika kwao na kwamba wanaweza kufukuzwa kazi, kuvuliwa madaraka, kushushwa cheo au kukatwa mishahara.
Uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi na kuahirishwa katika baadhi ya maeneo kutokana ama kukosekana kwa majina ya wagombea, baadhi yao kuwekewa nembo za vyama wasivyotoka au uhaba wa vifaa vya kupigia kura.
Hata hivyo, halmashauri 145 kati ya 162 zilizofanya uchaguzi huo hazikuwa na dosari, tatu hazikufanya uchaguzi kabisa kutokana na vifaa kuchelewa, 14 zilikuwa na kasoro katika baadhi ya vijiji, vitongoji na mitaa na uchaguzi wake kuahirishwa mpaka Desemba 20 na 21. Akitoa taarifa ya awali ya uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema pamoja na kasoro hizo, uchaguzi huo umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80.
“Katika uchaguzi huu hakukuwa na vitambulisho vya mpigakura kama ilivyo katika Uchaguzi Mkuu. Uchaguzi huu unafanyika katika mtaa au kitongoji hivyo ni rahisi watu kutambuana na pia mtu akishapiga kura si rahisi kurudia mara ya pili na tuliagiza mpigakura awe ama na kitambulisho cha kazi, leseni au kile cha kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kutambulika,” alisema.
Alisema malalamiko na kasoro zilizoripotiwa katika vyombo vya habari haziwezi kujibiwa wala kutolewa ufafanuzi na Tamisemi hadi baada ya kupata ripoti kutoka mikoani.
Akizungumzia malalamiko ya wananchi kutoyaona majina yao, Ghasia alisema ulitolewa muda wa siku tatu kwa wananchi kufanya uhakiki lakini wengine hawakufanya hivyo.
“Kuhusu majina kubadilishwa au kuisha kwa wino na kukosekana kwa vitu vidogovidogo hilo linaweza kuwa limefanyika kutokana na uzembe tu. Ndiyo maana tumeagiza tupewe taarifa rasmi.”
Akizungumzia kasoro zilizobainika katika karatasi za kupigia kura, alisema utaratibu wa kuandaa vifaa hivyo ulikuwa ukifanywa na halmashauri husika na si Tamisemi, hivyo ni vigumu kwa wizara hiyo kuagiza walioandaa vifaa wachukuliwe hatua.
“Mfano Temeke na Ilala walimtumia Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Awali, aliwapelekea vifaa vyenye matatizo, hata walipovirejesha ili avirekebishe, vilirudishwa vikiwa bado na kasoro. Mpiga Chapa aliingia mkataba na manispaa na ndiyo aliyepewa zabuni,” alisema.
Alisema suala hilo linafanyiwa uchunguzi ili kubaini kama kasoro katika wilaya hizo zimesababishwa na Mpiga Chapa wa Serikali au wilaya husika.
Alipotafutwa mpiga chapa mkuu wa serikali, Cassian Chibogoyo kuzungumzia kuhusu tuhuma za ofisi yake kuwa sehemu ya dosari za uchaguzi katika manispaa za Ilala na Temeke, alisema tuhuma amezisikia na kwamba atawasiliana na wizara kabla ya kutoa majibu yake leo.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم