KILAINI, NZIGIRWA, TWIMANNYE NITAUNGAMA NIKIWATAZAMA USONI

Baba Askofu Methodius Kilaini akitoa huduma kanisani.
UKIHOJI dhambi za viongozi wa dini harakaharaka utaambiwa fuata mafundisho yao usifuate matendo. Hili ni kinyume na Mtume Paul aliyefundisha waumini wake kuwa wamfuate yeye kama alivyomfuata Yesu.
Kwa kuwa dini ni muhimu kwenye kaya yangu sibishi sana katika hilo, lakini kuhusishwa kwenye fedha chafu kwa viongozi wa dini Askofu Methodius Kilaini, Euesebius Nzigirwa na Alphonce Twimannye kumenibadilisha mtazamo.
Sikuwahi kuuliza utakatifu wa viongozi hao wa dini kwa sababu za kutofuata matendo yao; lakini sakata la ufisadi wa Escrow wa zaidi ya shilingi bilioni 300 limenifanya nijiulize kimoyomoyo watawa hawa walipewa fedha hizo kwa ajili ya kazi gani?
Swali hili lipo na litaendelea kuwepo kwa sababu Mkuu wa Kaya sijapata majibu ya msingi. Kwa hali  hiyo, hata nitakapokwenda kuungama dhambi zangu mbele ya watumishi hao wa Mungu nitakuwa nawatazama usoni.
Ukweli ni huo; nitakuwa natubu dhambi zangu lakini wakati huohuo nayauliza mapaji ya uso ya viongozi hao kulikoni wakajichotea mamilioni ya fedha ambazo hazina utakaso? Nitafanya hivyo kwa sababu utetezi unaoenezwa juu ya watawa hao kuhusu kupewa fedha za Escrow haujanikata kiu. Nafikiri siyo mimi tu, ni pamoja na wanazengo wenzangu katika kaya hii.Askofu Euesebius Nzigirwa(wa pili kulia) akiingia kanisani.
Wapo wanaosema kuwa viongozi hao wa dini walipewa mamilioni hayo kama sehemu ya sadaka. Swali langu; lini sadaka ya kanisa akapewa kasisi na siyo kuwekwa kwenye kapu la makusanyo kanisani?
Nasisitiza; nitaungama nawatazama usoni. Nitafanya hivyo kwa sababu hata kama wao ni sehemu ya kanisa na kwamba inawezekana walitumwa kidini kupokea fedha hizo, vipi kanisa husika halijatoa kauli ya kutambua sadaka hiyo mpaka leo?
Hahaha...inachekesha kiasi pale wengine wanapoibuka na utetezi kuwa, watumishi hao wa Mungu walipewa fedha hizo kama msaada wa kiutu. Swali; msaada kwa ajili ya dhiki gani wanazokabiliana nazo watawa hao waliopewa kibali na maandiko kuwa wale kupitia huduma zao.
Kama nilivyosema; sitaacha kutubu kwao kwa sababu ya umuhimu wa ibada lakini suala la kuwatazama usoni sitaliacha mpaka nitakapopewa mantiki ya kutofanya hivyo. Nafikiri hata mjukuu wangu mkubwa kaniambia anasubiri jibu.
Hata kama sikusoma sana mambo ya dini lakini najua kuwa huduma za kiroho hutolewa bure, hivyo kuifanya sababu ya kuwepo kwa malipo ya kiroho kukosa mashiko. Na isitoshe maandiko yanaonya kuwa huwezi kutumikia mabwana wawili kwa maana ya Mungu na mali. Hii ina maana kwamba, siyo sahihi pia kwa watawa kuwa ‘wachuuzi’ kwa kisingizio cha kupata fedha za kusaidia waumini wao, kwa sababu kazi ya ulezi ni ya kanisa kuu siyo padri wala askofu pekee.
Kwa hoja hizo msimamo wangu ni kuwa, nitakwenda kanisani, ila wakati wa kuungama nitakuwa nawatazama usoni wanaoniungamisha madhambi yangu ya ulevi, matusi, wivu na chuki.
Nitafanya hivyo huku najiuliza wanitoweje kibanzi kwenye jicho langu wakati wao wana boriti machoni? Mkuu wa Kaya nimeishiwa uvumilivu katika hili; wakitaka nifute msimamo wangu wajitakase na wao kwenye sakata la Escrow bhaanaaa!
Kama hilo halitoshi, kwa kuwa mimi ni Mkuu wa Kaya namuomba sana mkuu wa kanisa atoe tamko kuhusu watumishi hawa wa Mungu ambao hawakutajwa kwenye adhabu zilizopendekezwa na bunge, ambapo mimi nawasilisha maazimio ya wananzengo wenzangu kuwa,  viongozi hao wa dini wavuliwe nyadhifa zao. NA HOJA HIYO IMEUNGWA MKONO!

Post a Comment

Previous Post Next Post