Kamati ya Bunge yaikalia kooni Tanapa

Arusha. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limetakiwa kutekeleza agizo la Serikali la kusimamia Msitu wa Asili wa Mlima Meru ili kuboresha uoto wa asili, badala ya msitu huo kuendelea kuwa chini ya Wakala Msitu Tanzania (TFS).
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alitoa agizo hilo, juzi wakati kamati hiyo ilipokuwa ikifanya hitimisho baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha ulipo msitu huo.
Lembeli alisema tangu 2005, kupitia Gazeti la Serikali, GN 280, iliagizwa msitu huo kuwa chini ya Tanapa, inashangaza kuona wakala wa msitu nchini umekuwa ukikaidi mpango huo.
“Kuanzia sasa, tunaitaka Tanapa kusimamia msitu huu bila kuingilia maeneo ya Chuo cha Sokoine na Chuo cha Msitu cha Olmotonyo kwa lengo moja tu la kuendelea kuhifadhi uoto wa asili wa msitu huu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema Lembeli.
Alisema kuna umuhimu kwa Serikali hasa Wizara ya Maliasili na Utalii kuingilia kati na kutatua mgogoro huo ili kuhakikisha Tanapa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha unautunza msitu huo na kusitishwa mpango wa uvunaji miti.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mgimwa alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Bunge na kusema utaratibu utazingatiwa kwa masilahi ya Taifa.
“Tutatekeleza haya tuliyoagizwa na kamati,” alisema.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post