Dar/mikoani. Kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow inayoendelea kulitingisha Taifa, jana ilitawala mahubiri
ya Sikukuu ya Krismasi katika makanisa mbalimbali nchini, viongozi wa
dini wakionyesha kutoridhishwa na maelezo na hatua zinazochukuliwa.
Wakihutubia waumini wao, viongozi hao walitumia siku hiyo kukemea vitendo vya ufisadi, wizi na uzembe.
Hofu ya Escrow
Ujumbe wa Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika
(DCT) wa Kanisa la Anglikana, Dk Dickson Chilongani ulilenga kueleza
hofu ya wananchi kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ugumu
wa maisha, ukosefu wa ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu
na elimu pamoja na wimbi la viongozi waandamizi wasiokuwa waaminifu na
waadilifu.
Akihubiri katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu
mjini Dodoma, Askofu Chilongani alisema mbali na maisha ya ufukara na
ukosefu wa huduma, sakata la Escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
aliyoitoa Jumatatu vimezidi kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya
waonekane kama hawana tumaini.
Akitumia mtindo wa kuhoji, Askofu Chilongani
alianza kwa kuhoji, “Kitu gani kinakutia hofu unaposherekea sikukuu hii,
watu wengi tunaishi katika ulimwengu wa hofu kutokana na ufukara,
ukosefu wa huduma, tunajiuliza tutawasomeshaje watoto wetu, tutapataje
huduma bora za matibabu, yaani kila mmoja wetu ana hofu,” alisema.
Askofu Dk Chilongani alisema ingawa kila mtu ana
hofu yake lakini sakata la akaunti ya Escrow limejenga hofu kwa
mwananchi, kila mmoja akihoji na kutengeneza majibu yake jambo linalotoa
picha kuwa jibu sahihi halijatolewa au kupatikana.
“Mimi siyo mwanasiasa wala mtaalamu wa masuala ya
siasa lakini kuna hili sakata la Escrow ambalo juzijuzi Rais amelitolea
ufafanuzi, hili nalo linazidi kuwajengea wananchi hofu, wengine
wanakosoa maazimio ya Bunge, wengine wanataka Serikali itoe maamuzi
yenye tija kwa umma, yaani ni hofu tu,” alisema.
Escrow ni fedha za umma
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo
alisisitizia kuwa fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ni
mali ya umma kutokana na taarifa iliyowasilishwa na PAC bungeni.
Kauli hiyo inakuja baada ya Rais Kikwete kusema
fedha hizo ni mali Kampuni ya IPTL na zilikuwa Sh202 bilioni na si Sh306
bilioni kama inavyodaiwa.
Akihubiri katika kanisa hilo jana, Lusekelo
maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema: “Niliisikiliza kwa makini mwanzo
hadi mwisho (hotuba ya Rais) leo nimeona niseme machache kwamba fedha
hizo ni mali ya umma. Mimi siungani na hao wanaodai fedha hizi siyo za
umma lakini kwa hali hii hakuna jinsi inabidi tumwachie Mungu maana yeye
ndiye atakayeweza kutuvusha kutoka hapa tulipo,” alisema.

Post a Comment